
Wapiganaji wenye silaha wa Hamas wamewaachilia mateka watatu wa Israeli katika Ukanda wa Gaza leo Jumamosi, Februari 15. Mabasi ya wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru na Israel pia yameondoka katika gereza la Negev. Haya ni mabadilishano ya sita kwa wafungwa wa Kipalestina tangu kuanza kwa usitishaji vita, ambao wiki hii uliponea kuvunjika.
Imechapishwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Baada ya kuzuiliwa kwa takriban siku 500, Sacha Trupanov, Muisraeli mwenye asili ya Urusi mwenye umri wa miaka 29, Yair Horn Muisraeli mwenye asili ya Argentina mwenye umri wa miaka 46 na Sagui Dekel-Chen, Muisrael mwenye asili ya Marekani mwenye umri wa miaka 36, walionyeshwa jukwaani huko Khan Younis, wakiwa wamezingirwa na kundi la wapiganaji wa Kiislam wenye silaha waliojifunika nyuso zao wa Hamas na wale wa kundi la Islamic Jihad, kundi mshirika la wapiganaji wa Kipalestina
Wanaume watatu walioachiliwa Jumamosi hii, wakionekana kuwa na hali nzuri kiafya, walilazimishwa kusema maneno machache kwenye kipaza sauti mbele ya umati. Kisha walikabidhiwa kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ambayo iliwakabidhi kwa jeshi la Israeli. Mateka hao watatu “walivuka mpaka na kuingia katika eneo la Israeli” na wako njiani kuelekea mahali ambapo wataunganishwa na familia zao, taarifa fupi ya jeshi la Israel imesema.
Mapema Ijumaa jioni, katika video kutoka Islamic Jihad, mmoja wa mateka hao Muisraeli mwenye asili ya Urusi Sacha Trupanov anliweza kuonekana kwenye ufuo wa Gaza akiwa na fimbo ya kuvua samaki, anaripoti mwandishi wetu huko Jerusalem Sami Boukhelifa. Alionekana akitabasamu kwenye handaki alilokuwa ameshikiliwa. Picha hizi za propaganda ni ujumbe kwa Waisraeli kusema: “Mateka wenu wako sawa.” Kwa sababu afya ya mateka wengine watatu wa Kiisraeli walioachiliwa wiki iliyopita ilizua wimbi la hasira nchini Israeli. Walionekana dhaifu sana na wamedhoofika. Hamas kisha wakawalazimu kusalimia umati wa watu wa Gaza. Tukio ambalo lilichochea hasira nchini Israeli.
Kama ilivyo kwa kila zoezi la kuachiliwa kwa mateka, mamia ya wapiganaji wa Hamas waliojifunika nyuso na kujiham kwa slaha walizingira jukwaa huko Khan Younis kusini mwa ardhi ya Palestina iliyoharibiwa na miezi kumi na tano ya vita. Kila ukombozi huko Gaza unafanywa kwa uangalifu na Hamas na Islamic Jihad, kuwasilisha ujumbe tofauti.
Siku ya Jumamosi, kwa kujibu mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump ambao unapendekeza kuwaondoa kwa nguvu Wagaza, Hamas imejibu kwa kuonyesha bango kubwa lililochora Jerusalem na nyuma yake Misikiti, eneo la tatu takatifu la Uislamu na kutoa ujumbe: “Ikiwa tutahamishwa kwa nguvu, itakuwa tu kurudi Jerusalem.” Hamas pia walionyesha kioo cha saa karibu na picha za mateka, na maneno “Muda unakwenda” yameandikwa juu yake. Wapiganaji wa Hamas na Islamic Jihad wamesimama mbele ya umati wa watazamaji huku nyimbo za taifa zikirushwa kwenye vipaza sauti.
Wanaume hao watatu walitekwa nyara kutoka Kibbutz Nir Oz wakati wa shambulio la kiwango kikubwa na ghasia zilizotekelezwa Oktoba 7, 2023 na vuguvugu la Kiislamu la Hamas kusini mwa Israeli kutoka Ukanda jirani wa Gaza, ambalo lilianzisha vita katika eneo la Palestina. Kuachiliwa kwao kunakuja huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mario Rubio akitarajiwa nchini Israeli Jumamosi jioni. Kati ya watu 251 waliochukuliwa mateka, 73 bado wako Gaza, ikiwa ni pamoja na angalau 35 waliouawa, kulingana na jeshi la Israel.
Wafungwa wa Kipalestina pia wameachiliwa
Israeli kwa upande wake lazima iwaachilie wafungwa 369 wa Kipalestina. Thelathini na sita walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha. Lakini waliosalia 333 ni wakaazi wa Ukanda wa Gaza, waliokamatwa baada ya Oktoba 7 na wasiohusiana na shambulio la Hamas.
Mapema asubuhi, zaidi ya mabasi kumi yaliyokuwa yamewabeba wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru na Israeli yaliondoka katika gereza la Ktziot kusini mwa Israeli siku ya Jumamosi. Wengi wao wamepelekwa Ukanda wa Gaza kutoka kwenye gereza la Ktziot. Basi lingine lililowabeba wafungwa wa Kipalestina limeondoka katika jela ya kijeshi ya Israel ya Ofer katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu kuelekea Ramallah, kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa AFP kwenye eneo la tukio. Basi hilo limefika Jumamosi likishangiliwa na umati wa watu huko Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa, mwandishi wa habari wa AFP amebainisha. Wafungwa walioachiliwa huru wamepandishwa kwenye mabega ya umati na kukumbatiwa na ndugu zao kabla ya kuelekea kuchunguzwa afya zao haraka. Wanne kati yao walilazwa hospitalini, Shirika la Hilali Nyekundu limesema. “Timu zetu kwa sasa zinawahamisha wafungwa wanne walioachiliwa kutoka sehemu ya mapokezi kwenda hospitali,” Shirika la Hilali Nyekundu limesema katika taarifa.