Gomez aletewa mtu Wydad AC

WYDAD AC inaripotiwa kutaka kumsajili mshambuliaji wa Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Relebohile Mofokeng nafasi anayocheza pia Mtanzania Selemani Mwalimu ‘Gomez’ aliyetambulishwa mwezi uliopita kikosini hapo.

Gomez tangu atambulishwe na vigogo hao amecheza mechi moja kwa dakika 30 dhidi ya COD Meknes timu hizo zilipotoka sare ya 0-0 na katika mchezo huo, bao la Mtanzania huyo lilikataliwa kwa madai alikuwa ameotea.

Inaelezwa kocha wa timu hiyo, Msauzi Rulani Mokwena ameushinikiza uongozi kuipata saini ya chipukizi huyo ambaye awali ilidaiwa nawindwa na Barcelona.

Matamanio makubwa ya Mokwena ni kuipata saini ya Mofokeng ili akaisaidie timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu la FIFA itakayoanza June na miamba hiyo ambayo mara ya mwisho kubeba taji la Ligi Kuu ya Morocco (Botola Pro) ni msimu wa 2021/22 itakipiga na Manchester City.

Endapo Wydad itamsajili Mofokeng mwenye mabao matatu na asisti mbili kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huenda kazini kwa Gomez ambaye alianza kupata nafasi ya kuaminiwa kikosi hapo kukawa na kazi.

Mkali huyo wa kufumania nyavu hadi sasa rekodi yake ya kufunga mabao sita haijafikiwa na nyota wenzake wa Fountain Gate katiika Ligi Kuu Bara  huku Salum Kihimbwa akisaliwa na mabao mawili kumfikia na zimesalia mechi nane ligi kumalizika.