
“NDIO dada.”
“Ukishakata simu nipigie tena. Nikipokea uniambie ninaitwa, shangazi amezidiwa. Umesikia?”
“Sawa. Nitakupigia.”
Simu ikakatwa. Nikatoka maliwatoni na kurudi sebuleni. Nilipoketi tu simu ikaita tena. Nikaitoa kwenye mkoba na kutazama namba. Ilikuwa namba ile ile ya mtumishi wangu.
Nikaipokea mbele ya Sele.
“Hello vipi huko?” Nikajidai kuuliza.
“Shangazi amezidiwa, hali imekuwa mbaya sana,” sauti ya mtumishi wangu ikasikika kwenye simu.
Nikajidai kugutuka.
“Amezidiwa sana?”
“Kwa kweli hali ni mbaya sana, unatakiwa uje haraka.”
“Sawa, basi nakuja.”
Wakati nakata simu Sele aliniulia.
“Nani amezidiwa sana?”
“Ni shangazi yangu.”
Nikainuka haraka haraka.
“Sele mimi naenda. Sijui kama shangazi yangu nitamkuta hai au atakuwa ameshakufa!”
“Basi wewe nenda, lolote litakalotokea utanipigia simu.”
“Sawa.”
Sele akanitoa nje.
Tulipotoka nje Sele alinipa shilingi laki moja ya ziada. Alinisindikiza hadi kituo cha teksi, akalipia kabisa pesa ya teksi. Nikaagana naye na kujipakia.
Wakati teksi ikiwa kwenye mwendo nilimwambia dereva anipeleke Mbezi.
“Utaniongeza pesa,” akaniambia.
“Hakuna tatizo.”
Tukiwa njiani Mustafa akanitumia meseji.
“Uko wapi?” Akaniuliza.
“Niko hapa kwa jirani, kwani wewe uko wapi?” Na mimi nikamuuliza nikifanya sijui kama yuko nyumbani.
“Niko nyumbani,” akanijibu.
“Nisubiri ninakuja,” nikamwambia kwenye meseji.
Nilipofikia Mbezi nilimlipa dereva pesa aliyotaka nimuongeze kisha nikafungua geti na kuingia ndani.
Mtumishi wetu aliponiona alinifuata kunako geti.
“Baba yuko chumbani,” akaninong’oneza.
“Alinitumia meseji,” nikamwambia. Kisha nikamuuliza.
“Hajakwambia kitu?’
“Hajaniambia. Aliingia chumbani, hajatoka.”
“Sawa.”
Bila shaka yule mtumishi alishajua kuwa nyendo zangu za nje hazikuwa na heri japokuwa sikuwa nimemfichulia ukweli wote.
Niliingia chumbani. Nikamkuta Mustafa amelala usingizi kabisa.
“Niliutia mkoba wangu kwenye kabati nikabadili zile nguo na kuvaa za nyumbani kisha nikamuamsha.
“Baba Rama, mbona umelala saa hizi?’
Mustafa akaamnka. Ute ulikuwa umemtoka kidogo akaufuta kwa mkono.
“Umesharudi?” Akaniuliza.
“Nimerudi muda mrefu, nilikuacha ulale. Naona umechoka.”
“Nilikuwa nakusubiri wewe nikapitiwa na usingizi.”
“Unatoka wapi?’
“Nilikwenda Buguruni na rafiki zangu tukanunua mbuzi tukamchinja na kugawana nyama.”
“Iko wapi hiyo nyama?”
“Huyo msichana ameiweka kwenye friza.”
“Ndio tuipike leo?”
“Ni karibu kilo nne, huwezi kuipika yote. Pika kiasi tu.”
“Sawa.’
“Na wewe ulikwenda kufanya nini huko kwa jirani?’
“Kumtembelea tu. Mara kwa mara anakuja kwangu kunisalimia na mimi leo nikaona nikamsalimie.”
“Ujirani huo…!”
“Una nini?”
“Mwisho mtazua umbea. Unajua mimi sipendi ushoga ushoga na watu ambao hujui tabia zao. Watakuharibu. Shauri yako.”
Mh! Kama ni kuharibika, nimeshaharibika siku nyingi, nilijisemea kimoyo moyo.
“Kwa hiyo hutaki nitembeleane na majirani zangu?” Nikamuuliza.
“Sio kwamba sitaki, uwe muangalifu na uchague jirani mzuri wa kufanya urafiki naye.”
“Huyo msichana ni mtu mzuri na ninamuamini, ana mume wake na hana tabia za ovyo ovyo.”
Mustafa alionyesha kutotaka kuendelea na zile shutuma akainuka kwenye kitanda na kuketi. Akaitazama saa yake kisha akaniuliza.
“Utapika nini, wali au ugali?’
“Kwani leo utakula hapa?”
“Ninatamani kula ugali, nitakula hapa. Hiyo nyama mnataka mle ninyi tu?’
“Basi tutapika huo ugali.”
“Mimi ninatoka kidogo lakini saa saba nitakuwa nimerudi.”
“Yako ni hayo tu, kwani ukisubiri hapa hapa itakuwaje?’
“Nina shughuli zangu, siwezi kukaa hapa hadi muda huo.”
“Haya bwana, wewe nenda tu utapikiwa huo ugali.”
Mustafa akainuka kitandani na kutoka. Alipotoka nilisubiri atoe gari nikafungua kabati na kutoa ule mkoba wangu, nikakaa kitandani.
Niliufungua nikatoa zile pesa nilizopewa na Sele na kuanza kuzihesabu. Nilihakikisha zilikuwa shilingi milioni moja taslim. Nikazificha ndani ya kabati mahali ambapo nilikuwa na hakika Mustafa asingeziona hata kama angepekua kabati hilo.
Nilipomaliza, nilitoka nikaenda kufungua friza na kuitazama hiyo nyama iliyoletwa. Nikamuita mtumishi wetu.
“Njoo na kisu na sufuria,” nikamwambia.
Mtumishi huyo alipofika nilichukua kisu nikakata pande la nyama na kulitia kwenye sufuria.
“Kaikatekate uibandike jikoni.”
“Niikaange?”
“Hapana, ichemshe kwanza.”
Mtumishi huyo alipokwenda jikoni nikaenda kuketi sebuleni.
Mustafa alirudi saa saba na nusu, alikuta ugali ukiwa tayari. Nikala pamoja na yeye. Baada ya kumaliza kula tu Mustafa akaondoka.
Nikabaki nyumbani hadi saa kumi na moja jioni Sele aliponipigia simu. Kwa vile nilikuwa nimekaa na mtumishi wetu niliingia chumbani na kupokea ile simu.
“Habari ya muda huu?” Sele akaniuliza.
“Nzuri, sijui wewe.”
“Hali ya shangazi inaendeleaje?”
Nilikuwa nimeshasahau kuwa nilimdanganya kuwa shangazi amezidiwa. Nikamjibu haraka.
“Ana nafuu kidogo”
“Nilikuwa nataka kukwambia kitu.”
“Niambie.”
“Nataka unipe jina lako kikamilifu pamoja na jina la mama yako.”
“Ya nini hayo majina?”
“Si ndio nataka kupanga ndoa, lazima tutazamie majina.”
“Sele huo ni ushirikina. Majina hayapangi ndoa. Ndoa inapangwa na watu.”
“We nitajie tu.”
“Halafu uyapeleke kwa mganga?”
“Najua mimi.” Sele akaniambia baada ya kusita kidogo.
“Jina langu ni Mishi binti Ramadhani na jina la mama yangu ni Hawa.”
Niliona nimtajie hayo majina kama alivyotaka. Lakini jina la mama yangu lilikuwa silo. Nilimtajia jina jingine.
Kama alikuwa anataka kwenda kuniroga anifanye zezeta wakati ananioa atajiroga mwenyewe.
“Umeridhika?” Nikamuuliza nilipoona yuko kimya.
Hakunijibu kitu, nikahisi alikuwa anaandika yale majina kwenye karatasi.
Baada ya kupita sekunde chache ndipo sauti yake iliposikika.
“Wewe pia ukitaka jina langu, la baba yangu na la mama yangu nitakupa.”
“Ya nini?”
“Naona kama umepata wasiwasi, wakati hii ni kawaida.”
“Lakini si nimeshakutajia.”
“Poa. Nitakupigia baadaye.”
“Sawa.”
Sele akakata simu.
Nikawa najiwazia peke yangu. Niliolewa na Musa kisha nikaolewa na Mustafa, hakuna mwanaume yeyote aliyeniuliza jina la mama yangu kabla ya ndoa. Lakini huyu Nswahili wa Ilala anataka jina la mama yangu. Anataka alifanye nini.
Nilichokuwa najua ni kuwa baadhi ya wanaume wanapotaka kuoa mke huchukua majina ya mke likiwemo na la mama yake na kwenda kuyatazamia kwa waganga.
Huko anaweza kuambiwa mwanamke huyu nyota yake ni kubwa kuliko ya mume na hivyo ukimuoa atakutawala.
Watu wengi wakisikia hivyo huzivunja nyota za wachumba zao ili wawatawale wao na kuwafanya mabwege. Mimi hilo sitalikubali na halitawezekana kwa sababu jina la mama nililompa si jina la kweli. Na mara nyingi jina lala mama ndilo linalotakiwa ili kuvunja nyota ya mke.
“Ameula wa chuya,” nikajiambia kimoyomoyo. “Kama yeye ni Mzaramo, mimi upande mmoja ni Mdigo wa Tanga, upande mwingine ni Muarusha, haniwezi,” niliendelea kujiambia.
Sele hakunipigia simu hadi siku ya pili yake. Alinipigia simu saa nne asubuhi wakati Mustafa hayuko nyumbani, akaniambia.
“Kuna kitu nataka kukuambia lakini naomba tukubaliane.”
“Kitu gani?” Nikamuuliza.
“Jina lako haliafikiani na langu katika ndoa. Nimeshauriwa nikuoe kwa jina jingine na si jina la Mishi,” akaniambia. Ni yale yale niliyokuwa nikiyawaza.
“Jina langu na lako haliafikiani kivipi?’
“Yaani nyota zetu hazikubaliani kuishi pamoja. Waswahili wanasema vumbi na upepo vikiwepo pamoja ni tatizo.”
“Sele mbona sikuelewi. Sasa nani ni upepo na nani ni vumbi.”
Sele akacheka.
“Nimekupa mfano tu. Haya mambo huwezi kuyaelewa, wazee wetu ndio wanajua na wanataka watutengezee maisha mazuri.”
“Sikiliza Sele, wewe unatiwa presha bure. Hayo mambo ya kutazamia majina ni ya kizamani. Siku hizi watu wanaoana tu. Hakuna vumbi wala upepo,” nikampa makavu.
“Mishi naomba tukubaliane kwa hilo. Ubishi haufai. Kama tumekubaliana kuoana ni vizuri tufuate zile taratibu za ndoa. Wewe kubali nikuoe kwa jina jingine.”
“Yaani hapo utakuwa umevunja nyota yangu sio?”
Inaendelea…