Google kuja na ‘AI chatbot’ kwa watoto

Dar es Salaam. Kampuni ya teknolojia ya Google imesema ipo mbioni kuzindua programu ya Akili Mnemba ya mazungumzo (AI Chatbot) ya Gemini ambayo itakuwa mahususi kwa watoto walio chini ya miaka 13.

Kwa mujibu wa The New York Times ya nchini Marekani toleo hilo itaanza wiki ijayo kwa watoto ambao akaunti zao za Google zinasimamiwa na wazazi kupitia huduma ya Family Link.

Imeeleza hatua hiyo ni sehemu ya mipango ya kampuni kuvutia watumiaji wadogo kupitia bidhaa za Akili Mnemba katika kuwasaidia watoto kuuliza maswali, kupata msaada wa kazi za shule na masuala ya hadithi.

Itakavyokuwa ni kwamba watoto watatumia Gemini kupitia akaunti zilizoundwa chini ya mfumo wa Family Link, ambao huruhusu wazazi kusimamia huduma kama Gmail na YouTube kwa watoto wao. Ili kutengeneza akaunti ya mtoto, mzazi lazima atoe taarifa binafsi zikiwamo jina na tarehe ya kuzaliwa ya mtoto.

Msemaji wa Google, Karl Ryan amesema Gemini itakuwa na vizuizi mahsusi kulinda watoto dhidi ya maudhui hatarishi yanayoweza kuhatarisha ustawi wao.

Hatua hiyo inakuja wakati shule, vyuo na mashirika mbalimbali duniani bado yanapambana na athari za teknolojia ya Akili Mnemba, zinazoweza kuandika maandiko au kuzalisha picha za kuaminika kutoka mtandaoni.

Duniani tayari mamilioni ya vijana wanatumia chatbots kwa msaada wa masomo, ushauri wa uandishi na hata kama marafiki wa kidijitali.

Lakini mashirika ya watoto, likiwemo Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), imeonya Akili Mnemba inaweza kuwachanganya, kuwapotosha au hata kuwadanganya watoto ambao bado hawawezi kutofautisha kati ya binadamu na mashine.

UNICEF iliwahi kusema “AI ya kizazi kipya imeshazalisha maudhui hatari”, Google ilikiri hatari hizo katika barua pepe yake kwa wazazi, ikieleza “Gemini inaweza kufanya makosa” na kuhimiza wazazi kuwasaidia watoto wao kufikiri kwa umakini kuhusu majibu wanayopata.

Hata hivyo, barua hiyo ilipendekeza wazazi wawafundishe watoto jinsi ya kuhakiki ukweli wa majibu ya Gemini, wakikumbusha pia kwamba: “Gemini si binadamu na mtoto asitoe taarifa binafsi au nyeti kwa Gemini.”

Ingawa kampuni inajaribu kuchuja maudhui yasiyofaa, bado kuna uwezekano watoto wakaona vitu ambavyo wazazi hawataki waone.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Mei 5, 2025 mzazi Herieth Marwa mwenye mtoto aliyeko kidato cha kwanza amesema hatua hiyo ni nzuri kwa sababu mtoto atatumia kujifunza na kuona vitu vilivyo ndani ya umri wake hasa katika kujifunza.

Amesema mtoto atajifunza mambo mengi na itamsaidia kwa kuwa hajawahi kuona programu ya AI iliyokuja na mpango huo wa kulinda watoto.

“Mtoto wangu ana umri wa miaka 13 yuko kidato cha kwanza huwa anatumia AI kujifunza mambo ya shuleni akiwa huko na hata akirudi nyumbani.

“Akianza kutumia hii iliyoweka muda wa miaka 13 sitakuwa na wasiwasi maana najua haitompa nafasi pengine ya kutafuta vitu vingine visivyo na umri wake,” amesema mzazi huyo.

Akizungumzia faida yake amesema, Akili Mnemba za mazungumzo zinasaidia kupata maarifa zaidi ukilinganisha na kitabu ambacho kimewekewa ukomo (limited).

“Mfano mada ya shuleni akitafuta kwenye AI itamletea mambo mengi zaidi ambayo yako kwenye mtandao yanayohusiana na mada husika hivyo akili yake itatanuka zaidi,” ameeleza.

Aidha amesema Akili Mnemba ni nzuri kwa kujifunzia na si katika kujibia mitihani na mazoezi anayopewa na mwalimu wake.

Kwa upande wake Rashid Mansa aliyejikita sekta ya teknolojia na dijitali anasema faida yake itasaidia watoto hasa walio chini ya darasa la sita kimasomo hasa wale wanaosoma shule zinazotumia kompyuta.

“Pia, hasara yake itadumaza ubongo na zile motisha za kwenda maktaba kusoma vitabu kwa kuwa Akili Mnemba hiyo ina kila kitu,” amesema.

Amesema itawezekana mtoto akapewa taarifa zisizo za kweli na itatengeneza tabaka kwa wenye uwezo wa kupata simu na wasio nao.

Hata hivyo katika hatua nyingine ya kusaidia watoto Google imewahi kuja na huduma kwa watoto, ikiwemo YouTube Kids iliyozinduliwa mwaka 2015.

Kwa upande mwingine kampuni kubwa kama Google, Amazon na Microsoft tayari zimelipa faini kubwa kwa kuvunja sheria ya Marekani ya ulinzi wa faragha ya watoto mtandaoni, ambayo inataka ruhusa ya mzazi kabla ya kukusanya taarifa za mtoto aliye chini ya miaka 13.

Kwa mujibu wa Google, wazazi watajulishwa pindi mtoto wao atakapoanza kutumia Gemini kwa mara ya kwanza na wataweza kusimamia mipangilio ya chatbot hiyo, ikiwemo kuizima kabisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *