
SIMU ya upande wa pili ikakatwa.
Nikabaki nimeduwaa nikiwaza. Taarifa ile sikuitarajia kabisa. Kama tukio hilo lingetokea wakati Mustafa hayupo, kusingekuwa na tatizo. Ningeweza kumhudumia mume wangu huko Muhimbili. Lakini tukio hilo limetokea wakati Mustafa akiwepo.
“Nitafanyaje?” Nikajiuliza.
Nitamueleza nini Mustafa wakati nahitajiwa huko hospitali?
Nikajimbia kama ajali ilikuwa mbaya kiasi kwamba taniboi wake alikufa hapo hapo huenda Musa mwenyewe pia yuko katika hali mbaya. Wamenificha tu kuniambia ukweli.
Kama itakuwa ni hivyo, hiki ndio kipindi changu cha kuumbuka! Nilijiambia.
Wakati naendelea kufikiria la kufanya simu yangu ikapigwa tena. Namba iliyopiga ilikuwa nyingine.
Nikaipokea.
“Natumaini nazungumza na mke wa Musa,” sauti ya kiume ikaniuliza.
Niligundua kuwa miguu yangu ilikuwa inatetemeka.
“Ndio mimi?”
“Umepata taarifa ya mumeo kupata ajali?”
“Ndio nimepata.”
“Hivi sasa ameletwa katika hospitali ya Muhimbili, yuko wodi ya majeruhi. Unahitajika uende ukamuone.”
“Lakini hali yake ikoje?”
“Amevunjika miguu yote miwili na alipata majeraha madogo madogo.”
“Kama miguu yote imevunjika anahudumiwa na nani?”
“Ndio maana unahitajika uende ili ujue mahitaji yake.”
“Sawa, nitakwenda.”
Simu ikakatwa.
Nikajaribu kuipiga namba ya Musa ili nizungumze naye lakini simu yake ilikuwa haipatikani.
Moyo ulikuwa ukinienda mbio na mwili ulikuwa umenifumka jasho.
Swali lililokuwa linaumiza akili yangu ni jinsi nitakavyoweza kumhudumia Musa akiwa hospitalini wakati huku niko na mume mwingine!
Baada ya kuwaza kwa sekunde kadhaa niliamua kumpigia smu Mustafa.
“Uko wapi?” Nikamuuliza.
“Si nimeondoka hapo nyumbani muda huu huu?” Mustafa akaniuliza kwa ukali kidogo.
“Nimekuuliza hivyo kwa sababu, kuna taarifa nimeletewa sasa hivi.”
“Taarifa gani?”
“Kuna kaka yangu amepata ajali ya gari, amevunjika miguu yote miwili, natakiwa kwenda kumuona hospitalini.”
“Ni kaka yako yupi huyo?”
“Ni kaka yangu, anaishi Tanga, yeye ni dereva wa malori. Nimeambiwa amepata ajali akiwa Zambia, leo ndio ameletwa yuko Muhimbili.”
“Mmh!” Mustafa akaguna kisha akaniambia.
“Mimi sijui kama una kaka yako ambaye ni dereva wa malori.”
“Yupo lakini anaishi Tanga ndio sababu hujamuona, ni kaka upande wa shangazi yangu.”
“Sasa nisubiri nakuja muda huu huu.”
“Nilikuwa nataka uniruhusu niwahi kwenda. Nimeshapigiwa simu mara mbili.”
“Nitakupeleka na gari, nisubiri nakuja sasa hivi.”
Mustafa kakakata simu.
Sasa imeshakuwa balaa, nikajiambia. Mustafa anataka anipeleke kwa gari lake! Si watakwenda kukutana waume wawili?
Wazo moja likanijia kwamba niondoke bila kumsubiri Mustafa kwa vile nimeshamuarifu tukio lililotokea.
Kama atakuja na kunikosa ataambiwa nimewahi kwenda Muhimbili.
Wazo hilo likapingwa na wazo jingine. Niliona kwamba kama Mustafa atakuja na kukuta nimeshaondoka anaweza kukasirika na pia atanifuata huko hospitalini. Kile ninachokikataa cha kukutana na mume mwenzake ndicho kitakachotokea.
“Sasa nifanye nini?” Nikajiuliza. “Nimsubiri Mustafa au niondoke?”
Sikupata jibu.
Ghafla nikaisikia simu yangu ikiita. Nilipoitazama nikaona namba ya Mustafa.
Nikaipokea.
“Niko hapa nje, toka twende,” Mustafa akaniambia kwenye simu.
Moyo ulinishituka.
Bila shaka nilipompigia simu aliamua kurudi na hakuwa mbali.
Nikajikuta nikimuuliza.
“Umeshakuja?”
“Ndio, niko hapa nje. Nakusubiri.”
Sikuwa na ujanja tena isipokuwa kujiandaa na kutoka. Nilizima simu yangu na kujipakia kwenye gari la Mustafa. Lakini sikuwa na raha. Akili yangu ilikuwa ikiwaza kila kitu.
Mustafa akaliondoa gari.
“Kwa hiyo tunaelekea muhimbili?” Akaniuliza wakati akitia gia ya pili.
“Ndio, tunaenda Muhimbili.”
Kama ni kuachwa na waume wote wawili itakuwa leo, nikajiambia kimoyomoyo.
“Huyo kaka yako mimi simjui, na sikuwahi kukusikia hata siku moja ukaniambia kuwa una kaka yako ambaye ni dereva wa malori.” Mustafa akaniambia huku akiendesha.
“Sijawahi kukwambia kwa sababu hafiki sana huku Dar lakini ninaye kaka yangu ambaye ni dereva wa malori na anakujua wewe, sema hamjakutana tu,” nikamwambia kwa kujikaza.
