HADITHI: Bomu Mkononi – 29

“WACHA we…!”

“Nampa kila kitu anachotaka.”

“Usiniambie…”

“Ndio nakwambia shoga. Usione kimya, kimya kingi kina mshindo!”

“Na kweli kina mshindo, sasa mmepanga kuoana lini?’

“Bado kwanza, nasikia hata Mustafa ameoa!”

Hapo moyo ukanipasuka.

“Mustafa yupi?” Nikajidai kuuliza.

“Yule rafiki yake aliyekuwa akifanya naye biashara.”

“Amemuoa nani?”

“Simjui, nilisikia tu kuwa ameoa.”

 “Labda, huwezi kujua.”

Pakapita ukimya mfupi. Nikamuuliza Amina.

“Utakuja lini?”

“Labda wiki ijayo lakini kwa vile namba yako nimeigundua nitakupigia.”

“Poa.”

Baada ya kuzungumza na Amina nikapata mawazo, ni nani aliyemwambia kuwa Mustafa ameoa? Hivi ni kweli hajui ni nani aliyeolewa na Mustafa au alikuwa ananivunga mimi tu? Nikajiuliza.

Sikutaka siri yangu ya kuolewa na zaidi ya mume mmoja itoke nje. Kama Amina ameshagundua kuwa nimeolewa na Mustafa haitakuwa siri tena. Upo uwezekano mkubwa kwa Mustafa na pia kwa Musa kuja kugundua kuwa nimewafanyia udanganyifu.

Maneno huenda na watu, kama mtu mmoja amepata hizi habari ni rahisi kuenea kwa watu wengine, nikajiambia.

Nilijiambia kwamba nitakuja kumuuliza vizuri nitakapokutana naye. Kama alishindwa kunieleza kwenye simu atakuja kunieleza tukiwa uso kwa uso.

Kwa vile madhumuni yangu yalikuwa ni kurudi kwa Sele nikamuandaa mwanangu na kuchukua baadhi ya nguo zake. Nikamwambia mtumishi wangu kuwa naondoka na mwanangu lakini kama Mustafa akitokea anipigie simu.

Nikamsisitizia kuwa Mustafa akitokea amwambie kuwa nimeenda kwa shangazi lakini niliondoka muda mfupi tu uliopita, sikutaka amwambie kuwa nimekuwa huko kwa muda mrefu.

Nilimuachia pesa kidogo za kutumia kisha nikaondoka na kumuachia nyumba.

Nilirudi Ilala kwa Sele. Nikakaa na mwanangu kwa siku tatu lakini kila siku nilikuwa napiga simu Kimara na Mbezi kujua hali za huko.

Siku ya nne yake Sele akanipigia simu na kunijulisha kuwa magari yake yameshawasili katika bandari ya Dar hivyo kesho yake angerudi ili kuyatoa bandarini.

Nikafurahi niliposikia habari ile kwani Sele aliniahidi kuwa katika magari hayo mawili gari moja litakuwa langu.

Kuanzia hapo mawazo yangu yakawa kwenye gari. Sikujali lingekuwa gari la aina gani, nilichojali ni kuendesha mwenyewe.

Siku iliyofuata Sele akawasili jioni. Wakati wote wa uchumba wangu na Sele sikuwahi kumueleza kwa uwazi kuwa nilizaa mtoto. Niliogopa kumueleza hivyo kwa kuona kuwa angebadili mawazo na asingetaka kunioa tena.

Jioni ile alipokuja akamuona mwanangu.

“Ni nani huyu?” Akaniuliza.

“Ni mwanangu,” nikamwambia.

Nilihisi alikuwa amegutuka lakini uso wake bado ulionekana mtulivu.

“Ametoka wapi?”

“Alikuwa kwa shangazi, wamemleta jana.”

“Ni mwanao wewe mwenyewe?”

