UPEPO umebadilika! Ndio, kiungo Yusuf Kagoma amejipatia umaarufu baada ya wababe wa Kariakoo, Simba na Yanga kumnyatia na mmoja kati yao kuwa na kisu kikali na kuinasa saini yake akitokea Singida Fountain Gate.
Yanga ndiyo ilianza kufanya naye mazungumzo, lakini Simba ilimbeba kutokana na uhitaji zaidi na mchezaji huyo na ilimaliza dili mapema kuliko watani zao.
Licha ya Simba kuwahi kunasa saini ya kiungo huyo, Yanga hawakutaka kukubali na kusababisha mzozo uliotatuliwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mashabiki wa Simba hivi sasa wanachizika na kiwango bora cha kiungo huyo aliyesajiliwa akitokea Fountain Gate, ambaye amekuwa akicheza sambamba na Fabrice Ngoma iliyemsajili kabla ya kuanza kwa msimu huu akitokea Al Hilal ya Sudan.

Kagoma ni mtaalamu eneo la kiungo hasa kutokana na uwezo wake wa kupokonya mpira na kukaa nao mguuni kwa muda kabla ya kutoa pasi ndefu au fupi ambazo zimekuwa zikiwafikia walengwa kwa usahihi.
Hiyo ndiyo sifa mojawapo ya mchezaji anayecheza nafasi ya kiungo, ni lazima awe na uwezo wa kupiga pasi zinazofika. Kagoma amekuwa akicheza sambamba na Fabrice Ngoma na wametengeneza pacha nzuri inayoiweka Simba kwenye nafasi nzuri ya ulinzi, pia kupiga pasi sahihi.
Hicho kiwango chake ndicho kimemfanya awe tegemeo chini ya kocha Fadlu Davids, akiwabwaga mkongwe Mzamiru Yassin ambaye alikuwa akicheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza akisaidiana na Sadio Kanoute aliyeondoka baada ya kumaliza mkataba.
Mzamiru ambaye aliongeza mkataba wa miaka miwili kwa dau nono msimu huu hana uhakika wa namba kikosini, huku nafasi hiyo pia ikiwaweka nje nyota wengine wawili wa kigeni, Deborah Mavambo na Augustine Okajepha ambao wote wameingia mwanzoni mwa msimu huu.

Msimu uliopita, Kanoute ambaye ameondoka na Mzamiru walikuwa wamejihakikishia nafasi kikosi cha Simba, lakini uwepo wa Ngoma na Kagoma ambaye ameingia msimu huu umewang’oa.
Kagoma anayafanya hayo ukiwa ni msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi cha Simba huku akimuweka benchi Mzamiru ambaye amehudumu kwa muda marefu Simba akitwaa mataji mbalimbali na kuwa miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri kimataifa.
Umahiri wa Kagoma unaifanya Simba kumkaushia Mzamiru ambaye ni mkongwe baada ya mfalme wa muda mrefu kwenye eneo hilo ndani ya Simba, Jonas Mkude, kutimkia kwa watani zao, Yanga.
Uwepo wake pia ukawa unampa wakati mgumu Mzamiru, kwani alikuwa ni panga pangua katika kikosi cha kwanza na baada ya kuondoka alipata nafasi ya kucheza na sasa mambo ni yaleyale.
Hata hivyo, unaambiwa baada ya ujio wa Kagoma ambaye amefanikiwa kumshawishi Fadlu kumuamini na kumpa namba kikosi cha kwanza sambamba na Ngoma kwenye eneo hilo ambalo limekuwa limekuwa likivutia mastaa kibao kutoka mataifa tofauti.
Uimara wa Kagoma katika eneo la kiungo huenda umetatua changamoto iliyokuwa inawatesa viongozi wa Simba ambao kila dirisha walikuwa wanajaribu kufanya usajili, ukiachana na uwepo wa mastaa wengine wa kigeni ambao wanakaa benchi amepita nyota mwingine ambaye alishindwa kuonyesha.
Baada ya kuondoka Kanoute Simba ilimsajili Babacar Sarr ambaye hakuwa na maajabu hadi viongozi walipoamua kumalizana naye kwa kumvunjia mkataba na kusaka mbadala mwingine.
Kagoma na Ngoma wamefanikiwa kuituliza timu wakisaidiana na ukuta unaoongozwa na Abdulrazack Hamza na Che Malone, wakiwa na kipa kinara wa clean sheet, Moussa Camara wakiruhusu nyavu kutikishwa mara tano kwenye mechi 16 walizocheza Ligi Kuu Bara.
STAILI YA UCHEZAJI
Kasi, uwezo wa kukaba na usahihi wa uamuzi ni miongoni mwa vitu ambavyo inawezekana Fadlu ameviona kwa Kagoma kiasi cha kumuamini na kumpa nafasi ya kucheza akiwa tayari ametoa nafasi kwa wachezaji wote wa eneo hilo kuonyesha walicho nacho.
Fadlu amejipata, ni rahisi kusema hivyo, kwa mechi za hivi karibuni kutokana na kikosi chake kujirudia tofauti na mwanzo ambapo alikuwa anatoa nafasi kwa kila mchezaji na Kagoma kaingia kikosi cha kwanza.
Kocha huyo amemtambulisha kikosini Kagoma huku akimkata Deborah ambaye usajili wake ulizungumzwa sana na ubora wake aliouonyesha mechi alizopewa nafasi sambamba na Mzamiru kutokana na ubora wa mzawa huyo mwenye uzoefu wa Ligi Kuu Bara.
Kagoma ni mzuri mwenye kukaa na mpira mguuni wadau wakipenda kutumia neno la ‘anajua kuficha mpira’, pia ni mwepesi wa kupora mipira kwa wapinzani na kutoa pasi sahihi, licha ya makosa madogomadogo aliyo nayo yanayosababisha kuonyeshwa kadi.
Inawezekana mashabiki wakaona mengi kutoka kwa mchezaji huyo hasa katika utoaji pasi sahihi kwa kuwa mbali na kasi aliyonayo, uwezo wa kufanya uamuzi kwa haraka lakini pia ni mrefu, hivyo anaongeza namba ya wachezaji wenye vimo virefu kwenye safu ya ulinzi ya Simba ambayo imeongeza uimara.
MWENYEWE ATIA NENO
Kagoma ameliambia Mwanaspoti kuwa kupata namba mbele ya nyota wa kigeni na mkongwe ndani ya kikosi hicho kunatokana na upambanaji na kufuata maelekezo ya kocha.
“Kila mchezaji ni bora, lakini kila mmoja ana aina yake ya uchezaji. Nilipopata namba ya kucheza nilionyesha juhudi na kuamini kuwa nilichofanya leo kesho kinahitaji jitihada zaidi,” anasema mchezaji huyo.
“Napambana na wengi kwenye nafasi ninayocheza, sitakiwi kujisahau au kubweteka. Ili niwe bora nimekuwa mchezaji wa kujifunza kila siku na kuongeza jitihada siku hadi siku.”