Ghorofa mbili stendi ya Magufuli ziko tupu kwa miaka minne

Ikiwa imetimiza siku 1,087 tangu Stendi ya Magufuli kuanza kutumika, eneo la chini stendi hiyo lenye ghorofa mbili halijawahi kutumika, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Hata hivyo, kuna baadhi maeneo ya stendi hiyo yamepangishwa kwa ajili ya ofisi mbalimbali, zikiwamo za wasimamizi wa kituo, Polisi, Uhamiaji, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), sehemu ya kulala wageni na Kituo cha Afya cha Kairuki.

Stendi ya Magufuli yenye uwezo wa kuhudumia watu zaidi ya 200,000 kwa siku, ilianza kutumika Februari 24, 2021 ikiwa ni siku mbili tangu aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kuizindua.

Eneo hilo halijawahi kutumika baada ya ujenzi kusimama, hali inayolifanya kugeuka kichaka cha watu kujificha na kufanya shughuli nyingine tofauti na matarajio yaliyokuwapo awali.

Pia kutokana na ujenzi huo kulegalega baadhi ya watu wameanza kuiba vifaa mbalimbali ikiwemo nyanya za umeme huku wakijisaidia na kuacha nguo zilizochafuka katika eneo hilo.

Haya yanafanyika wakati ambao Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ingeweza kujipatia fedha nyingi kwa kupangisha eneo hilo kwa ajili ya biashara mbalimbali kama maduka makubwa ambayo yalitarajiwa kuwapo, lakini sasa hata miundombinu iliyokuwa imewekwa ikiwemo milango ya vioo imeanza kuvunjwa.

Stendi kwa sasa inahudumia mabasi ya zaidi 1,000 ya abiria na teksi 280 kwa siku, pia ina maeneo ya maegesho na vituo vya bodaboda, bajaji na mama na baba lishe na kulifanya eneo hilo kuwa fursa kubwa kibiashara.

Machi mwaka jana, aliyekuwa Meneja wa kituo hicho, Isihaka Waziri akizungumza kwenye mkutano na wadau wanaofanya kazi katika stendi hiyo, alisema ujenzi wa stendi umekamilika kwa asilimia 97, lakini ulikuwa umesimama baada ya mkandarasi kuondoka kwa kutolipwa kwa wakati.

Mkandarasi aliyekuwa amepewa kazi hiyo ni Kampuni ya Hainan International Limited ya China na kwenye bajeti ya mwaka 2024/25 Halmashauri ya Ubungo ilitenga Sh3.2 bilioni kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kuendeleza ujenzi.

Ujenzi wa stendi hiyo uligharimu Sh50.9 bilioni na maeneo ambayo ujenzi haujakamilika ni maegesho ya magari, ambayo ikikapokamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi karibu 3,500 huku mapato yaliyotabiriwa kwa mwaka yakiwa ni Sh10 bilioni.

Akizungumzia mapato yanayokusanywa kwa njia ya kielektroniki wakati huo, Waziri alisema yalikuwa yameongezeka kutoka Sh3 milioni hadi kufikia Sh5 milioni kwa siku.

Hali ilivyo

Mwananchi ilipata nafasi ya kuingia katika ghorofa hizo mbili ambazo hazijamalizika ujenzi na kushuhudia hali ilivyo katika eneo hilo.

Baadhi ya maeneo yalioneka kuwa na tope lililoganda ambalo kwa mwonekano liliingia ndani ya eneo hilo kupitia mvua kubwa iliyonyesha na kubeba maji matope.

Matope hayo hayana dalili ya kusafishwa huku baadhi ya watu wakiwa wamejisaidia na kutupa nguo ambazo walijisafishia, ikiwa ni ishara kuwa eneo hilo halina mtu aliyeingia kwa muda mrefu.

Mbali na hayo, kumefanyika wizi wa nyaya huku baadhi yake zikiwa zimechunwa gamba la juu ili kuondoka na shaba kirahisi na maganda kubaki kama uchafu.

Nyaya zinazoibwa ni zile ambazo zilipaswa kutumika kuingiza umeme ndani ya ghorofa hizo, kabla ya kufungwa kwa dali.

Kwa mujibu wa mlinzi ambaye hakutaka jina lake liandikwe, eneo hilo kutokukamilika hadi sasa limekuwa maficho la watoto wa mitaani na watu wanaofika kuiba vifaa.

 “Tumekuwa tukifanya msako wa kukamata watu wanaokaa huku na wakati mwingine wanakuja polisi kuangalia na kuwafukuza, lakini doria hii inapita mara moja hivyo mtu akikariri ratiba ni rahisi kufanya uhalifu,” alisema.

Alisema watu wanaoiba vifaa katika eneo hilo wanapitia madirishani, hawawezi kupita kwenye milango kutokana na ulinzi uliopo.

Mlinzi huyo amesema baadhi ya viongozi wanaotembelea eneo hilo hawapelekwi eneo la chini kwa kuwa halijakamilika na hivyo kuishia kwenye ghorofa za juu na maeneo mengine ya stendi.

Wasemavyo watumiaji

Mmoja wa abiria amelieleza mwananchi kuwa kuacha eneo hilo bila uendelezaji ni sawa na kutupa fedha ambazo zilikwishatumika awali.

“Unajua hili eneo ni kama wamekosa tu mpango mkakati wa kulifanya likamilike, kama fedha ndiyo tatizo wangeweza kumpa mtu mkataba akamalizia mwenyewe na kufanya biashara zake kwa makubaliano maalumu,” anasema Lawrence James mkazi wa Tandika.

Alisema kwa namna eneo lilivyo, kuweka maduka inaweza kuwa vigumu kwa baadhi ya watu kufika, lakini ikiwa zitaruhusiwa baa kufanya shughuli zake kunaweza kusisimua biashara za stendi kwa ujumla.

“Mtu mwenye ubunifu kabisa wa biashara kama yule wa Kitambaa Cheupe au Samaki Samaki akipewa hapa, utaniambia biashara itakayofanyika kwenye hii stendi, tatizo ni nani ambaye anatoa mawazo, hapo ndiyo shida inaanzia,” alisema.

Hata hivyo, kuwekwa baa kulipokelewa tofauti na Mariam Juma ambaye anasema huenda hilo likawa gumu kwa sababu kuna hospitali na nyumba ya kulala wageni.

“Labda wamwambie mmiliki afunge vifaa vya kuzuia kelele ili wagonjwa na wageni kwenye ile nyumba ya wageni wasipate usumbufu, vinginevyo inawezaa kuwa karaha licha ya kuwa biashara itasisimka,” alisema Mariam.

Wasemavyo viongozi

Alipotafutwa kuzungumzia hali ilivyo katika maeneo hayo, Meneja wa stendi ya Magufuli, Isaac Kasebo alitaka suala hilo aulizwe Mkurugenzi wa Manispaa ya  Ubungo, Aron Kagurumjuli.

Alipotafutwa Kagurumjuli, alisema ujenzi wa eneo hilo unatarajiwa kuendelea katika mwaka huu wa fedha baada ya kupitishwa kwa bajeti ya mwaka 2025/2026.

“Mpango wa kumalizia pale unaendelea na kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha zimetengwa, pindi itapotolewa mkandarasi ataingia kazini kumalizia kazi,” alisema Kagurumjuli.

Kuhusu matumizi yasiyofaa ya eneo hilo na namna wanavyodhibiti watu kuingia au wizi, Kagurumjuli alisema wamekuwa wakihakikisha kunakuwa na ulinzi kwa saa 24 ili kuzuia watu wasiingie katika eneo hilo ambalo bado halijaanza kutumika.

Mpango wa awali

Awali jengo hili lenye ghorofa saba mbali na kuhudumia mabasi yanayoingia na kutoka mikoa mbalimbali nchini, pia lilitarajiwa kuwa na hoteli, hosteli, bustani ya kupumzikia, maduka makubwa (mall) kwa mujibu wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sporah Liana.

Lakini hadi sasa stendi hiyo imefanikiwa kuwa na nyumba ya kulala wageni pekee huku bustani na hosteli vikibaki kuwa simulizi za kwenye vyombo vya habari, ambazo ziliwahi kutolewa na viongozi tofauti bila ya kutekelezwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *