Haki, amani vitawale uchaguzi leo

Leo nchi yetu inahitimisha safari ya siku 104 tangu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa alipotoa tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa Watanzania wenye sifa kutumia haki yao kupiga kura leo.

Tunafahamu vituo vya kupigia kura kuchagua mwenyekiti wa kijiji, mtaa na kitongoji pamoja na wajumbe wa halmashauri ya maeneo hayo, vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni na baada ya hapo kutakuwa na muda wa kuhesabu kura hadi kutangaza matokeo.

Ni hitaji na maombi yetu kuwa haki, amani vitawale katika kipindi chote hicho.

Tunayasema haya kwa kutambua kuwa amani siku zote ni tunda la haki, hivyo wakati tukiwasihi Watanzania, wagombea na viongozi wa vyama vya siasa kudumisha amani, tunatoa rai kwa wasimamizi na wasaidizi wao kutenda haki katika uchaguzi huu.

Tunafahamu safari ya siku 104 ilipita katika milima na mabonde. Hiyo ni kama kula ng’ombe mzima, na hivyo hatuoni sababu watu washindwe kumalizia mkia, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha haki inatamalaki katika muda wote uliosalia.

Leo ni siku ambayo chombo kinachosimamia uchaguzi huu- Tamisemi- kinapaswa kuonyesha uadilifu na weledi na kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya Watanzania kuwa uchaguzi umekuwa ukiharibiwa mikononi mwake.

Dhana hii imejengeka nchini na kumekuwepo kauli zinazoipa nguvu, kama ile ya goli la mkono au kwamba matokeo ya kura sio lazima yawe yale ya kwenye sanduku la kura, bali inategemea nani anayehesabu na kutangaza matokeo.

Kwa hiyo Watanzania wanapokwenda katika vituo kwa ajili ya kupiga kura, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wajitahidi kutenda haki ili wagombea wote na mawakala wao waondokane na hofu waliyonayo.

Pale kunapojitokeza kupishana lugha kati ya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi na mawakala wa vyama vya siasa juu ya jambo lolote katika kituo, basi busara na hekima vitumike ili kuhakikisha mgogoro huo unamalizwa kwa njia ya amani.

Tunafahamu kusipokuwa na umakini na kila upande ukaona haki haitendeki, kunaweza kuibua vurugu na hata umwagaji damu, jambo ambalo linaweza kuepukwa kwa kutumia busara na hekima kwa kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na pia ni vema kama Watanzania tuendelee kucheka na kusalimiana.

Tunawasihi wapigakura wajitokeze katika vituo na kupiga kura na kusiwe na visingizo vyovyote, kwani Serikali ilishatangaza leo ni siku ya mapumziko.

Ni rai yetu pia kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha linatekeleza wajibu wake kwa weledi, maadili na bila kuonyesha chembe ya upendeleo wowote na lijizuie matumizi ya nguvu bila sababu, bali lisimamie usalama na taratibu zitakazowezesha haki itendeke na matokeo yatangazwe bila mikwaruzano.

Tunatamani pia kuona waandishi wa habari watakaokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kuuhabarisha umma, hawawekewi vikwazo visivyo na sababu wakati wa upigaji kura, uhesabuji kura na utangazaji wa matokeo vituoni.

Uchaguzi huu utakuwa wa haki, huru na unaoaminika iwapo kila anayehusika atatekeleza wajibu wake aliokasimiwa kisheria kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazousimamia.

Kila mmoja ajione ni mshindi kwa kuufanya uchaguzi huu kuwa ni wa huru na haki na unaoaminika na kukubalika na umma ili kudumisha amani tuliyonayo.