HADITHI: Kwa Mtutu wa Bunduki – 2

MMOJA wa maafisa usalama aliyekuwa kiwanjani hapo alimwambia Temba, msichana mwenye jina la Myra alipokewa na watu wawili na kupakiwa kwenye gari moja kati ya magari mawili aina ya Buty ya rangi nyeusi.

Mpaka hapo Temba hakuwa amepata fununu yoyote ya kutekwa kwa msichana huyo ambaye kadiri alivyoelezwa aliondoka kiwanjani hapo kwa gari aina ya Buty iliyokuwa ikisindikizwa na gari jingine la aina hiyo hiyo. Akaamua kwenda Tegeta kilipokuwa kiwanda hicho cha Saruji.

***********

Mwana wa bilionea Christopher Lee, Isaac alipopakiwa kwenye Land Rover jeupe, yeye na mwenzake walifungwa mikono ndani ya gari. Gari hilo liliwatoa nje ya jiji na kushika barabara ya Bagamoyo. Liliwapeleka hadi msitu wa Pande likasimama.

Mzee Christopher Lee alipompigia simu Isaac akiwa London, mmoja wa polisi hao bandia ndiye aliyepokea simu na kujibishana na Mzee Christopher Lee kabla ya kukata simu na kuwashusha mateka wao. Simu ya Isaac ikiwa imechukuliwa, dereva aliyekuwa naye naye alipekuliwa na simu yake ikachukuliwa.

Baada ya hapo Land Rover iliondoka na kuwaacha hapo hapo. Wakati huo ndege iliyomleta Myra ilishatua Dar es Salaam na Myra kupokewa na watu wengine waliomdanganya kuwa wameagizwa na Isaac baada ya gari la Isaac kupata pancha. Myra alipelekwa mahali kusikojulikana.

Wakati Isaac na mwenzake wanafika Dar kwa msaada wa gari la mkuu wa wilaya, moja kwa moja walikwenda kiwanja cha ndege. Baada ya kuuliza kuhusu mgeni wake aliyewasili kwa ndege iliyotoka Ethiopia aliambiwa ndege ilishawasili na abiria wote wameshaondoka.

Alipoulizwa kulikoni? Akaueleza mkasa wa dada yake Myra ndipo watu wa usalama wa taifa walipombainishia kuwa kuna taarifa kwamba Myra ametekwa na kwamba kulikuwa na inspekta wa polisi aliyefika hapo kiwanjani kudodosa kuhusu suala lake.

Watu hao wa usalama wa taifa wakampeleka Isaac kituo cha polisi cha kiwanjani hapo kupata maelezo zaidi.

Alipojitambulisha na kueleza kuhusu masahibu yaliyomfika na taarifa kwamba huenda dada yake anayeitwa Myra aliyekuwemo kwenye msafara huo ametekwa nyara, maafisa wa kiwanja hicho walimuuliza jina la dada yake.

“Anaitwa Myra Christopher Lee.”

“Kuna kachero kutoka makao ya polisi aliyekuja kuhoji kuhusu msichana mwenye jina hilo akiwa na taarifa kwamba ametekwa nyara hapa hapa kiwanja cha ndege.” Mkuu wa kituo hicho alimwambia.

 “Waliompokea walionekana?” Isaac akauliza.

“Kuna afisa usalama mmoja ambaye ameeleza kwamba alimuona akipokewa na watu wawili.”

“Walikuwa Waafrika?”

“Ndiyo.”

“Walimchukua kwa gari la aina gani?”

“Imeelezwa kwamba aliondoka na Buty ya rangi nyeusi.”

Isaac akashusha pumzi ndefu.

“Ni kweli dada yangu ametekwa. Wametumia gari langu waliloninyang’anya.”

“Sasa unapaswa kwenda kutoa ripoti Central Police ili watu hao waweze kufuatiliwa.”

Inspekta Temba alishafika Tegeta kwenye kiwanda cha Saruji cha Christopher Lee. Alishaambiwa kwamba afisa mkuu wa kiwanda hicho bwana Isaac aliondoka kwenda kiwanja cha ndege kumpokea dada yake aliyekuwa anawasili kutoka Ethiopia.

Wakati Temba akiendelea na mahojiano akapigiwa simu na mkuu wa kituo cha polisi cha kiwanja cha ndege.

“Afande kuna ripoti imetufikia kuhusiana na kile ulichokuja kutuuliza.” Mkuu wa kituo hicho akamwambia Inspekta Temba kwenye simu.

“Ripoti hiyo inasemaje?”

“Inakubidi urudi tena uonane na huyu Bwana Isaac, yuko hapa.”

“Yuko na Mayra?”

“Hapana. Tuna shaka kwamba Myra ametekwa nyara.”

“Huyo Isaac anasema alikuwa wapi?”

“Ametuambia kwamba alikuwa ametekwa nyara pamoja na dereva wake wakati wanakuja kiwanja cha ndege kumpokea huyo mgeni wake.”

“Mwambie anisubiri ninakuja hapo hapo.”

“Sawa.”

Dakika chache baadaye Temba akawasili kiwanjani hapo. Alikutana na Isaac kwenye kituo cha polisi.

Isaac alimueleza Temba mkasa mzima uliomtokea. Hapo ndipo Temba alipothibitisha kwamba Myra alikuwa ametekwa.

“Walikuzuia wewe usije kumpokea dada yako ili waweze kumteka na alichukuliwa hapa kiwanjani na gari mbili aina ya Buty za rangi nyeusi.”

“Ndizo hizo tulizokuwa tunakuja nazo.”

“Sasa wamezitumia ili kumdanganya Myra aone ni gari zao.”

