
Arusha. Amani ya Tanzania ili iendelee kudumu, viongozi wa Serikali wametakiwa kuongeza kiwango cha uvumilivu na kuepuka matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa baadhi ya watu wenye mitazamo tofauti.
Aidha, wametakiwa kutenda haki kwa watu wanaowaongoza, na pale wanapotofautiana kujenga tabia ya kutumia njia ya mazungumzo kwa ajili ya kumaliza tofauti zao.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa, Aprili 18, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa Makanisa ya Pentekoste Arusha (CPCT), Askofu Ayoub Muna, kwenye ibada ya Ijumaa Kuu ya Pasaka ya Umoja wa Kanisa Mkoa wa Arusha (Ukama).
Amesema kuwa ujumbe wa Pasaka mwaka huu ni ‘toleo la amani kwa watu wote’ na kuwa ni jukumu la kila mmoja kwa nafasi yake kulinda amani na kutoa mchango kwa kusali ili amani iendelee kutawala.
“Tuvumiliane kwa sababu Watanzania wamezaliwa wa aina mbalimbali, kuna wenye akili nzuri, upungufu, na wengine wanafikiria maisha yao binafsi.
Ili amani ya Tanzania iendelee kudumu, kunahitajika viongozi wa wananchi kuongeza kiwango cha kuvumiliana na Watanzania ambao wametofautiana nao katika mitazamo yao. Katika kulinda amani yetu, tusitumie nguvu iliyopitiliza,” amesema makamu huyo na kuongeza;
“Moto hautawaka Tanzania sababu Mungu ameweka viongozi wa kiroho. Unajua, ukishindana na mtu anayekupinga wewe na kutumia nguvu kubwa, anaweza kuwa mashuhuri kukushinda wewe. Tutumie nguvu kidogo, tusimwage petroli katika nchi yetu. Usipige mbu kwa kutumia rungu, utapasua TV.” ameongeza.
Kuhusu haki, Askofu huyo amewataka viongozi kutenda haki kwani wanapoitendea jamii haki, wanabaki kwenye mioyo yao.
“Sisi watumishi wa Mungu tumepewa jukumu la kuhubiri amani, na Watanzania waungane kwani amani ikiondoka ndiyo tutajua umuhimu wake. Najua ninaweza kupewa majina mengi, naweza kuambiwa mimi ni chawa, na siku hizi wanasema tunatafuta posho, si kweli,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Ukama, Askofu Isaac Amani wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, amesema ili kulinda amani, hasa wakati Taifa linapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, ni muhimu maandalizi yakafanyika, ikiwa ni pamoja na mazungumzo kufanyika badala ya kutishiana.
“Tunaombea maandalizi sahihi ya uchaguzi mkuu ulio mbele yetu. Maandalizi ya amani yatazaa amani ili tuponye taifa kwa kuliweka mbele kwanza amani tuliyonayo, tusiichezee ikaondoka, kwani hakuna hata mmoja atakayenufaika na kuondoka kwa amani.
“Mazungumzo yafanyike, kutishiana kuondoke. Nia njema ionekane, kwani ukiotesha embe utavuna maembe, ukiotesha michongoma utavuna michongoma. Tuangalie usalama, kamati za maridhiano ziundwe, watu wazungumze,” amesema Askofu huyo.
Akitoa salamu za Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema amewaomba viongozi wa dini mkoani humo kuendelea kufundisha ukweli bila woga na kutoogopa kusema ukweli.
Kuhusu uchaguzi, amesema watumishi wa Mungu waseme waliyoyasikia kutoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu aliyowapa kuyanena ili waliponye taifa.
“Mimi huwa nawaonea wivu watumishi wa Mungu kwa sababu mnayemtumikia ndiye Alfa na Omega, kwake kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri. Naomba msisite kutufundisha viongozi wa Serikali, msiogope kutuambia ukweli.
“Nitawalinda viongozi wa dini katika mkoa wangu ili wafundishe kweli bila woga. Cheo ni cha muda tu. Hata ukiminya haki za watu, ni suala la muda tu,” amesema.