HADITHI: Kwa Mtutu wa Bunduki – 4

ALIPOONDOKA Tegeta, Temba alielekea Segerea. Aliegesha gari nje ya gereza hilo akaelekea kwenye lango la kuingilia gerezani. Askari wa magereza waliokuwa kwenye lango hilo walikuwa wakimtambua wakampisha apite.

“Karibu afande.” Askari mmoja alimkaribisha.

“Asante. Mkuu wa gereza nimemkuta?”

“Ndiyo yupo ofisini kwake.”

“Nakwenda kumuona mara moja.”

“Sawa afande.”

Temba alikwenda moja kwa moja ilipokuwa ofisi ya mkuu wa gerea hilo. Alipoingia ofisini humo alimkuta mkuu wa gerea akisoma gazeti.

“Heshima yako mkuu.”

“Nashukuru sana. Karibu.”

“Asante.”

Temba akakaa kwenye kiti.

“Habari ya kazi?”

“Nzuri. Sijui wewe.”

“Kuna tatizo kidogo. Kuna mfungwa mmoja aliyehukumiwa kifungo cha miaka thelathini mwezi Novemba mwaka jana, anaitwa Christian Bambo.”

“Ndiyo Bambo, tuko naye.”

“Huyu mtu bado anatumikia kifungo hicho?”

“Ndiyo, bado anatumikia kifungo chake.”

“Kuna uhalifu uliotokea hii leo. Kuna watu walitekwa nyara na wamemtambua mmoja wa watekaji kwa kutumia picha za wahalifu tulizonazo. Wametuonyesha picha ya Bambo na kutuambia yeye ndiye aliyekuwa akiendesha gari lililowateka.”

Mkuu wa gereza akatikisa kichwa.

“Huyo mtu tuko naye. Kama utapenda kumuona naweza kumuagiza askari amlete umuone.”

“Hiki kitu kimenichanganya kidogo.”

“Watu wanaweza kufanana.”

“Kufanana gani kwa kiwango hicho? Bambo ninayemfahamu mimi ana mshono juu ya jicho lake la kushoto na huyo ameelezwa pia ana mshono kama huo. Watu wanaweza kufanana sura na sio alama zilizomo kwenye miili yao.”

“Ngoja nimwagize askari aje hapa umuone.”

Mkuu wa kituo akainua mkono wa simu na kuipiga. Simu ya upande wa pili ilipopokewa, alisema.

“Mtume askari amlete Bambo ofisini mwangu.”

Baada ya kusema hivyo akaurudisha mkono wa simu mahali pake.

“Ataletwa sasa hivi.”

“Nilidhani labda alikata rufani akaachiwa.”

“Hapana. Baada ya kifungo hicho hakukata rufani.”

Baada ya dakika chache, askari wa magereza akaingia ofisini humo akiwa amefuatana na Christian Bambo.

Temba alipomuona alisema.

“Kweli bado mko naye.”

“Huyo anayesemwa atakuwa siye huyu.” Mkuu wa gereza akasema.

“Nashukuru sana kwa kunithibitishia hilo.”

Inspekta Temba alipoondoka kwenye gereza hilo alikwenda Sinza ilikokuwa Tamasha Night Club. Kulikuwa na msichana mmoja aliyekuwa akiitwa Suzana ambaye alikuwa akifanya kazi hapo. Msichana huyo alizaa na jambazi Simon Kumbo ambaye picha yake ilitambuliwa na Mkwetu kuwa ni miongoni mwa watu waliowateka nyara.

Suzana ambaye alikamatwa mara kadhaa na kuhojiwa na polisi kuhusu mahusiano yake na Simon na pia kutakiwa kueleza mahali alipo Simon, mara zote amekuwa akisisitiza kuwa alishaachana na mwanaume huyo na kwamba alikuwa hafahamu mahali aliko.

Hata hivyo, Temba alijiambia kwa vile Simon alikuwa amezaa naye, ni lazima watakuwa wanakutana. Na kama waliachana kweli huenda wamerudiana kwani tangu Suzana alipodai kuwa waliachana ilishapita miaka mitatu.

Wakati Temba akiendesha gari aligundua kuwa kulikuwa na gari iliyokuwa ikimfuata kwa nyuma. Hakujua gari hilo lilianza kumfuata kutoka wapi lakini aligundua lilikuwa likimfuata yeye.

Ulikuwa uzoevu wake wa kikachero uliomfanya agundue kuwa gari hilo lilikuwa likimfuata yeye. Mara moja akashuku huenda gari hilo lilikuwa linamfuata kumchunguza nyendo zake.

Temba alijiambia huenda walikuwa watu waliomteka Myra waliokuwa wakimfuatilia. Hata hivyo, Temba aliendelea na safari yake ya kuelekea Tamasha Night Club.

Laiti angetambua dhamiri ya watu waliokuwa wakimfuata na nini kingetokea pindi gari hizo zitakapokaribiana, Temba angeacha kwenda Tamasha na angerudi makao ya polisi haraka.

*************

Mkurugenzi wa upelelezi alikuwa amesimama kando ya dirisha ofisini kwake akitazama nje kwenye barabara, kiganja cha chake cha mkono wa kulia kikiwa kimekishika kiganja  cha mkono wa kushoto.

Alikuwa akitazama nini? Hakuwa akitazama chochote. Kila kitu kilichokuwa mbele ya macho yake alikuwa amekizoea. Hakukuwa na cha ajabu kwake. Lakini alisimama hapo ili kukiruhusu kichwa chake kuwaza vyema.

Tukio la kutekwa kwa binti wa mwekezaji, tajiri Christopher Lee aliyekuwa akizuru hapa nchini lilimsababishia msongo wa mawazo na hivyo kumfanya aone vyema kusimama kuliko kukaa.

Alikuwa akijiuliza endapo binti huyo hatapatikana katika muda wa siku saba, nini kitatokea? Mzazi wake atakuwa tayari kutoa fedha zilizotakiwa au binti huyo atauawa?

Alitambua kuwa mambo yote mawili hayatakuwa mazuri kwa mustakabali wa nchi yetu inayohimiza wawekezaji kutoka nje.  Alijiambia kama mzee Christopher Lee atalazimika kulipa pesa hizo ili kumuokoa mwanawe, nchi yetu itatazamwaje na jumuiya ya kimataifa kuhusu suala la uwekezaji?

Au kama binti huyo atauawa baada ya pesa hizo kutotolewa, jumuiya ya kimataifa itaiona Tanzania si mahali salama pa kuwekeza.

Lawama za nje zitakuja kwa nchi nzima. Lakini lawama za ndani zitakwenda kwenye jeshi la polisi hususani idara yake ya upelelezi inayohusika na makosa ya jinai.

Kutokana na sababu hizo, mkurugenzi huyo alijiambia, lilikuwa ni jukumu lake yeye kuhakikisha binti huyo anapatikana akiwa salama. Alikuwa akimuamini kachero aliyempa jukumu hilo lakini kuchelewa kwake kumpa ripoti ya nini kinaendelea hadi muda huo kulimtia wasiwasi.

Wakati akiendelea kuwaza, simu yake iliyokuwa juu ya meza ikaita. Mkurugenzi huyo aligeuka akaenda kwenye kiti akakaa na kuinua mkono wa simu na kuuweka sikioni.

“Mkurugenzi wa upelelezi hapa.”

“Ninataka kujua umefikia wapi?” Sauti ya mkuu wa jeshi la polisi ikamshitua.

“Mkuu imemtuma Inspekta Temba kwenda Segerea kuchunguza kuhusu mmoja wa wale watu waliotambuliwa kuhusika kumteka Isaac na dereva wake. Kama nilivyokufahamisha mwanzo, mtu yule ni mfungwa lakini wale watu wamesema walimuona katika tukio lile. Sasa Temba amekwenda Segerea kujua kama mfungwa huyo anaendelea kutumikia kifungo chake au alikata rufani na kuachiwa.”

“Tangu ameondoka hajakupigia simu kukufahamisha chochote?”

“Hajanipigia bado. Alisema akitoka Segerea atakwenda Tamasha Night Club, Sinza kuzungumza na mwanamke ambaye alikuwa na uhusiano na mtu wa pili ambaye alitambuliwa kwenye picha.”

“Tunatakiwa kupata taarifa ya kila tukio. Waziri ananipigia simu kila wakati kutaka kujua kinachoendelea. Jaribu kumpigia simu Temba ili akupe taarifa aliyopata.”

“Sawa mkuu, nitampigia.”

Simu ya upande wa pili ikakatwa. Mkurugenzi wa upelelezi akampigia Inspekta Temba.

Simu ya Temba ilikuwa inaita bila kupokewa. Kitendo hicho kikamshitua mkurugenzi huyo kwani hakikuwa cha kawaida. Hakikuwa cha kawaida si kwa Temba tu bali kwa afisa yeyote aliyekuwa chini yake.

Alimpigia tena kwa mara ya pili. Bado simu iliendelea kuita bila kupokewa.

“Kwanini hapokei simu?” Mkurugenzi huyo akajiuliza kwa hamaki akiwa amekunja uso.

Alipumua kwa sekunde kadhaa kabla ya kumpigia mmoja wa mkachero wa idara yake aliyekuwa akitumainika, kachero Victor Msembeko.

“Msembeko hebu njoo ofisini kwangu,” alimwambia baada ya Msembeko kupokea simu yake.

“Sawa mkuu, nakuja.”

Msembeko aliondoka ofisini kwake akapanda ngazi ya jengo hilo la makao ya polisi hadi ghorofa ya tano ilikokuwa ofisi ya mkurugenzi wa idara ya upelelezi.

Kama ilivyo kwa kachero yeyote anapoitwa ofisini kwa mkuu wake alikuwa na wasiwasi wa sintofamu. Alikuwa hajui anaitiwa nini, kulikuwa na kazi anayoitiwa au kulikuwa na mushikeli wowote? Hakupata jibu.

“Kaa kwenye kiti.” Mkurugenzi huyo alimwambia Msembeko mara tu alipomuona.

Msembeko alikaa kwenye kiti huku tashiwishi likisomeka usoni mwake.

Mkurugenzi alimueleza Msembeko kwa muhutasari kuhusu ziara ya Inspekta Temba huko Segerea na Sinza.

“Hivi sasa nampigia simu lakini haipokewi. Nimempigia mara mbili, simu inaita tu. Nataka uende Segerea na Sinza ujue nini kimemtokea.”

“Sawa mkuu, acha niende.”

“Nenda mara moja. Kama kuna lolote utanipigia simu huko huko kunijulisha. Sawa?”

“Sawa mkuu.”

Dakika kadhaa baadaye Msembeko aliwasili katika gereza la Segerea na kuonana na mkuu wa gereza hilo.

“Inspekta Temba aliwasili hapa kama saa moja hivi iliyopita.” Mkuu wa gereza hilo alimjibu Msembeko baada ya kumuuliza kuhusu kachero huyo.

“Alikuja kukuuliza suala gani?”

“Suala la Christian Bambo, mfungwa wetu anayetumikia kifungo cha miaka thelathini.”

Inaendelea…