Guardiola akiri kinachoitesa Man City

Manchester, England. Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ameelezea kipigo cha mabao 3-2 ambacho timu yake imekipata nyumbani jana Februari 11, 2025 ni kama ishara ya kushuka kwa ubora wao.

Katika mchezo huo ambao umechezwa katika Uwanja wa Etihad, Man City licha ya kutangulia kufunga bao mara mbili, iliwaruhusu Real Madrid kusawazisha na kupata bao la ushindi katika dakika za nyongeza za mechi hiyo.

Matokeo hayo yanaifanya Man City kuwa na mlima mrefu wa kupanda katika mechi ya marudiano itakayochezwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, Jumatano ijayo, Februari 19 ili itinge hatua ya 16 bora.

Guardiola amesema kuwa timu yake haipo kwenye ubora ambao imekuwa nao hivyo wana kazi kubwa ya kufanya katika mechi zilizo mbele yao.

“Inatokea mara nyingi msimu huu. Maamuzi mabaya, ndiyo hayo tu. Ninakubali. Sio kuhusu mimi na wewe, au timu tu, ni kila mtu.

“Hatujatulia vya kutosha. Nimekuwa hapa kwa miaka mingi na tumekuwa timu isiyo ya kawaida,

Mwaka huu nakubali mpinzani anapokuwa bora lakini kwa sasa siko katika hali nzuri kutoa utulivu kwa timu na kusimamia hali hii.

“Uwajibikaji ni wetu sote, sio wachezaji pekee. Kwangu mimi itakuwa rahisi kumlaumu mchezaji fulani lakini huo ni ujinga na haufanyi kazi, ni mimi wa kwanza na wachezaji pia. Ukweli ni kwamba hatuko imara vya kutosha katika nyakati hizo. Leo sio ubaguzi, ilitokea mara nyingi. Leo ndivyo ilivyo, kesho unapaswa kuendelea na kuwa na miguu safi na akili safi,” amesema Guardiola.

Katika mechi ya marudiano, Manchester City inahitajika kupata ushindi wa utofauti wa mabao mawili ili iweze kutinga hatua ya 16 bora.