Haaretz: Zaidi ya Wazayuni 10,000 wameshakimbilia Canada mwaka huu kutokea Israel

Idadi ya walowezi wa Kizayuni wanaokimbilia Canada imeongezeka kwa kasi kutokana na vipigo inavyopata Israel kutoka kwa wanamapambano wa Lebanon na Palestina.

Gazeti la Kizayuni la Haaretz limeripoti habari hiyo na kuongeza kwamba zaidi ya walowezi 10,000 wamekimbilia Canada katika ardhi za Palestina walizokuwa wanazikalia kwa mabavu kutokana na vipigo vikali wanavyopata kutoka kwa wanamapambano wa kambi ya Muqawama. 

Ripoti ya gezeti hilo imesema kuwa, Wazayuni 7,850 wameshaomba na kupokea visa za kazi za Canada tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2024, ikibainisha kuwa, hilo ni ongezeko la mara tano zaidi ikilinganishwa na mwaka jana. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2023, Waisraeli 1,585 walipokea visa za kazi za Canada.

Wimbi la walowezi wa Kizayuni wanaokimbia Israel limeongezeka sana kutokana na vipigo vya wanamapambano wa kambi ya Muqawama 

Gazeti hilo la Israel limeongeza kuwa, miongoni mwa sababu za kuweko wimbi hilo kubwa la wakimbizi wa Kizayuni ni hali tete ya kisiasa na kiusalama ya Israel, pamoja na kuongezeka migogoro, dhulma za kijamii na kushindwa utawala wa Kizayuni kushughulikia masuala muhimu.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni kabisa zilizotolewa na Wizara ya Uhamiaji ya Canada, vibali 3,425 vya kazi ya muda na 4,424 vya kazi vya kawaida vimetolewa kwa walowezi wa Kizayuni kati ya mwezi Disemba 2023 na mwishoni mwa mwezi Septemba 2024.

Mapema wiki hii, tovuti ya habari ya Ynet ilinukuu takwimu kutoka Ofisi Kuu ya Takwimu ya Israel (CBS) ikifichua ongezeko kubwa la idadi ya walowezi wa Kizayuni walioamua kuishi nje ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, hata kabla ya utawala huo ghasibu kuanzisha mashambulizi yake ya kikatili dhidi ya Ghaza zaidi ya miezi 13 iliyopita.