“Ndiyo ni mwanangu, si nilimzaa na yule mume niliyeachana naye.”

“Mbona hujaniambia kama una mtoto?”

“Nadhani nilikwambia lakini hukutilia maanani.”

“Sikumbuki kama uliwahi kunieleza kitu kama hicho.”

“Labda umesahahu.”

Sele akanyamaza kimya lakini alionekana kupata mawazo fulani. Pengine hakutaka nijue kuwa hakufurahishwa aliniuliza.

“Anaitwa nani mwanao?”

“Anaitwa Rama.”

“Rama njoo mwanangu,” akamuita.

Angefanyaje wakati ndoa imeshapita. Kuniacha asingeweza kwa sababu nilijua alikuwa akinipenda. Ilibidi amkubali tu yule mtoto.

Rama alipoitwa alimfuta baba yake. Sele akamshika mkono.

“Hujambo?” Akamuuliza.

“Sijambo baba, shikamoo.”

“Marahaba. Kumbe unajua kuwa mimi ni baba yako!”

Rama akamkubalia kwa kichwa.

Ili kumfanya Sele aondoe mawazo nilikwenda kuketi kando yake nikamwambia Rama aende akacheze.

Pale pale tulipokaa nikaanza kumpa Sele maneno matamu ya chumbani kisha nikamshika mkono kuminua, nikaingia naye chumbani. Wewe utajua kilichonifanya nimpeleke huko chumbani.

Sele alikaa Dar wiki nzima kushughulikia magari yake. Magari yalipotoka aliyakamilishia taratibu zote za kiserikali za kuyatumia.

Mwenyewe alikuwa anajua kuendesha, mimi nilikuwa sijui. Akanipeleka kwenye chuo cha udreva kupata mafunzo ya udereva. Ninaporudi kutoka chuoni, alikuwa akinifundisha nyumbani.

Siku za mwanzo mwanzo kujifundisha gari sukani ilinipa taabu sana ninapoendesha, yaani kuliongoza gari barabarani ilikuwa mtihani. Kwa vile nilikuwa na pupa ya kuendesha niliona kama sitaweza lakini taratibu nikawa naweza kuliongoza gari kwa mwendo wa taratibu.

Kwa vile Sele alihitaji kurudi Marerani akaondoka na kuniacha na ile gari nililokuwa najifundishia. Yeye aliondoka na lile gari jingiune. Angeweza kwenda na basi kama kawaida yake lakini kwa kutaka sifa aonekane ana gari akaamua kwenda nalo.

Wakati naendelea na mafunzo ya gari, Mustafa akarudi kutoka China. Nilipigiwa simu nikiwa nyumbani kwa Sele.

“Dada, baba yake Rama amerudi.” Mtumishi wangu aliniamabia kwenye simu.

“Amerudi saa ngapi?” Nikamuuliza kwa taharuki.

“Hapa nyumbani amekuja sasa hiuvi.”

“Amesemaje?”

“Amekuulizia tu nikamwambia umekwenda kumjulia hali shangazi yako huko Ilala.”

“Akasemaje?”

“Kauliza shangazi gani, nikamwambia simjui.”

“Sasa yuko wapi?”

“Ameingia chumbani.”

“Sawa. Nakuja.”

Nilipokata simu tu Mustafa akanipigia.

“Habari yako?” Akaniuliza.

“Nzuri, uko wapi?” Nikajidai namuuliza.

“Kwani wewe uko wapi?”

“Nilikuja hapa Ilala kwa shangazi yangu anaumwa.”

“Mbona simjui huyo shangazi yako?”

“Wewe humjui kwa sababu sijakuonesha lakini ni dada wa marehemu baba yangu.”

“Ninachokumbuka uliniambia huna ndugu wa karibu hapa Dar.”

Nikabadili maneno.

“Huyo shangazi alitoka Tanga, aliletwa hapa Dar kutibiwa.”

“Anaendeleaje?’

“Hajambo kidogo.”

“Naomba uje nimesharudi.”

“Sawa nakuja.”

Nikamuandaa mwanangu haraka haraka. Nikafunga nyumba. Kwa vile tulikuwa na mlinzi sikuwa na wasiwasi na nyumba, nikaenda kupanda teksi.

Nilipofika Mbezi, kwa vile nilikuwa na mtoto wetu, Mustafa hakunitilia mashaka sana. Aliona kama nilikwenda kwa wanaume nisingechukua mtoto.

Nilikuwa nimeshamfundisha Rama akiulizwa na baba yake aseme kuwa tulikuwa kwa bibi yake yaani shngazi yangu.

Na kama niliyejua kwani Mustafa alimuuliza Rama.

“Mlikuwa wapi Rama?”

Rama akanitazama kisha akajibu.

“Tulikuwa kwa bibi?”

“Wapi?”

“Ilala. Mama anamuita shangazi.”

Sikutaka aendelee kumuuliza maswali, nikamuuliza Mustafa.

“Habari ya safari?”

“Nzuri, sijui nyinyi hapa.”

“Sisi hatujambo.”

“Naona safari hii umechelewa sana.”

“Si sana. Nimekaa wiki nne tu.”

“Siku nyingine ukichelewa sana ni wiki tatu tu.”

“Ndio. Hii wiki ya nne nilikuwa nasubiri nitumiwe pesa. Pesa zangu zilipungua. Huyo jamaa ndio aliyenichelewesha.”

“Kwani safari hii umeleta nini?”

“Nimekuja na spea za magari.”

“Spea za magari peke yake?’

“Nilipata oda ya spea za magari peke yake, sikununua bidhaa zingine.”

“Umeshazipeleka?”

“Ndio nataka nitoke hivi, niwaone hao jamaa.”

Mustafa akanyanyuka.

“Kwa hiyo hutakula?”

“Ni hapo nikirudi.”

“Upikiwe nini?”

“Chipsi zitatosha.”

“Sawa.”

Mustafa akatoka.

Mara tu baada ya Mustafa kuondoka simu yangu ikaita. Namba iliyokuwa inanipigia sikuwa nikiifahamu.

Nikaipokea.

“Hello…!

“Hello…habari yako?” Sauti ya kiume ikanisalimia.

“Nzuri.”

“Nazungumza na mke wa dereva Musa?”

Moyo wangu ukashituka. Nilishukuru kwamba Mustafa hakuwepo.

“Kwani wewe nani?”

“Mimi ni meneja wa kampuni anayofanya kazi ya udereva.”

“Ndiyo, mimi ni mke wake.”

“Kuna tukio limetokea…”

“Tukio gani?”

“Musa alipata ajali ya gari juzi wakati akirudi kutoka Zambia.”

“Haa! Yuko wapi sasa?”

“Leo ndio ameletwa Dar, yuko hospitali ya Muhimbili.”

“Hali yake ikoje?”

“Taniboi wake alifariki hapo hapo, yeye amevunjika miguu yote miwili.”

Mama yangu wee!

Nilihisi machozi yanataka kunitoka.

“Huo mwili wa taniboi wake pia umeletwa?” Nikauliza.

“Umeshaletwa, umepelekwa kijijini kwao, sijajua mazishi yatakuwa lini.”

Mmh! Niliguna kabla ya kuuliza.

“Mume wangu ndio amevunjika miguu?”

“Ilikuwa ajali mbaya sana. Ni jambo la kushukuru Musa kunusurika.”

Pakapita kimya cha sekunde kadhaa kabla ya sauti ya mtu huyo kusikika tena.

“Sasa unatakiwa ufike Muhimbili kumuona?”

“Sawa, nitafika.”

“Kama kutakuwa na tatizo lolote linalohusu pesa utanipigia kwa kutumia namba hii.”

“Sawa.”

Inaendelea…