
Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola amethibitisha kwamba hali ya timu yake ni tete na ikiwa watapoteza mchezo ujao rasmi watakuwa wamelipoteza taji la Ligi Kuu England msimu huu.
Mabingwa hawa mara nne wa EPL, wikiendi iliyopita waliweka historia ya kupoteza kwa kichapo cha mabao mengi zaidi katika uwanja wao wa nyumbani chini ya Guardiola baada ya kufungwa mabao 4-0 dhidi ya Tottenham.
Licha ya kichapo hicho, Man City imeendelea kusalia katika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 23.
Akizungumzia hali ya kikosi chake, Guardiola alisema: “Bila shaka kila kitu hakipo sawa. Katika miaka minane hatujawahi kukutana na hali kama hii. Kwa sasa sisi ni wanyonge. Wakati mwingine unapaswa kupitia hali hii. Unapaswa kukubaliana nayo, huu sio wakati wa kuanza kulaumiana, inatakiwa tukae pamoja na tushikamane, hatupaswi kukimbia,” alisema Guardiola.
Kocha huyo pia alisema huu ni wakati ambao wachezaji na timu kwa ujumla inabidi ishikamane zaidi kuliko ilivyowahi kuwa hapo awali na kitu pekee kinachowatofautisha wao ni pale wanapopitia changamoto husimama na kuzikabili kwa pamoja.
Guardiola, ambaye amepoteza mechi tano kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya ukocha amesema jambo zuri kwake ni kwamba wachezaji wake huwa wanakosa amani na kuwa na mawazo sana pale wanapopoteza mchezo.
“Kutakuwa na tatizo kama wachezaji wangu hawakuwa na wasiwasi au kama mimi sitakuwa na wasiwasi. Sijui nini kitakachotokea msimu huu, lakini hata kwa sekunde moja sitashindwa kuamini wachezaji. Hakuna timu duniani inayoweza kudumisha mafanikio kwa miaka minane, tisa, kumi mfululizo.”
Kocha huyu pia alizungumzia kuhusu mbio za ubingwa akisema ikiwa watapoteza tu mchezo wao wa wiki ijayo dhidi ya Liverpool basi watakuwa wameaga vita ya ubingwa.
“Ndio tunaweza kuondolewa kwenye mbio ikiwa watashinda mechi yao ya kesho (jana) na ijayo. Kuna sababu nyeti za kupoteza mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu England, jambo la umuhimu kwa sasa ni kujaribu kushinda mechi ijayo.”
Man City pia imekuwa timu ya kwanza bingwa mtetezi wa EPL na kupoteza mechi tano mfululizo za michuano yote katika msimu mmoja tangu ilipofanya hivyo Chelsea mwaka 1956, pia ilikuwa ni mara ya kwanza wanapoteza mechi ya EPL kwenye uwanja wa nyumbani baada ya kutofanya hivyo katika mechi 35.
Kichapo kutoka kwa Liverpool katika mchezo ujao utakaopigwa kwenye dimba la Anfield, kinaweza kuwafanya kuwa pointi 11 nyuma ya Liverpool.
Man City ina kibarua cha kucheza Ligi ya Mabingwa dhidi ya Feynoord Jumanne kabla ya kukutana na Liverpool mwisho wa wiki hii.
Mchezo wa mwisho kwa matajiri hawa wa Jiji la Manchester kupata ushindi ilikuwa ni dhidi ya Southampton, Oktoba 26.