Gazeti la The Guardian linalochapishwa nchini Uingereza limetangaza kuwa litaacha kuweka maandiko yake kwenye X, mtandao wa kijamii uliokuwa ukijulikana kama Twitter.
Katika taarifa yake, gazeti hilo maarufu limeashiria wasiwasi liliopata kutokana na kuongezeka hisia hasi na misimamo ya kufurutu mpaka ndani ya jukwaa hilo, ambayo limesema yamefunika manufaa ambayo hapo awali ulikuwa nayo mtandao huo kama chombo cha ushiriki wa uandishi wa habari na ujumuishaji wa wasomaji.
Uamuzi huo wa Guardian umetangazwa huku kukiwapo na uchukuaji hatua kali za kuwafuatilia watumiaji wa X, ambao ulishuhudiwa zaidi wakati wa uchaguzi wa rais wa Marekani.
Gazeti hilo mashuhuri nchini Uingereza limetaja kuongezeka kwa maudhui hatarishi zinazozungumziwa kwenye mtandao wa X, ikiwa ni pamoja na mielekeo ya ‘nadharia za njama’ za mrengo mkali wa kulia na matukio ya ubaguzi wa rangi, kama sababu zilizolifanya liamue kujitoa kwenye mtandao huo wa kijamii.

Elon Musk, ambaye alianza kuwa mmiliki wa X mwaka 2022, tangu wakati huo amekuwa akiyaangalia kijuujuu tu mabadiliko ambayo gazeti la The Guardian linaamini yanachangia kueneza mazingira ya sumu na hatarishi kwa vyombo vya habari, yenye ushawishi mkubwa kwenye mahubiri ya kisiasa.
Gazeti la Guardian limesisitiza kuwa halitatumia tena akaunti yake yoyote rasmi ya uhariri kwenye X lakini watumiaji kwenye jukwaa hilo wataweza kuendelea kusambaza makala zake…/