“Sasa tutafanyaje inspekta kwa sababu hao watu wameshampigia baba na baba amenipigia mimi kuniuliza lakini simu ilipokewa na watu waliotuteka wakamueleza wazi kwamba wametuteka ila Myra hawatamuachia mpaka wapatiwe kitita cha dola milioni mia moja.”

Temba akapiga mluzi wa mshituko.

“Dola milioni mia moja!”

“Ndiyo. Dola milioni mia moja. Hawa watu wanafanya mzaha na pesa na wanafanya mzaha na roho za watu kwa maana wamesema wasipopewa hizo pesa watamuua dada yangu.”

“Ndani ya hilo gari kulikuwa na watu wangapi?”

“Kulikuwa na watu wanne na walikuwa na bastola.”

Na umewaona na kuwakariri vizuri sura zao?”

“Ndiyo nimewakariri vizuri.”

“Ukiwaona tena au ukiona picha zao unaweza kuwatambua.”

“Bila shaka yoyote.”

“Sawa. Umesema simu yako wameichukua?”

“Ndiyo wameichukua pamoja na simu ya dereva wangu.”

“Sikiliza kijana. Ondoa wasiwasi wako. Hawa watu wamefanya jaribio ambalo hawataliweza. Watapatikana tu na dada yako atakuwa salama kabla ya siku saba. Nitawachukua kwenye gari langu twende makao ya polisi.”

“Sasa siwezi kuwasiliana na mzee kumueleza hali iliyotokea. Najua atakuwa na wasiwasi.”

Temba aliyekuwa ameketi akainuka.

“Usijali. Utawasiliana naye. Nifuateni.”

************

Ndani ya makao ya polisi heka heka ilikuwa imepamba moto. Isaac na dereva wake ambaye alijitambulisha kwa jina la Faustin Mkwetu walipelekwa katika chumba cha maktaba ya polisi ya picha za wahalifu waliokuwa wamehakikiwa kuwa ni wahalifu waliowahi kukamatwa na kutumikia vifungo au wale wanaoendelea kutafutwa na polisi.

Chumba hicho kilikuwa kimetundikwa picha za wahalifu wanaotafutwa kwenye kuta. Picha zilizokuwa kwenye kuta zilikuwa zile za wahalifu waliofanya matukio ya uhalifu katika siku za karibuni. Picha hizo zilikuwa na majina ya wahalifu hao, nyingine zikiwa na anuani zao pamoja na miji wanayopenda kutembelea hapa nchini.

“Mtaanza kuzikagua kwa makini hizo picha zilizotundikwa kwenye kuta. Endapo mtaona picha ya mmoja wa watu waliowateka mtanifahamisha. Endapo hamtaona picha yoyote nitawapa albam za picha mkague picha nyingine.” Temba aliwaambia Isaac na Mkwetu walipoingia kwenye chumba hicho.

“Umejuaje kama picha zao zitakuwa hapa?” Isaac akamuuliza Temba.

“Hizo ni picha za wahalifu wanaofahamika ambao wamewahi kukamatwa au kutafutwa na polisi. Tunaamini hao watu waliowateka wanaweza kuonekana kwenye picha hizo. Endeleeni kutazama hizo picha. Tunataka kuujua mtandao wao.”

Isaac na Mkwetu wakaanza kuzitazama picha hizo wakikizunguka chumba hicho. Isaac baada ya kukizunguka chumba hicho alitikisa kichwa kabla ya kumwambia Inspekta Temba: “Sidhani kama tutaweza kuwagundua wale watu kwenye hizi picha. Sijamuona yeyote.”

“Bosi umezitazama kwa haraka. Kuna hii picha hapa.” Mkwetu akamwambia Isaac.

“Nimeangalia picha zote.”

“Kuna hii hapa.”

Mkwetu sasa alikuwa ameiwekea kidole picha aliyokuwa anaionyesha. Temba akamfuata Mkwetu.

“Picha ipi?” Alimuuliza.

“Hii hapa. Huyu mtu alikuwepo. Huyu ndiye aliyechukua simu yangu.”

Temba akaitazama picha hiyo.

“Hebu nimuone.” Isaac akasema na kusogea mahali aliposimama Mkwetu na Temba.

“Yes, nakumbuka nilimuona. Lakini una uhakika kwamba ndiye huyu huyu au tunawafananisha?”

“Ndiye huyu huyu.”

“Okey. Inspekta, mmojawapo ni huyu. Mwenzangu amemuangalia vizuri.”

Temba aliichomoa ile picha pamoja na maelezo yake kwa kifupi.

“Huyu anaitwa Simon Kumbo.” Temba aliwaambia huku akisoma maelezo yaliyokuwa chini ya ile picha.

“Ni mhalifu wa siku nyingi ambaye tunaamini alihusika katika matukio mengi ya ujambazi. Hajawahi kukamatwa na anatafutwa na polisi.”

“Kama hajawahi kukamatwa picha yake mliipata vipi?” Mkwetu akamuuliza.

“Picha yake ilipatikana chumbani kwake baada ya kugundua kuwa alikuwa akiishi Vikunguti. Lakini wakati tunafika alikuwa ameshakimbia, mpaka sasa hajapatikana. Ni mjanja na ni hodari wa kuwakwepa polisi. Anapenda kutembelea miji ya Arusha na Nairobi. Ana mzazi mwenzake aliyemzalisha mtoto mmoja ambaye anafanya kazi katika klabu moja ya usiku, anaitwa Suzana. Hebu endeleeni kutazama picha nyingine kwa makini, mnaweza kuwagundua wengine.”