
Washington imethibitisha siku ya Jumatano kwamba inafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Hamas kuhusu mateka walioko Gaza, kwa kushauriana na Israeli. Mazungumzo hayo ambayo hayajawahi kushuhudiwa yanavunja sera ya muda mrefu kwamba Marekani haifanyi mazungumzo ya moja kwa moja na makundi ambayo inayaona kuwa ya kigaidi.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Hii ni mara ya kwanza. Marekani imethibitisha Jumatano, Machi 5, kwamba inafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Hamas, kwa kushauriana na Israeli.
Mashauriano hayo yanaachana na sera ya muda mrefu kwamba Marekani haifanyi mazungumzo ya moja kwa moja na makundi ambayo inayachukulia kuwa ni ya kigaidi, jambo ambalo limekuwa likifanyika kwa Hamas tangu mwaka 1997. Pia yanakuja wakati muafaka katika Ukanda wa Gaza unaonekana kuwa hatarini.
Alipoulizwa kuhusu majadiliano haya, yaliyofichuliwa kwa mara ya kwanza na tovuti ya Axios, msemaji wa Ikulu ya Marekani Karoline Leavitt amejibu kwamba mjumbe maalum wa Marekani kwa ajili ya mateka, Adam Boehler, “allihusika katika mazungumzo haya, (na) ana mamlaka ya kuzungumza na mtu yeyote.”
Msemaji huyo alikataa kutoa maelezo ya majadiliano hayo, akisema “Maisha ya Marekani yako hatarini,” lakini akasema Israeli “imeshauriwa,” madai ambayo baadaye yamethibitishwa na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu katika taarifa fupi.
Kwa upande wao, maafisa wa Hamas wamefichua kwa shirika la habari la AFP kwamba “mazungumzo kadhaa yamefanyika kati ya Hamas na viongozi mbalimbali wa Marekani, mazungumzo ya mwisho yaliongozwa na mjumbe wa Marekani, na suala la wafungwa wa Israeli wenye uraia wa Marekani wanaoshikilia, wakiwa hai au wamefariki, liliibuliwa.”
Afisa mwingine mkuu wa Hamas akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, amezungumzia “mikutano miwili ya moja kwa moja kati ya Hamas na maafisa wa Marekani katika siku za hivi karibuni huko Doha.”
Kuna mateka watano wa Kimarekani bado wanazuiliwa huko Gaza, wanne kati yao wamethibitishwa kufariki na mmoja anayeaminika kuwa hai, kulingana na hesabu ya shirika la habari la AFP.
Onyo kutoka kwa Rais wa Marekani
Siku hiyo hiyo kama ufichuzi huu, Donald Trump ametoa “onyo la mwisho” kwa Hamas kuwaachilia mateka, vinginevyo “watu wa Gaza” wana hatari ya “kifo”.
“Kwa watu wa Gaza: muna mustakabali mzuri, lakini sio ikiwa munashikilia mateka. Mkifanya hivyo,mumefariki! Fanyeni uamuzi SAHIHI,” rais wa Marekani ametishia katika ujumbe kwenye mtandao wake wa Truth Social.
Pia almesema kuwa alikuwa akituma “Israel kila inachohitaji kumaliza kazi” huko Gaza, akisisitiza kwamba “hakuna mwanachama wa Hamas ambaye atakuwa salama ikiwa hamtafanya kile ninachosema”, wakati ambapo makubaliano ya amani katika Ukanda wa Gaza yanaonekana kutishiwa.
“Wakati wa kuondoka Gaza ni sasa, wakati bado munaweza,” ameongeza, akiwaambia viongozi wa kundi la wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas.