Kulingana na duru za hospitali ya Al-Quds, watu hao wameuawa baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa Israel karibu na kituo cha usambazaji wa misaada cha GHF katika Ukanda wa Gaza.
Shirika la habari la Palestina, WAFA, limeripoti kuwa zaidi ya watu 100 walijeruhiwa. Kwa jumla, Wapalestina 23 waliuawa kwenye mashambulizi tofauti ya Israel katika Ukanda wa Gaza alfajiri ya Jumanne, limesema shirika hilo la habari.
Soma pia: Kiongozi wa upinzani Israel asema serikali ya sasa haiwakilishi watu
Wakati huo huo, waombolezaji walikusanyika hii leo kuwazika wapendwa wao 19 katika eneo la Khan Younis, waliouawa kwenye mashambulizi ya anga ya Israel yaliyolenga mahema yaliyowahifadhi wakimbizi wa ndani.
Hospitali ya Nasser imesema majeruhi wengine kadhaa wamepokelewa kwenye hospitali hiyo.
Hata hivyo Israel, imesema haikubaliani na maelezo hayo bali inachofahamu ni kwamba wanajeshi wake walifyatua tu risasi za tahadhari hewani.
Kwa upande mwengine, mpaka sasa hakuna mafanikio yaliyopatikana katika mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas, lakini kulingana na maafisa waIsrael na Marekani, juhudi zinaendelea za kulishawishi kundi la Hamas kulegeza msimamo wake juu ya pendekezo linaloungwa mkono na Marekani kuhusu kufikia makubaliano ya kusimamisha mapigano huko Gaza.
Wakati huo huo, Ufaransa imesema imepokea ahadi mpya kutoka kwa Kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas, kuhusu mageuzi kabla ya mkutano wa wiki ijayo ambao serikali ya Ufaransa inaweza kuwa mstari wa mbele katika nchi za Magharibi zenye nguvu, kutangaza kuwa inaunga mkono hatua za kutambuliwa taifa huru la Palestina.
Soma pia: Rais Mahmoud Abbas awataka Hamas waweke silaha Chini
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema Abbas kwenye barua hiyo amelaani mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023 kwenye ardhi ya Israel, ametoa wito wa kuachiliwa mateka wote na ameahidi mageuzi zaidi.
Rais Macron, kwa kushirikiana na Saudi Arabia,wanaandaa mkutano wa kimataifa utakaoongozwa na Umoja wa Mataifa wa kujadili juu ya kutambuliwa taifa huru la Palestina utakaofanyika mjini Paris.
Israel imesema haitakubali Mamlaka ya Palestina iwe na jukumu lolote katika Ukanda wa Gaza baada ya vita na imezilaumu nchi zinazozingatia kuutambua uhuru wa Palestina, ikisema kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kuyapongeza mashambulizi ya kundi la Hamas.
Hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar, amesema amekasirishwa na uamuzi wa Uingereza wa kuwawekea vikwazo mawaziri wawili wa Israel. Amesema serikali ya Israel itafanya mkutano maalum wiki ijayo kuamua jinsi ya kuijibu Uingereza kwa uamuzi wake huo aliouita “usiokubalika.”
Soma pia: Waziri wa Ulinzi Israel aamuru jeshi kuendeleza vita Gaza
Uingereza na washirika wengine wa kimataifa rasmi, watawawekea vikwazo mawaziri wawili wa Israel, Itamar Ben-Gvir na Bezalel Smotrich, wenye siasa kali za mrengo wa kulia, kutokana na mwenendo wao katika vita vya Gaza.
Vyanzo: RTRE/DPA