Gaza: Makubaliano ya kubadilishana wafungwa wa Kipalestina kwa miili ya mateka wanne

Wapatanishi katika mzozo kati ya Israeli na Hamas wamefikia makubaliano, chini ya kivuli cha Misri, kwa ajili ya kuachiliwa kwa Wapalestina 602 ambao walikuwa waachiliwe siku ya Jumamosi ili kubadilishana na mateka wanne wa Israeli, chombo cha habari chenye uhusiano na serikali ya Misri cha Al-Qahera kimesema siku ya Jumanne. Shirika la Kiislamu la Palestina limethibitisha makubaliano haya kwenye Telegram, na kubainisha kuwa ni sehemu ya awamu ya kwanza ya usitishaji vita na Israeli.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Kati ya mateka 251 waliotekwa nyara Oktoba 7, 62 wamesalia Gaza, 35 kati yao walifariki, kulingana na jeshi la Israeli. Kwa mujibu wa Hamas, ni mateka wanne tu waliofariki ambao bado hawajarudishwa Israeli wakati wa awamu ya kwanza ya makubaliano hayo.

Siku ya Jumamosi, Hamas iliwaachilia huru Waisraeli sita katika kile ambacho kingekuwa ni mara ya saba ya kubadilishana mateka kwa wafungwa wa Kipalestina. Lakini kwa mara nyingine tena iliandaa zoezi hili la kuachiliwa kwa mateka wa Israeli, ikiwaonyesha mateka watano kwenye jukwaa wakitazamana na umati wa watu, mbele ya mabango makubwa ya kuwaenzi wapiganaji wa Hamas waliouawa, kabla ya kuwakabidhi kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.

Kisha Israel ilifuta mpango wa kuachiliwa huru Wapalestina 620, ikitaka kusitishwa kwa “sherehe za kudhalilisha”. Tawi lenye silaha la Hamas kisha likatoa video siku ya Jumamosi jioni, ambayo inaonekana ilirekodiwa mchana huko Nousseirat, katikati mwa Ukanda wa Gaza, ikionyesha mateka wawili wakitazama zoezi hili la kuachiliwa kwa mateka wa Israeli na kumwomba Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu kuchukua hatua kwa ajili yao.

Jukwaa la Familia za mateka lilieshutumu “maonyesho ya ukatili haswa yanayochukiza”. ICRC ilizitaka pande zote kufanya mazungumzo ya wafungwa na mateka “kwa njia ya heshima na ya faragha”. Katika kujibu kusitishwa kwa kuachiliwa kwa wafungwa, Hamas iliishutumu Israeli kwa “kuweka makubaliano yote ya usitishaji katika hatari kubwa” na kutoa wito kwa nchi zinazopatanisha kuingilia kati.

Mwisho wa awamu ya kwanza mnamo Machi 1

Mjumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump katika Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, anatarajiwa katika eneo hilo wiki hii kujaribu kuongeza muda wa awamu ya kwanza ya usitishaji vita ulioanza kutekelezwa Januari 19 huko Gaza baada ya miezi 15 ya vita. Awamu hii ya kwanza itamalizika Jumamosi Machi 1. Lakini mazungumzo yaliyopangwa juu ya kuendelea kwa mchakato huo, ambayo yalipaswa kuanza mapema Februari, bado hayajaanza.

Awamu ya pili inatakiwa kumaliza vita hivyo mara moja na kwa wote, jambo ambalo mrengo wa kulia unaoshirikiana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu unapinga, na kutishia kuvunjwa kwa serikali yake. Hamas, kwa upande wake, ilisema iko tayari kuwaachilia “kwa wakati mmoja” mateka wote waliosalia katika awamu hii ya pili.

Awamu ya tatu na ya mwisho ya makubaliano hayo itakuwa kwa minajili ya ajili ya ujenzi mpya wa Ukanda wa Gaza.