Viongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) wamesisitiza kuwa sababu kuu ya kuendelea vita Ukanda wa Gaza na kutofikia natija juhudi za usitishaji vita ni hadaa na ukwamishaji unaofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni.
Viongozi wa Hamas wameeleza kuwa mapatano yoyote watakayofikia na utawala wa Kizayuni ni lazima yajumuishe masuala ya kuondoka jeshi la utawala huo katika Ukanda wa Gaza, kufikiwa usitishaji vita wa kudumu, kuondolewa mzingiro wa Gaza na kurejea wakimbizi katika makazi yao.

Viongozi wa Hamas wamesema pia kuhusu hatua za nchi suluhishi kwa ajili ya kufanikisha usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza kuwa, Misri na Qatar zimetoa mapendekezo kwa ajili ya kusimamisha vita kwa siku kadhaa, kuongeza misaada ya kibinadamu na kubadilishana baadhi ya mateka hata hivyo mapendekezo hayo hayajumuishi kusitishwa kikamilifu mapigano na kuondoka utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kurejea Gaza wakimbizi wa Kipalestina katika makazi yao. Mapendekezo hayo aidha hayatoi jibu kwa mahitaji ya usalama ya raia, kwa misaada ya kibinadamu na kwa suala la kufunguliwa vivuko hasa kivuko cha Rafah.
Sami Abu Zuhri mmoja wa viongozi wa Hamas amesema: “Wamarekani wanataka kufikiwa makubaliano ya wazi huko Gaza; Hamas haijakataa wito wowote kwa madhumuni ya kupatikana njia ya ufumbuzi. Hatuwezi kuwakabidhi mateka wa maghasibu katika hali ambayo wanaendelea kuwaua wananchi wa Palestina. Mpango uliowasilishwa kwa Hamas haudhamini matakwa ya wananchi wa Palestina,” amesema Abu Zuhri.

Wakati huo huo, Najib Miqati Waziri Mkuu wa serikali ya Lebanon amesema katika mazungumzo na Meja Jenerali Aroldo Lázaro Sáenz Kamanda wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon (UNFIL) kwamba: Kupanuka kwa wigo wa hujuma za adui Israel katika maeneo tofauti ya Lebanon kwa mara nyingine tena kunathibitisha upinzani wa adui Mzayuni kwa juhudi zote zilizofanywa za kufikia usitishaji vita mkabala wa maandalizi ya kutekeleza kikamilifu azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la UN. Waziri Mkuu wa Lebanon amebainisha haya baada ya Antony Blinken Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kudai kuwa timu ya mazungumzo imepiga hatua nzuri kuhusu suala la kusimamisha vita huko Lebabon. Viongozi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wanatoa madai ya kusitisha vita katika hali ambayo jeshi la utawala huo tangu Jumatatu tarehe 23 Septemba linaendesha mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo mbalimbali kusini mwa Lebanon.

Katika miezi ya hivi karibuni, kufuatia kupanuka vita vya utawala wa Kizayuni na kuibuka hali ya machafukoge katika eneo, viongozi wa Marekani na wa utawala wa Kizayuni wanadai kuwa wamezingatia mipango mbalimbali kwa ajili ya usitishaji vita. Madai haya yanatolewa katika hali ambayo mashambulizi ya Wazayuni dhidi ya Gaza na Lebanon kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani yanaendelea na hata yameshtadi pia katika siku za karibuni. Kwa mfano, Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza kuwa watu wasiopungua 52 wameuawa shahidi na zaidi ya 70 kujeruhiwa katika mashambulizi ya juzi ya anga ya jeshi la Israel katika eneo la Baalbek huko Lebanon.
Kwa hiyo, viongozi wa makundi ya muqawama wa Palestina wametambua vyema malengo la ukwamishaji wa Marekani na utawala wa Kizayuni na kusisitiza kanuni na misingi yao isiyobadilika kwa ajili ya kusitisha vita. Kuondoka Gaza wanajeshi vamizi, kurejea katika makazi yao wakimbizi ni kati ya misingi mikuu ambayo inatiliwa mkazo na Wapalestina katika mchakato wa mazungumzo yoyote au mpango wa usitishaji vita kwa lengo la kutetea na kudai haki zao halali.
Usama Hamdan Mwakilishi wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuhusu suala hili kwamba: Si mantiki kuzungumzia usitishaji vita wa upande mmoja kwa sababu tunachotaka ni kusimamishwa kikamilifu mashambulizi dhidi ya wananchi wa Palestina. Muqawama umegharimika pakubwa katika njia hii, na serikali ya Marekani ilikusudia kunufaika na suala la mazungumzo kwa maslahi ya uchaguzi wa nchi hiyo na kutenganisha njia ya kambi za muqawama hata hivyo imefeli. Kile kinachofanywa na serikali ya Marekani ni kushiriki kikamilifu katika jinai; na lau ingetaka kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel basi ingesita kuwapatia maghasibu silaha na zana za kijeshi.