Gaza: Takriban watu 220 wameuawa kulingana na jeshi la Ulinzi wa Raia

Jeshi la Ulinzi wa Raia katika Ukanda wa Gaza limetangaza siku ya Jumanne, Machi 18, idadi mpya ya vifo vya watu wasiopungua 220 katika mashambulizi ya usiku ya Israeli,  kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa makubaliano usitishwaji mapigano Januari 19, 2025.

Imechapishwa:

Dakika 2

Na: RFI na mashirika mengine

Matangazo ya kibiashara

Muda wa usitishwaji mapigano katika Ukanda wa Gaza ulimalizika saa 8:20 usiku kwa saa za Gaza mnamo Machi 18, anaandika mwandishi wetu huko Jerusalem, Michel Paul. Wakati jeshi la Israeli halikutoa maelezo yoyote kuhusu mashambulizi hayo ya anga, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu imesema kuwa imewaamuru wanajeshi wa Israeli kuchukua “hatua kali” dhidi ya Hamas. Mashambulizi haya ya Israel katika Ukanda wa Gaza yanakuja “kufuatia Hamas kukataa mara kwa mara kuwaachilia mateka wetu, pamoja na kukataa kwake mapendekezo yote iliyopokea kutoka kwa mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na wapatanishi,” ofisi ya Benjamin Netanyahu imesema. “Israel sasa itachukua hatua dhidi ya Hamas kwa kuongeza nguvu za kijeshi,” imeongeza katika taarifa. Mashambulizi ambayo yatadumu “kwa muda mrefu iwezekanavyo,” ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli imebainisha.

Msemaji wa Ikulu ya White House amesema muda mfupi baadaye kwenye kituo cha Fox News kwamba utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump ulishauriwa na Israel siku ya Jumatatu kuhusu mashambulizi hayo.

Mwisho wa kusitisha mapigano?

Mwakilishi mkuu wa Hamas ameishutumu Israeli kwa “upande mmoja” kusitisha makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa Januari 19 na awamu ya kwanza ambayo ilimalizika Machi 2. Wapatanishi wa Kiarabu wameshindwa kuendeleza mazungumzo kati ya taifa la Kiyahudi na kundi la Palestina tangu kumalizika kwa awamu hii ya kwanza. Awamu ya pili ya makubaliano hayo ilikuwa kuruhusu kuachiliwa kwa mateka wa mwisho wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza na kupelekea kusitishwa kwa kudumu kwa uhasama.

Siku ya Jumanne asubuhi Hamas imeishutumu Israel kwa kuanza tena “uchokozi” wake dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza na kuhatarisha mateka wa Israeli ambao bado wanazuiliwa katika eneo hilo.

Mashambulizi mengi

Kulingana na Jeshi la Ulinzi wa Raia, watu wasiopungua 220, wakiwemo watoto, waliuawa katika mashambulizi haya ya Israel. Zaidi ya watu 150 pia wamejeruhiwa, huku zaidi ya mashambulizi 30 yakiripotiwa usiku kucha. Zaidi ya vifo 103 vimerekodiwa huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, na vingine kati ya Nuseirat (katikati), Jiji la Gaza, na kaskazini mwa eneo hilo.

Nyumba tatu zililengwa huko Deir el-Balah, katikati mwa Ukanda wa Gaza, mashahidi na madaktari wameripoti. Jengo pia lilmeshambuliwa kwa bomu katika mji wa Gaza, huku mashambulizi yakifanywa dhidi ya walengwa huko Khan Younis na Rafah, kusini mwa eneo la Palestina. Katika hatua hii, ni jeshi la anga la Israeli ambalo linashambulia, lakini vyanzo vya kijeshi vinaonyesha kuwa operesheni hiyo inaweza kupanuka haraka sana. Kwa siku kadhaa, Israel imekuwa ikidai kuwa Hamas ilikuwa ikichukua fursa ya mapatano hayo kujenga upya vikosi vyake katika eneo la Palestina.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *