Gamondi, Fadlu wanavyoleta mifumo mipya Bongo

Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa soka, mbinu za uchezaji zinaendelea kubadilika na kujiimarisha. Makocha wa Yanga na Simba, Miguel Gamondi na Fadlu Davids, wamefanikiwa kuingia katika anga za mbinu zinazotumiwa na kocha maarufu na wakubwa duniani kama Pep Guardiola wa Manchester City.

Wamejikita katika kutumia mianya iliyopo kati ya mabeki na kati wa pembeni, maarufu kama “half-spaces.” Huu ni mfano wa jinsi makocha wanavyoweza kuendeleza mbinu za kisasa ambazo zinaweza kuleta matokeo mazuri uwanjani.

Lakini pamoja na hivyo, wamehama kutoka kwa makipa wanaoruka kama nyani na sasa kipa bora kwenye timu zao ni yule mwenye uwezo wa juu wa kuutumia mguu wake badala ya mikono.

Tazama uwezo wa makipa wanaosajiliwa kwenye timu hiyo kwa sasa na utazame hali ilivyokuwa miaka kadhaa nyuma utaelewa mabadiliko hayo yanayozungumziwa hapa.

SOKA LA KISASA

Katika soka la kisasa, kuna umuhimu mkubwa wa mchezaji kuweza kubadilika kulingana na mahitaji ya timu Gamondi na Fadlu wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na wachezaji wao ili kuhakikisha wanaunda mifumo inayoweza kuhimili changamoto za wapinzani lakini hapa mchezaji mwenye faida kubwa zaidi kwao ni yule ambaye anaweza kucheza nafasi nyingi uwanjani.

Katika mbinu zao, makipa sasa wana jukumu kubwa la kuanzisha mashambulizi, jambo ambalo limewasaidia wachezaji kama Djigui Diarra wa Yanga na Ayoub Lakred na sasa Moussa Camara wa Simba kuonyesha uwezo wao katika matumizi ya miguu “Footwork.”

Wakati huohuo, makipa kama Ley Matampi wa Coastal Union na Mohamed Mustafa wa Azam nao wakijitahidi katika kuanzisha mashambulizi na kudaka. Hii inaonyesha jinsi makipa wanavyoweza kuwa sehemu ya mashambulizi, sio tu kulinda lango. Mbinu hii inahitaji makipa kuwa na ujuzi wa kudaka, lakini pia uwezo wa kutoa pasi za haraka na sahihi ili kuanzisha mashambulizi ya haraka kwa wapinzani wao, kipa kusogea karibu na mstari wa kati ni jambo lingine ambalo linafanya kazi kubwa kwenye mfumo huu wa half Space.

Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akiwapa maelekezo baadhi ya mastaa wake. Picha na Mtandao

Mabeki wa pembeni pia wana jukumu muhimu katika mbinu hizi za kisasa. Wakati ambapo zamani walikuwa wakitumikia kama walinzi pekee, sasa wanakuwa mawinga wakishambulia, lakini wanaingia kwenye mstari mmoja katikati ya mabeki wa kati na viungo. Mfano mzuri ni Chadrack Boka wa Yanga, ambaye ameonyesha uwezo wa kupambana katika eneo la mashambulizi zaidi, kana wakati unaweza kumtazama na kufikiri kuwa ni winga, na kuna wakati unaweza kumuona Maxi Nzegeli kama beki wa kati au pembeni kutokana na mifumo hii ya kisasa.

Hata hivyo, mabeki wa pembeni kama Pascal Msindo wa Azam ni kati ya wale ambao wameonekana kubadilika haraka zaidi kwenye mifumo hii ya kisasa.

MABADILIKO KATIKA MAJUKUMU

Wachezaji wa pembeni, ambao mara nyingi walikuwa wakicheza katika maeneo ya namba 7 na 11, sasa wanatumika kwa ufanisi zaidi katika half-spaces. Hii ni tofauti na zamani ambapo walikuwa wakifanya kazi katika maeneo ya pembeni pekee. Sasa, wanajumuishwa katika mashambulizi ya kati, wakifanya kazi kwa karibu na viungo ili kuongeza nguvu na ubora wa mashambulizi lakini wakiwa wanatakiwa kupiga pasi nyingi kwenye eneo dogo. Hii inahitaji wachezaji kuwa na uelewa mzuri wa mbinu za timu na jinsi ya kujiweka katika nafasi zinazofaa.

Katika mfumo wa kisasa, ushirikiano ni muhimu. Makocha kama Rachid Taoussi wa Azam FC na Patrick Aussems wanaelewa umuhimu wa kuwapa wachezaji wao nafasi ya kujifunza na kuboresha ujuzi wao. Kwa mfano, Gamondi anasisitiza kuwa wachezaji wanahitaji kuelewa nafasi zao na jinsi ya kuwasiliana ili kufanikiwa. “Kila mchezaji lazima aelewe jukumu lake katika mfumo, kwani ni muhimu kwa matokeo mazuri,” alisema Gamondi.

