
Rome. Vatican imesema kuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis hayuko tena kwenye hatari ya kifo kutokana na maradhi yanayomsumbua, huku ikieleza kuwa dawa anazotumia zimeanza kuonyesha matokeo chanya kwenye mwili wake.
Taarifa ya Vatican leo Jumanne Machi 11, 2025, imesema kuwa ishara ya maendeleo na kuimarika kwa afya ya kiongozi huyo imeonekana jana kwenye mfumo wa mapafu yake.
Papa Francis (88) amelazwa katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma kwa zaidi ya wiki tatu zilizopita. Alilazwa Februari 14, 2025, akisumbuliwa na maambukizi makali kwenye mfumo wa upumuaji ambayo yamewalazimu madaktari wanaomtibu kumuweka katika uangalizi wa karibu wa afya yake.
Katika taarifa yake ya hivi karibuni ya kiafya, Vatican ilisema madaktari wa papa wameshaondoa hali ya tahadhari juu ya afya ya kiongozi huyo wa kiroho wakimaanisha, hayupo tena kwenye hatari ya kifo kutokana na maradhi hayo.
“Maendeleo yaliyoonekana katika siku zilizopita yamezidi kuimarika kama ilivyothibitishwa na vipimo vya damu na tathimini za kitabibu pamoja na mwitikio mzuri kwa matibabu ya dawa,” imeeleza taarifa hiyo ya Vatican.
Ingawa madaktari wameondoa utabiri wao wa awali, Vatican ilisema bado wanatarajia Papa Francis kuendelea na matibabu ya dawa hospitalini kwa siku zaidi. Pia, hakuna muda maalumu uliotajwa kuhusu lini ataondoka hospitalini.
Inaelezwa kuwa Papa Francis aliendelea kuwa katika hali thabiti ama inayoimarika kwa wiki iliyopita, baada ya kukumbwa na hali za dharura mara mbili katika kipindi cha wiki moja iliyopita.
Vatican pia ilisema mapema Jumatatu iliyopita kuwa Papa Francis anaendelea na matibabu yake na tiba ya ugonjwa ulioko kwenye mfumo wa upumuaji ili kumsaidia kupumua.
Vatican pia ilisema kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, ambaye amekuwa akitumia kiti cha magurudumu kwa miaka ya hivi karibuni kutokana na maumivu ya goti na mgongo, pia anaendelea na tiba ya mwili kusaidia utembeaji wake.
“Papa anaendelea kupumua kwa kusaidiwa na oksijeni hospitalini, akitumia bomba dogo la oksijeni chini ya pua yake wakati wa mchana na mashine ya kusaidia kupumua usiku anapolala,” imesema taarifa hiyo.
Historia ya maradhi
Papa amepitia vipindi kadhaa vya maradhi katika miaka miwili iliyopita na huwa rahisi kupata maambukizi ya mapafu kwa sababu aliwahi kuwa na pleurisi akiwa kijana na sehemu ya pafu lake moja kuondolewa.
‘Nimonia’ ni maambukizi makali katika njia ya mapafu yote mawili ambayo yanaweza kusababisha yavimbe na kupata makovu, hivyo kufanya iwe vigumu kupumua.
Papa Francis, ambaye ataadhimisha miaka 12 tangu kuchaguliwa kwake kama papa Alhamisi, hajaonekana hadharani tangu alipoingia hospitalini, ikiwa ni kipindi kirefu zaidi cha kutokuwepo kwake kwa umma tangu awe papa.
Papa, anayejulikana kwa kufanya kazi kupita kiasi, ameendelea kufanya kazi kutoka hospitalini.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari