
Nchini Guinea, familia za waathiriwa wa mkasa wa Nzérékoré wamewasilisha malalamiko dhidi ya mamlaka ya mpito. Mnamo Desemba 1, 2024, uwanja wa michezo wa jiji hilo uliokuwa na watu wengi kupita kiasi ulikumbwa na tukio baya la mkanyagano wakati wa mechi ya kandanda iliyoandaliwa kwa heshima ya Jenerali Mamadi Doumbouya.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Watu 56 walifariki, kulingana na ripoti rasmi ya serikali, angalau 140 kulingana na muungano wa mashirika yasiyyo ya kiserikali katika eneo la Nzérékoré, ambao ripoti yao ya uchunguzi inanyooshea kidole “nia ya mamlaka ya kuficha ukweli” kuhusu hali halisi ya tukio hilo baya la mkanyagano.
Kwa jumla, familia 98 ziliwasilisha malalamiko siku ya Jumatatu, Machi 10, kwa mahakama ya mwanzo ya Nzérékoré (TPI) kwa takriban makosa kumi na tano na uhalifu, ikiwa ni pamoja na “mauaji, kuua bila kukusudia, kushindwa kutoa msaada, kuhatarisha wengine na kuficha maiti.” Malalamiko haya yote yanalenga waandaaji wa mechi, lakini haswa polisi, wanajeshi na viongozi wa kisiasa wa Nzérékoré, pamoja na Waziri wa Afya, Félix Lamah, na Waziri wa Michezo, Kéamou Bogola Haba, wote waliokuwepo kwenye uwanja wakati wa mkanyagano.
Hakuna uchunguzi wa “wazi”
“Tumegundua kuwa hakuna uchunguzi uliofunguliwa. Hakuna waathiriwa waliopokelewa, wala ndugu wa waathiriwa. Kwa hiyo, kwa makubaliano ya wahanga hao na wazazi wa wahanga ambao nao wapo katika harakati za kujipanga katika shirika, tumeamua kuwasilisha malalamiko ya mara kwa mara. Kinachoonekana wazi ni kwamba magari ya viongozi hao yalipita juu ya watazamaji vijana waliokuwa pale. Lango likawaangukia watu, magari yalipita juu yao na hapo ndipo kulitokea vifo vingi zaidi. “Miili hii yote ambayo ilisafirishwa hadi hospitali, mingi ilitoka huko,” anaelezea wakili Paul Lazard Gbilimou, akizungumza na Sidy Yansané, kutoka kitengo cha RFI kanda ya Afrika.
Kufichwa kwa maiti
Kunazungumzia kufichwa kwa maiti. Lakini hii ina maana gani? “Miili ilipelekwa katika kambi ya kijeshi, kwenye kambi ya mkoa wa nne wa kijeshi. Miili ilipelekwa huko na mpaka sasa hivi, hatujui miili hii ilikwenda wapi, kwa sababu mpaka sasa, kuna wazazi ambao hawana habari za watoto wao, kuna waume ambao hawana habari za wake zao, na kadhalika, wakili pia anabainisha. Kwa hiyo, tunaamini kwamba maiti hizi zilizokuwa kambini ni miili ambayo haijapatikana mpaka sasa, (na hii) wakati wazazi hawa wakiendelea kuomba miili yao, ili waweze angalau kuizika kwa heshima. “