#HABARI: Jeshi la Polisi limetoa taarifa ya uchunguzi wa tukio ambalo lilisambazwa katika mitandao ya kijamii kupitia picha mjongeo (video clip) kuanzia Agosti 2, 2024 ikimwonyesha binti mmoja akifanyiwa vitendo vya ukatili.
Akitoa taarifa hiyo Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu kamishna wa Polisi DCP – David Misime, amesema watuhumiwa wanne wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na tukio la udhalilishaji wa kijinsia, Aidha uchunguzi umebaini tukio hilo lilifanyikia eneo la Swaswa katika Jiji la Dodoma mwezi Mei 2024.
Pia Uchunguzi uliofanyika hadi sasa umefanikisha kumpata binti aliyefanyiwa ukatili huo na amehifadhiwa eneo salama na anaendelea kupata huduma zinazostahili kupewa mtu aliyefanyiwa ukatili wa aina hiyo.