Haaland, Raizin katika vita mpya

MSHAMBULIAJI wa TMA, Abdulaziz Shahame ‘Haaland’ amesema vita yake iliyopo ya ufungaji na nyota wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh inamfanya kutobweteka bali kuendelea kupambana zaidi, huku akieleza kila mchezo kwake anauchukulia kwa usiriaz.

Kauli yake inajiri baada ya nyota hao kupishana mabao mawili, Shahame akifunga mabao 12 huku Raizin ambaye ndiye kinara akiwa na 14, wakifuatiwa na Andrew Simchimba wa Geita Gold aliyefunga tisa, wakati Naku James wa Mbuni FC ya Arusha amefunga saba.

“Nafurahia kuona ushindani uliopo kwa sababu unanipa changamoto ya kuzidi kuongeza juhudi zaidi, siangalii tu vita yangu ya ufungaji, isipokuwa napambania pia timu yetu ifanye vizuri na ipande Ligi Kuu Bara msimu ujao ikiwezekana,” alisema.

Shahame aliyejiunga na timu hiyo msimu wa 2022-23 akitokea Pan Africans baada ya kuachana na Mbeya Kwanza, aliongeza msimu huu umekuwa ni mgumu, ingawa jambo analoliombea ni kutopata majeraha ili aendelee kushindana na wapinzani wake.

Msimu uliopita nyota huyo alifunga jumla ya mabao 10, katika Ligi ya Championship hivyo, kuivuka rekodi yake mwenyewe, huku akiweka wazi siri ya mafanikio hayo ni kutokana na ushirikiano anaoupata kutokea kwa wachezaji wenzake kikosini.