Manchester, England. Manchester City imemsajili nyota wa Eintracht Frankfurt, Omar Marmoush, kwa mkataba wa miaka minne na nusu ambapo City imekubali kutoa kiasi cha ada ya uhamisho wa shilingi 227 bilioni.
Marmoush, mwenye umri wa miaka 25, amekuwa na wakati mzuri msimu huu akiwa Frankfurt ambapo amefunga mabao 20 na kutoa pasi 14 za mabao katika mechi 26 alizocheza.

Baada ya kusaini mkataba wa miaka minne na nusu, mshambuliaji huyo raia wa Misri atacheza chini ya Pep Guardiola, akichukua nafasi ya Julian Alvarez ambaye alijiunga na Atletico Madrid mwanzoni mwa msimu huu.
“Leo ni siku nitakayoikumbuka daima, nimefurahi kusajiliwa na Manchester City moja ya klabu bora zaidi duniani. Familia yangu inajivunia kuniona nipo hapa Manchester City.” Amesema Marmoush.

Marmoush anakuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na City dirisha hili la Januari, baada ya mabeki wa kati Abdukodir Khusanov na Vitor Reis kujiunga na klabu hiyo. Marmoush anatarajiwa kupunguza mzigo wa kufunga mabao uliokuwa unamkabili Erling Haaland na kuongeza nguvu mbadala ya ushambuliaji.
Kasi yake, uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali, na utulivu wakati wa kushambulia vilimfanya Pep Guardiola kuvutiwa na mshambuliaji huyu.