HADITHI: Kwa Mtutu wa Bunduki – 3

ISAAC na Mkwetu wakazirudia tena zile picha zilizokuwa kwenye kuta.

Walipomaliza kuzikagua picha zote walimwambia Temba hawajagundua picha nyingine.

Ndipo Temba alipowatolea albamu za picha mbali mbali za wahalifu.

Baada ya kufungua kurasa tatu tu Mkwetu aligundua mtu mwingine.

“Inspekta mtu mwingine huyu hapa.” Mkwetu akamwambia Inspekta Temba aliyekuwa akirandaranda kwenye chumba hicho.

Temba aliposikia hivyo aliacha kuranda akamfuata Mkwetu ambaye macho yake yalikuwa yameganda kwenye picha ya mtu mmoja.

“Umemgundua yupi?” Temba akamuuliza.

“Huyu hapa.” Mkwetu akamuonyesha kwa kidole.

Temba akawa anaitazama picha ya mtu mwenye uso wa miraba minne, macho makubwa na pua iliyofura. Alikuwa na alama ya kushonwa ngozi kwenye paji la uso wake.

Christian Bambo.” Temba alitamka baada ya kusoma jina lake lililoandikwa chini ya picha yake.

Maelezo yaliyokuwa chini ya picha yalionyesha kwamba Bambo alikuwa akitumikia kifungo cha miaka thelathini jela kwa kosa la kufanya ujambazi wa kutumia silaha.

“Lakini huyu alishakamatwa na kushitakiwa. Hivi sasa anatumikia kifungo cha miaka thelathini jela.” Temba aliwaambia.

“Alihukumiwa lini?” Mkwetu akamuuliza.

“Alihukumiwa mwaka jana.”

“Bosi huyu si ndiye aliyekuwa akiendesha lile gari?” Mkwetu akamuuliza Isaac.

“Anaonekana kama ndiye yeye. Alikuwa amevaa kapelo.”

“Ndiye yeye. Alikuwa na alama ya mshono juu ya jicho lake la kushoto. Ile alama ni hii hapa anaonekana nayo.”

“Anaweza kuwa ndiye yeye.”

“Lakini mkumbuke kuwa huyu yuko kifungoni.” Temba aliwaambia.

“Ndiye yeye. Nimemuona vizuri.” Mkwetu alisisitiza na kuongeza.

“Hata uwekaji wake wa sharubu ni ule ule.”

“Kama atakuwa ni yeye atakuwa ameachiwa lakini tutafanya uchunguzi kujua ni yeye ama siye.”

“Haiwezekani asiwe yeye, ni yeye tu. Huenda ametolewa gerezani.” Mkwetu alimwambia Temba.

“Hizi picha nyingine tutakuja kuzitazama tena kesho. Tuna mengi ya kufanya muda huu na picha ni nyingi.” Isaac akamwambia Temba.

“Sawa. Kwa hawa watu wawili mliowatambua kwa leo wanatosha. Upelelezi wetu utaanza kwa hawa.”

Taarifa ya magari mawili aina ya Buty ya rangi nyeusi ya kampuni ya Christopher Lee yaliyotumika kumteka Myra ilikuwa imeingizwa kwenye mtandao wa kipolisi na hivyo kuanza kutafutwa nchi nzima.

Taarifa kuhusiana na magari hayo iliyaeleza magari hayo yalivyo, aina yake, rangi yake na namba zake ya usajili. Polisi walitakiwa kuyakamata popote watakapoyaona pamoja na watu watakaokutwa ndani ya magari hayo.

Mbali ya polisi kuchukua hatua hiyo, polisi wa kitengo cha mawasiliano cha polisi walikuwa wakifuatilia mionzi ya chip iliyokuwa kwenye simu ya  Isaac iliyoporwa na majambazi hao.. Waliamini kwamba hapo watakapoipata simu hiyo na majambazi hao watakuwa hapo hapo.

Baada ya hatua zote hizo, mkuu wa jeshi la polisi Inspekta Jenerali Lymo akampigia simu waziri wa mambo ya ndani.

“Mheshimiwa waziri uchunguzi umefanyika na imebainika ni kweli binti wa mwekezaji Christopher Lee ametekwa kiwanja cha ndege saa sita mchana alipowasili na ndege kutoka Adis Ababa Ethiopia.”

Akaendelea kumueleza.

“Kabla ya tukio hilo kaka yake ambaye alikuwa anakwenda kiwanjani kumpokea naye alitekwa akiwa na dereva wake. Inadaiwa kwamba alitekwa na watu wawili waliovaa mavazi ya polisi wa usalama barabarani ambao waliyasimamisha magari yao mawili aina ya Buty na kuwateka nyara kwa kutumia gari aina ya Land Rover la rangi nyeupe. Yale magari mawili aina ya Buty yalichukuliwa na majambazi hao.

IGP Lymo alisita akawaza kidogo kabla ya kuendelea.

“Huyu kaka mtu na dereva wake walikwenda kuachwa msitu wa Pande baada ya simu zao kuchukuiwa. Walirudi tena Dar kwa msaada wa gari la mkuu wa wilaya ya Bagamoyo lililokuwa linakuja Dar es Salaam.”

“Sasa ni kwanini waliwateka na kwenda kuwaacha msitu wa Pande?”

“Ilikuwa ni kuwazuia wasiende kumpokea huyo binti aliyekuwa anawasili kutoka Ethiopia kwani baada ya kuchukua magari yao walikwenda kiwanja cha ndege kumpokea wao na hivyo kumteka kwa urahisi.”

“Hao majambazi waliwasiliana na nani kujitambulisha na kueleza wanchokitaka?”

“Kwa mujibu wa maelezo ya mwana wa Christopher Lee majambazi hao walimpigia simu baba yao aliyeko Uingreza na kumueleza kwamba wamemteka binti yake na kwamba wanataka awalipe  dola milioni mia moja, la sivyo watamuua baada ya siku saba.”

“IGP hebu nifahamishe mmejipangaje kuhakikisha huyo binti anapatikana?”

“Napenda kukuhakikishia mheshimiwa waziri kwamba tumejipanga vizuri kiuchunguzi na tayari majambazi wawili miongoni mwao wameshatambuliwa kwa kutumia picha za wahalifu tulizonazo. Hao watu sasa wanatafutwa. Bado yale magari mawili aina ya Buty yaliyotumika kumteka binti huyo nayo yanatafutwa na polisi. Tumeshatoa taarifa nchi nzima kwa njia ya mtandao.”

“Sikiliza IGP, tukio lililotokea ni tishio kwa wawekezaji wengine. Unajua usalama ni muhimu. Ninataka mfanye kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa huyu binti anapatikana na waliohusika wanachukuliwa hatua. Vinginevyo hili tukio ambalo ninaamini huenda limeandaliwa na watu wasiotutakia mema litatuletea kashifa kubwa.”

“Nimekuelewa mheshimiwa. Ninakuahidi kwamba binti atapatikana.”

“Sawa.”

Waziri akakata simu. Akampigia mzee Christopher Lee.

Simu yake ilipokelewa baada ya kuita kwa sekunde chache.

“Hello…..!”

“Mzee Christopher Lee….”

“Ninakupata mheshimiwa waziri.”

“Mzee tumefanya uchunguzi na tumegundua ni kweli tukio ulilonieleza limetokea leo saa sita mchana. Hivi tunavyozungumza polisi na wapelelezi wanamtafuta binti yako na ninakuhakikishia kuwa atapatikana.”

“Unakiri  udhaifu wazi wazi.”

“Udhaifu upi mzee?”

“Usalama wenu uko wapi?”

“Usalama upo. Tukio kama hilo limetokea kisirisiri mno. Ni miongoni mwa matukio yanayoweza kutokea popote duniani. Cha msingi tupe muda tushughulike nalo.”

“Una uhakika kwamba mnaweza kumpata mwanangu akiwa mzima?”

“Mwanao atapatikana. Tayari majambazi wawili waliohusika kumteka wameshagundulika.”

“Wako wapi?”

“Bado wanatafutwa,”

“Wanaweza kugundulika lakini wasipatikane.”

“Ninakuhakikishia kwamba watapatikana.”

“Watapatikana lini?”

“Siwezi kukwambia watapaikana lini lakini ninakuhakikishia kwamba watapatikana.”

“Sikiliza waziri, wewe ndiye mwenye dhamana ya maisha ya watu. Ninakuomba uhakikishe kikweli kweli kuwa mwanangu anapatikana na waliohusika kumteka wanakamatwa. Nisingependa kusikia kitu kingine zaidi ya hicho. Umenielewa?”

“Nimekuelewa.”

“Roho ya mwanangu haiwezi kufanywa mtaji.”

“Nimekuelewa.”

“Isaac yuko wapi?”

“Isaac alikuwa ametekwa lakini ameshaachiwa na tuko naye.”

“Nataka kuwasiliana naye.”

“Simu yake imechukuliwa na majambazi hao lakini tutamfahamisha ajitahidi kuwasiliana na wewe.”

“Sawa.”

Wakati waziri akizungumza na mzee Lee, Inspekta Tamba alikuwa amempakia Isaac na Mkwetu kwenye gari akiwapeleka Tegeta kwenye kiwanda cha Saruji.

“Hili tukio limetusikitisha sana.” Temba alimwambia Isaac aliyekuwa amekaa siti ya mbele ya abiria.

“Kuwapata hawa watu kutategemea sana uwezo wenu wa kupambana na vikundi vya uhalifu kama hivi.”

“Uwezo upo na kwa vile mmeshawatambua watu wawili mmetuwekea barabara nyeupe ambayo tutaifuata hadi tuhakikishe tunampata dada yako.”

“Wametuona sisi ni tajiri siyo?”

“Wahalifu wanalenga mahali ambapo wanaona watafanikiwa.”

“Dar es Salaam hii matajiri ni wengi sana.”

“Nadhani wamehisi kwamba mzee Lee anaweza kutoa pesa kirahisi rahisi ili kumuokoa mwanawe.”

“Wamekosea sana. Sisi tunaweza kuwaleta FBI au CIA kuja kufanya uchunguzi.”

“Hatujahitaji watu kutoka nje kwa tukio kama hili. Tunao uwezo wa kutosha wa kuwatafuta wenyewe na kuwakamata.”

“Nina wasiwasi sana kwamba dada yangu anaweza kuuawa endapo pesa hizo hazitatoka.”

“Ondoa wasiwasi wako. Sisi tunajua tunachokifanya.”

Walipofika Tegeta Isaak na Mkwetu walishuka, Temba akawaambia anakwenda gereza la Segerea kuchunguza kuhusu mtu mmoja waliyemtambua kwenye picha ambaye anaamini kwamba bado yako kifungoni.

“Niandikie namba yako. Baadaye kidogo nitakuwa na simu nyingine. Nitataka kuwasiliana na wewe.” Jsaac alimwambia Inspekta temba.

“Sawa.”

Temba alichomoa notibuku yake akamwamndikia namba yake kisha akampa.

“Namba yangu ni hii.”

“Sawa. Nitakupigia.”

Inaendelea…