LONDON, ENGLAND: BAO lile. Hapana, sio bao. Ni ubishani unaojitokeza mara kwa mara kwenye mchezo wa soka, inapotokea mpira uliopigwa haukuonekana sawasawa kama umevuka mstari wa goli au la.
Mfano halisi wa tukio kama hilo kwa kipindi cha karibuni ni lile shuti la Stephane Aziz Ki baada ya shuti lake alilopiga kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, kwamba mpira haukuonekana kwa usahihi kama umevuka mstari wa goli au la.
Utata wa aina hiyo sasa unamalizwa na kinachofahamika kama goal-line technology.

Goal-line technology au inafahamika kwa jina jingine kama Goal Decision System ni mfumo wa vifaa vya umeme unaosimikwa kwenye magoli ya uwanjani kwa ajili ya kutumika kwenye kusaidia kutoa uamuzi kwenye mchezo kama mpira uliopiga umevuka mstari wa goli au la, ili ihesabike kuwa ni bao au si bao.
Kwenye maelezo mapana zaidi, mfumo huo unatumika kufichua kama mpira umevuka wote kwenye mstari wa goli, ambapo inapokea hivyo, kifaa maalumu cha umeme kilichotambua kwamba mpira umevuka wote mstari wa goli, kinatuma ujumbe kwenye saa maalumu, ambayo amevaa mwamuzi wa mchezo kwamba hilo ni bao.
Wakati mwingine kwenye macho ya kawaida, mpira unaweza kuonekana kama umevuka mstari, jambo ambalo wakati mwingine waamuzi wamekuwa wamekuwa wakiamuru kuwa hilo ni bao, kumbe kwenye uhalisia, mpira huo haujavuka wote na kwamba kama kungekuwa na matumizi ya teknolojia hiyo ya kuweka kamera na vifaa vingine vya umeme kwenye goli, vingesaidia kutoa uamuzi kutambua kama hilo ni bao au si bao.

Lengo la goal-line technology (GLT) si kubadili majukumu ya mwamuzi, lakini ni kumsaidia katika kufanya uamuzi wake. GLT ni lazima ithibitishe kwamba mpira wote umevuka mstari wa goli na kisha kifaa hicho kinatuma taarifa kwa mwamuzi ili kumsaidia kufanya uamuzi wa mwisho.
Kwa kulinganisha na teknolojia nyingine zinazotumika kwenye michezo, goal-line technology imeingizwa kwenye soka miaka ya karibuni, kuna baadhi ya vyama vya mchezo huo vimekuwa vikitumia kwenye michuano yake huku vingine vikiendeelea kupinga na kusuasua kutumia kutokana na sababu tofauti. Kuna baadhi ya nchi, vyama vyake vya soka vinashindwa kutumia teknolojia hiyo kutokana na gharama zake.
Julai 2012, Bodi ya Kimataifa ya Vyama Vya Soka (IFAB) ambayo ni wasimamizi wakubwa wa sheria 17 za mchezo wa soka, zilipitisha matumizi ya goal-line technology, ikisema itumike, lakini si lazima. Kutokana na matatizo ya kiuchumi na gharama zake za kuwa na goal-line technology, teknolojia hiyo imekuwa ikitumika kwenye michuano ya ngazi kubwa.
Goal-line technology kwa sasa inatumika kwenye Ligi Kuu kubwa za Ulaya na kwenye michuano mingine ya kimataifa tangu mwaka 2014, ambapo kwenye fainali zote za Kombe la Dunia kwa timu za kike na kiume, inatumika.

GLT dhamira yake kubwa na lengo lake ni kubainisha kwa usahihi kwamba bao limefungwa, hasa inapotokea mazingira magumu ya mwamuzi kuona kwa macho ya kawaida, endapo mpira huo haukugusa nyavu au kuvuka mstari wa goli kwa mita kadhaa.
Jinsi Inavyofanya kazi
Ni mfumo unaotumia kamera zaidi. Kamera hizo zinategeshwa kuelekea lilipo goli, hasa kwenye mstari wa goli, ambao ule unaochorwa kutoka mlingoti mmoja hadi mwingine. Lakini, ukiweka kando kamera hizo, mpira pia unatumika kwenye mechi hiyo ili teknolojia hiyo ifanye kazi vyema, utakuwa umewekwa sensa ndani, ambapo ikitokea umevuka tu mstari, vifaa hivyo vinawasiliana na kutuma ujumbe kwenye kifaa kingine maalumu, ambacho kinasukuma ujumbe huo kwenda kwenye saa ambayo atakuwa ameivaa mwamuzi, ambayo inahusiana na mfumo mzima. Mfumo wote huo ni wa umeme.

Mfano wa mfumo wa GLT ni ule wa Hawk-Eye, ambao ni mfumo maarufu wa kamera unaotumika kwenye ligi mbalimbali pamoja na michuano mingine.
Mfumo mwingine ni wa GoalControl, ambao pia unatumia kamera na huu ulitengenezwa na kampuni za Ujerumani.
Teknolojia hiyo inakubalika kutokana na kuondoa utata wa mabao wa kimarohani, ambayo timu zimekuwa zikifungwa wakati mpira haukuwa umevuka wote kwenye mstari wa goli, au umedunda katikati ya mstari na kurudi uwanjani. Kwenye Ligi Kuu za kulipwa huko Ulaya kama Ligi Kuu England, Bundesliga imekuwa ikitumia mfumo wa GLT.
Tukio ambalo lilichagiza mchakato wa kuwa na teknolojia hiyo ya kwenye goli kwenye soka ni lile tukio la England kunyimwa bao baada ya mpira uliopigwa na kiungo Frank Lampard kwenye mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Ujerumani kuonekana kuvuka kabisa mstari wa goli, lakini mpira huo haukuzama kwenye nyavu ikaonekana si bao.
Fainali hizo za Kombe la Dunia 2010 zilifanyika Afrika Kusini na miaka miwili baadaye, teknolojia ya GLT ilianza kufanya kazi, ikiruhusiwa kutumika kwenye mechi. Na sasa maelezo ya kuhusu teknolojia hiyo ya GLT inapatikana ndani ya sheria kati ya zile 17 zinazoongoza mchezo wa soka (Laws of the Game).

Teknolojia hiyo ya GLT inazungumziwa ndani ya Law 1 (Sehemu ya kuchezea); kuruhusu vifaa kufungwa kwenye eneo la kuchezea mpira. Law 2 (Mpira); kuruhusu mpira iliyowekewa teknolojia inaruhusu mazingira ya GLT.
Law 5 (Mwamuzi); Kumtaka mwamuzi kufanya majaribio ya GLT kabla ya mechi na asitumie kama ina tatizo.
Pia kwenye Law 10 (Matokeo ya mchezo); Kuruhusu matumizi ya GLT kuthibitisha kama ni bao limefungwa au si bao kwamba mpira haukuvuka mstari.
Na sasa GLT inatumika kwenye ligi mbalimbali za Ulaya, katika michuano ya Uefa na ya Fifa. Septemba 2024, tovuti ya FIFA iliorodhesha viwanja 144 vilivyokuwa na leseni ya kufunga mitambo ya teknolojia ya GLT, ambapo viwanja 135 vinatumia mfumo wa Hawk-Eye na vingine tisa vinatumia View, ambao ni mfumo mwingine uliopewa leseni ya kufunga mitambo ya GLT kwenye viwanja vya soka.