Gaza: Afrika Kusini yaishutumu Israeli kwa ‘kutumia njaa kama silaha ya vita’

Israeli “inatumia njaa kama silaha ya vita” huko Gaza kwa kuzuia misaada ya kibinadamu kwa eneo la Palestina tangu siku ya Jumapili, Afrika Kusini imeshutumu katika taarifa kutoka Wizara yake ya Mambo ya Nje siku ya Jumatano Machi 5.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

“Kwa kuzuia kuingia kwa chakula Gaza, Israeli inaendelea kutumia njaa kama silaha ya vita,” inashutumu Pretoria, ambayo iliasilisha malalamiko ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israeli mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Afrika Kusini “inalaani vikali kukataa kwa Israeli kuruhusu misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza” kwani watu milioni 2.4 waliozingirwa “wanahitaji chakula, malazi na vifaa vya matibabu haraka,” Pretoria imeonya.

Kutokana na mkwamo katika mazungumzo ya kuendelea kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israeli, serikali ya Benjamin Netanyahu imekuwa ikizuia misaada ya kibinadamu kuingia kwa wakazi tangu siku ya Jumapili.

Kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi ya Israeli katika mji wa Jenin katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, Afrika Kusini “pia inalaani” hizi “operesheni za kijeshi zinazoendelea za Israeli” ambazo “zinawakilisha ongezeko la hatari”.

Mnamo Januari 21, jeshi la Israeli lilianzisha operesheni inayolenga makundi ya wapiganaji wa Kipalestina kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, eneo linalokaliwa na Israeli tangu mwaka 1967.

Afrika Kusini inalaani kitendo cha Israeli “kuendelea kukiuka mamlaka na utimilifu wa ardhi ya Syria“, ambapo mashambulizi ya anga ya Israeli dhidi ya maeneo ya kijeshi kusini mwa Syria yameongezeka katika siku za hivi karibuni.

Baada ya kuanguka kwa Rais Bashar Al Assad mwezi Desemba, Israeli pia ilituma wanajeshi katika eneo lisilo na jeshi la Miinuko ya Golan kusini magharibi mwa Syria, kwenye ukingo wa sehemu ya tambarare inayokaliwa na Israeli tangu vita vya mwaka 1967 na kushikiliwa mwaka 1981. Unyakuzi huu hautambuliwi na Umoja wa Mataifa.