Fadlu Davids, kwa upande wake, anaamini kwamba mbinu zinawapa wachezaji wake fursa zaidi ya kuingia katika nafasi za hatari. “Half Space zinatoa nafasi za kuhamasisha mashambulizi, lakini pia zinahitaji ujuzi mkubwa na mchezaji kuelewa,” alisisitiza Davids. “Tunahitaji wachezaji wenye ujuzi wa kudhibiti mpira na kutoa pasi sahihi katika maeneo haya huu ni mfumo mgumu lakini unakuwa rahisi sana pale wachezaji wanapoelewa.” Hii inaonyesha jinsi makocha wanavyoweza kuendeleza uwezo wa wachezaji wao kwa kutumia mbinu za kisasa.

MAANA YA “HALF-SPACES”

Half-spaces ni maeneo maalumu katika uwanja wa soka yanayopatikana kati ya mistari ya pembeni na mistari ya katikati. Katika kila mchezo, maeneo haya yanaweza kutumiwa kwa ufanisi kuleta matokeo mazuri. Nusu nafasi hizi zinaweza kupatikana kwa urahisi, na zinatoa nafasi nzuri kwa mashambulizi. Wachezaji wanapoingia katika half-spaces, wanakuwa na nafasi ya kutengeneza mashambulizi kwa urahisi zaidi, huku wakitafuta nafasi za kufunga.

Asili ya neno “half-spaces” inachukuliwa kutoka kwa neno la Kijerumani “halbraum.” Katika Kiingereza, half-spaces pia zinaweza kuitwa “inside channels.” Neno hili linajieleza kwa urahisi, na ni muhimu kwa makocha kuelewa jinsi ya kuhamasisha na kuzuia wachezaji wao katika maeneo haya.

Lakini ni mfumo ambao makipa wanatakiwa kuwa na uwezo mkubwa zaidi mguuni kwa kuwa mara kwa mara mashambulizi huanza kupangiwa kwao na wengine wanaweza kugusa mpira mara nyingi zaidi kuliko hata mchezaji anayecheza ndani kwa kuwa suluhisho la mabeki wanapobanwa ni kurudi kwa kipa kuliko kupiga mpira mbele bila malengo.

Half-spaces hutoa njia rahisi zaidi ya kufikia lango la mpizani, kwani mpira unaweza kuhamishwa katika mwelekeo wowote. Hii inawapa wachezaji nafasi nzuri zaidi ya kupokea mpira na kujiandaa kwa shambulizi. Katika mashambulizi ya haraka, Half-spaces zinahakikisha kuwa wachezaji wanaweza kuhamasisha mashambulizi bila kuwa na vikwazo vingi. Hii ni njia bora ya kuleta mabadiliko katika mashambulizi, hasa katika mchezo wa soka wa kisasa.

CHANGAMOTO

Kuwa na ujuzi wa juu ni muhimu ili wachezaji waweze kudhibiti mpira na kutoa pasi sahihi katika half-spaces. Wachezaji wanahitaji kuwa na ufahamu mzuri wa jinsi ya kusimama katika nafasi sahihi ili kufanikisha malengo ya timu lakini lazima wawe na kasi ya hali ya juu kwa kuwa wanakuwa wengi kwenye eneo dogo. Pia, ni vigumu kufunga moja kwa moja kutoka kwenye Half-spaces, kwani wachezaji wanahitaji hatua nyingine kabla ya kufanya shambulizi. Hii inahitaji ujuzi wa juu na mawasiliano mazuri kati ya wachezaji.

Katika kujilinda, timu zinaweza kutumia mfumo wa mabeki watano ili kuzuia half-spaces. Hii inasaidia kuzuia wapinzani kuingia katika half-spaces kwa kukokota mpira au pasi. Ushirikiano kati ya wachezaji ni muhimu sana ili kuzuia wapinzani wasifike kwenye half-spaces kwa urahisi. Kwa kutumia mifumo ya ulinzi yenye nguvu, timu zinaweza kudhibiti maeneo haya na kuzuia mashambulizi hatari.

Kujilinda vizuri kunahitaji mawasiliano kati ya mabeki na viungo, ili kuhakikisha kila mchezaji anajua nafasi yake na jukumu lake. Hii inahitaji mafunzo ya kina na kuelewa mifumo ya mchezo. Makocha wanahitaji kuhakikisha wachezaji wao wana uelewa mzuri wa mbinu za kujilinda na kushambulia ili kuweza kuhimili changamoto kutoka kwa wapinzani mfano ni jinsi Arsenal walivyoweka ulinzi kipindi cha pili kwenye mchezo dhidi ya Man City katika mchezo wa Ligi Kuu England.