Haaland aweka rekodi ya mabao City

Manchester, England. Mshambuliaji wa Manchester City Erling Haaland ameweka rekodi ya kufunga mabao 100 akiwa na timu hiyo.

Staa huyo amefanikiwa kuweka rekodi hiyo baada ya kufunga bao moja jana kwenye mchezo wa Ligi Kuu  dhidi ya Arsenal ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 kwenye Uwanja wa Etihad.

Haaland amefunga bao hilo kwenye mchezo wa 105 akiwa na timu hiyo ya Manchester na kufikia rekodi ambayo aliwahi kuiweka staa wa zamani wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo.

Haaland alifanikiwa kufunga bao la kwanza kwenye mchezo huo katika dakika ya tisa ya mechi hiyo.

Ameonekana kuwa na wakati mzuri tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Borussia Dortmund mwaka 2022.

Ronaldo alifikisha idadi hiyo mwaka 2011 akiwa amecheza idadi hiyo ya michezo akiwa na Real Madrid.

Ronaldo alimaliza kipindi chake akiwa na Real Madrid akiweka rekodi ya kufunga mabao 450 kwenye michezo 428  mwaka 2018, hata hivyo ,jumla Ronaldo ana mabao zaidi ya 900 kwenye timu zote alizozichezea kwa sasa akiwa na Al Nassr.

Kwa upande wa Haaland amefunga mabao 73 kwenye michezo ya Ligi Kuu England akiwa amefunga mabao 18 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na mabao tisa kwenye michuano mingine.

Klabu ya Man City imetoa taarifa ya kumpongeza mchezaji huyo, taarifa hiyo ikisema kuwa ni wa 19 kufunga mabao 100 akiwa na City.

“Kila mmoja kwenye kikosi cha Manchester City tunataka kumpongeza Erling kutokana na rekodi hii mpya aliyoiweka akiwa na timu hii, tunaamini kuwa bado ana nafasi kubwa zaidi ya kufanya vizuri,” ilisema taarifa hiyo.

Staa huyo jumla amefanikiwa kufunga jumla ya mabao 305 kwenye michezo 255 akiwa tayari ana makombe mawili ya Ligi Kuu England.