Gamondi autaka ubingwa wa Afrika

Dar es Salaam. Baada ya msimu uliopita wa mashindano 2023/24 kumalizika, Yanga ikiwa na mataji mawili ya ndani, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) huku katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikitikisa vigogo mbalimbali, kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema anataka ubingwa wa Afrika.

Baada ya msimu uliopita kumalizika Yanga ilikuwa na kazi mbili kubwa, moja ilikuwa ni kubakisha wachezaji wao muhimu ambao mikataba yao ilifikia ukomo akiwemo Stephane Aziz KI, baada ya hapo walikuwa na kazi nyingine nzito ya kukiimarisha kikosi hicho kinachoshikilia rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara nyingi (30).

Baada ya sarakasi zote hizo, mabosi walitakiwa kuhakikisha mtaalamu wao wa ufundi kwa maana ya kocha Miguel Gamondi anasalia, kwani ndiye aliyekuwa nyuma ya mafanikio yote hayo.

Huu ni msimu mwingine ambao Gamondi ana mtihani wa kuendeleza kile alichofanya ule uliopita akiwa na kikosi bora zaidi chenye uwiano mzuri wa wachezaji karibu kila eneo na hapa anakiri hilo katika mahojiano maalumu ambayo aliyofanya na Mwananchi.

Ugumu wa kuendeleza mafanikio

Gamondi anaelewa wazi kuwa, kazi kubwa sio kufanikiwa tu bali kudumisha mafanikio hayo. “Sijawahi kuahidi chochote, ni kujituma, kujitolea na kutoa asilimia 100.

“Jambo gumu zaidi ni kuwa na mwendelezo kwenye kitu chochote ambacho umeanza kukifanya, msimu uliopita tulitwaa makombe, lakini sasa tupambane zaidi kuyatwaa tena,” alisema kocha huyo.

Gamondi anaamini kuwa si rahisi kuridhika na hali ya sasa na anachukua jukumu la kuwatia motisha wachezaji wa timu hiyo kila wakati huku akitaka kuona wakijitolea vilivyo, wakiwa tayari kwa changamoto mpya kila msimu kwa kuwa mashabiki wa timu hiyo wana matarajio makubwa.

“Katika soka, hata kama wewe ni kocha epuka sana kosa moja kwa kuwa linaweza   kugharimu ushindi,” anasema.

Malengo ya Yanga msimu huu

Kocha huyo ameweka wazi malengo yake msimu huu na kusema kuwa ni kufika hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwani anaona kuwa lengo la kila msimu ni kuhakikisha Yanga inabaki kwenye kilele cha soka la Tanzania na Afrika, huku akiamini kuwa kufanikiwa kwa timu kunahusisha si tu kuwa bora ndani ya nchi bali pia katika ngazi ya kimataifa.

“Tunajua kuwa wakati mwingine tunakutana na wapinzani wagumu, lakini lengo letu ni kudumisha nafasi yetu katika mashindano ya kimataifa na kusonga mbele kadiri iwezekanavyo, lazima tukiwa bora ndani ya ligi, iwe hivyo na kimataifa,” anasema.

Maendeleo ya Soka la Tanzania

Kocha huyo raia wa Argentina, anaamini kuwa soka la Tanzania limeendelea kwa kasi kubwa, anasema tangu alipojiunga na Yanga, ameona mabadiliko makubwa kwenye Ligi Kuu Bara, jambo ambalo linamfurahisha.

“Kila mwaka ligi inazidi kuwa bora, ninahisi furaha na heshima kubwa kuwa sehemu ya maendeleo haya, naamini kuna watu wamefanya kazi kubwa kuhakikisha haya yanafanikiwa, nawapongeza sana kwa kuwa ubora wa ligi utaendelea kuiboresha na timu ya taifa,” alisema.

Changamoto

Gamondi anafahamu changamoto zinazozikabili timu za Ligi Kuu ya Tanzania, hasa kuhusu mbinu za kiufundi na za kiulinzi za timu pinzani, anasema kuwa katika msimu uliopita, Yanga ilifanikiwa kushinda mechi nyingi dakika za mwisho, jambo ambalo lilionyesha jinsi wapinzani walivyoandaliwa vizuri kiufundi na kiulinzi.

“Ninaona maboresho katika mbinu za kiufundi za wapinzani wetu, jambo linalotufanya sisi pia kuwa bora zaidi, lakini niwashukuru sana viongozi wa Yanga kwa kuleta wachezaji wenye viwango vya juu.

“Kwa sasa tuna wachezaji 14 kwenye timu za taifa, jambo ambalo linaonyesha jinsi kikosi chetu kilivyo bora,” anasema.

Malengo yake Afrika

Akizungumzia kuhusu matarajio yake ya baadaye anasema, anataka kuona anachukua ubingwa wa Afrika.

Anasema anakumbuka msimu uliopita Yanga ilikaribia kufika hatua za juu za michuano ya CAF lakini ikakutana na changamoto kadhaa.

“Ndoto yangu ni kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika naamini ni jambo ambalo linawezekana, ishu ni muda na kujipanga vizuri,” alisema Gamondi aliyechukua nafasi ya Nasreddine Nabi.

Mechi za watani wa jadi

Gamondi anasema anafahamu vyema umuhimu wa mechi za watani wa jadi dhidi ya Simba ambapo walikutana kwenye Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu huu na Yanga kupata ushindi wa bao 1-0.

“Nafahamu jinsi ilivyo muhimu kushinda mechi ya watani wa jadi kwa mashabiki, lakini kwangu lengo ni kushinda michezo yote iwezekanavyo ili kuwa bingwa,” anasema.

Gamondi anaelezea jinsi mechi za watani wa jadi zilivyo na shinikizo kubwa zikiambatana na hisia kali na ushawishi mkubwa kwa wachezaji, anaamini kuwa msimu huu utakuwa mgumu zaidi, hasa kwa kuwa Simba imefanya mabadiliko makubwa katika benchi la ufundi na kuongeza wachezaji wapya.

“Simba ni wapinzani bora na kila msimu changamoto inazidi kuwa kubwa, nafikiri sasa wamejipanga vizuri pia,” anasema.