“Kwa hiyo umesema anaishi Tanga?”
“Yeye anaishi Tanga, kwa hapa Dar mwenyeji wake nitakuwa mimi.”
“Na huko Tanga wanazo hizo taarifa?”
“Wanazo.”
“Basi ni vizuri na mimi nimuone tujuane.”
“Sasa sijajua yuko katika hali gani?”
“Kama miguu yote miwili imevunjika atakuwa katika hali mbaya.”
“Ndio hivyo.”
Kufumba na kufumbua tukafika Muhimbili. Haukuwa muda wa kutazama wagonjwa lakini tulitumia uenyeji tukaingia. Tulikwenda hadi katika wodi ya majeruhi huku miguu yangu ikitetemeka. Nilijua dakika zangu za kuumbuliwa na waume zangu zilikuwa zikisogea kwa haraka.
Tuliangaza wagonjwa waliokuwemo, nikamuona Musa.
“Yule pale,” nikamwambia Mustafa.
Tukaenda. Musa alikuwa amelala kichalichali. Alionyesha alikuwa taabani. Mguu mmoja ulikuwa umening’inizwa. Mguu mwingine ulikuwa umefungwa bendeji ngumu.
Tulipofika kando ya kitanda chake nikamsalimia.
“Vipi hali yako?”
Musa akayakaza macho yake kunitazama.
“Hali yangu ndio kama unavyoniona. Miguu yangu yote miwili imevunjika.” Musa akaniambia.
Nilishukuru kuwa hakutumia neno. ‘Mke wangu.’
“Pole sana,” nikamwambia kisha nikamtazama Mustafa.
“Shemeji yako huyo, ulisema humjui,” nikamwambia.
Mustafa akampa mkono.
“Oh shemeji. Pole sana.”
Nilikuwa nimewazuga wote wawili. Musa alijua Mustafa ni kaka yangu na Mustafa nilishamwambia kuwa huyo majeruhi ni kaka yangu.
“Asante shemeji.” Musa akamjibu huku akionyesha kusikia maumivu makali.
“Hii ajali ilitokeaje?”
Musa akatueleza kwamba aligongana uso kwa uso na lori jingine lililokuwa linakwepa shimo.
Akatuambia kuwa taniboi wake alikufa pale pale, yeye ndio alivunjika miguu yote miwili.
Wakati Musa anatueleza daktari akaja kutuondoa.
“Tunataka kumhudumia mgonjwa,” akatuambia.
Tukaondoka. Nilishukuru vile tulivyoondolewa ingawa sikuwa nimezungumza chochote cha maana na Musa. Nikajiambia nitakwenda tena asubuhi nikiwa peke yangu. Kila itakavyokuwa nilijua Mustafa asingenifuata tena. Nilikuwa naijua tabia yake.
Tulitoka nje ya hospitali tukajipakia kwenye gari na kuondoka.
“Sasa itabidi uje tena kesho asubuhi umuone kaka yako, ujue anahitaji nini.” Mustafa akaniambia.
“Ndio, nitakuja kesho asubuhi niweze kuzungumza naye.”
Baada ya hapo tukabaki kimya. Nilishukuru jinsi nilivyoweza kuwazuga waume hao wawili wasijuane, kila mmoja akaamini kuwa mwenziwe ni shemeji yake. Ilitaka ujasiri sana na nilikuwa nao ujasiri huo.
Niliendelea kujiambia hata kama Mustafa alikuwa na wasiwasi na Musa kwamba ni mtu wangu, huenda ameondoa wasiwasi wake kwa kuamini kwamba Musa ni kaka yangu kama nilivyomwambia.
Mustafa alinirudisha nyumbani lakini hakuingia ndani. Aliponishusha kwenye gari aliondoka.
Asubuhi ya siku iliyofuata Mustafa alinipeleka Muhimbili, akaniacha nje. Hakuingia ndani.
“Utanisalimia, mimi nawawahi wale jamaa.” Mustafa akaniambia wakati anaondoka.
Hata sikujua ni jamaa gani hao aliokuwa akiniambia anawawahi. Huenda hakukuwa na jamaa yeyoye. Ulikuwa uongo wake tu.
Vile alivyoondoka nilifurahi kwa vile ningepata nafasi ya kuongea vizuri na Musa.
Nilipoingia hospitalini nilikwenda katika wodi aliyokuwa amelazwa Musa. Nilimkuta Musa akiangaza macho kwenye mlango akitarajia kumuona ndugu au jamaa yeyote aliyekwenda kumtembelea.
Nikamshitua.
“Mume wangu, una hali gani?”
Ndipo aliponiona.
“Oh Mishi, umeshafika?”
“Nimefika mume wangu, pole kwa matatizo.”
“Asante. Matatizo ni makubwa, yaani hapa bila msaada wa mtu inakuwa ni shida.”
“Kwanini?”
“Siwezi kuondoka hapa na siruhusiwi kuondoka. Hivyo kila kitu ni hapa hapa. Ndio maana niliwambia wakupigie simu ili uje unisaidie.”
“Kwa muda huu unahitaji msaada gani?”
Musa akaniambia msaada aliokuwa anahitaji nikamsaidia lakini ilinichukua muda.
“Inabidi kila asubuhi uje.” Musa akanimabia na kuongeza.
“Ukija niletee mswaki, dawa ya meno, sabuni ya maji ya Dettol kwa ajili ya kuni-sponji.”
“Nitakuletea lakini sina uhakika wa kuwahi kufika kila asubuhi.”
Inaendelea…