
Dar es Salaam. Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya vibonde wa Ligi Kuu Bara, KenGold, kitu kimemfanya kocha Miguel Gamondi kurudi kupitia video ya mechi hiyo na kubaini kitu, kisha akasisitiza, hakuna namna lazima atengeneze mbinu mpya kwa mastraika wote na timu kwa ujumla dhidi ya ‘wapaki basi’.
Yanga imecheza mechi mbili za Ligi Kuu ikiwamo ile ya kwanza dhidi ya Kagera Sugar na kuifunga mabao 2-0 kabla ya Jumatano kuinyoa KenGold kwa mbinde kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Katika mechi hizo Yanga imekumbana na wakati mgumu hasa kufungua safu ya ulinzi kwa upande wa Kagera kwani mabao yote yalipatikana kutokana na mashuti ya mbali ya Maxi Nzengeli na Clement Mzize.
Hata katika mchezo dhidi ya KenGold, Yanga ilifunga bao 1-0 dakika ya 13 kupitia kwa beki wa kati, Ibrahim Bacca aliyepanda wakati Stephane Aziz KI anapiga friikiki na kujitwisha mpira kuukwamisha wavuni na baada ya hapo, washambuliaji wa Yanga walishinda kufanya lolote hadi pambano lilipomalizika. Akizungumza na Mwananchi, Gamondi alisema, amegundua na anajua kuwa, timu nyingi zinakuja na akili ya kujilinda ili kuzuia kufungwa mabao mengi, hivyo wanajipanga upya ili kuwa na machaguo ya mbinu za kutengeneza mabao hata kama wakikutana na timu zenye kupaki basi.
“Kwenye mazoezi yetu kuanzia juzi na jana tumeanza kujipanga na hilo kuhakikisha tunakuwa tayari kukabiliana na ugumu wa namna hiyo. Nimeamua hivyo, ili kuwafanya mabeki wa pembeni, viungo na hata washambuliaji kuwa na njia nyingi za kutengeneza nafasi na hata kutumia nafasi ambazo watakazipata,” alifichua Gamondi anayeinoa Yanga kwa msimu wa pili akiwa ameshatwaa mataji matatu, ikiwamo Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, huku akiwa amebeba kombe la Toyota ikiwa Afrika Kusini.
“Baada ya hapa hakuna timu itakayotusumbua, kwani hatutakubali kupata ushindi mdogo tena katika michezo inayofuata,” aliongeza Gamondi anayejiandaa kuiongoza tena Yanga kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuikabili KMC ambayo msimu uliopita ilipigwa nje ndani kwa mabao 5-0 na 3-0 mtawalia.
Kwa maelezo ya Gamondi ni wazi washambuliaji wa timu hiyo, wakiongozwa na Prince Dube, Clement Mzize, Kennedy Musonda, Jean Baleke na viungo washambuliaji Pacome Zouzoua, Aziz KI, Duke Abuya, Mudathir Yahya, Maxi Nzengeli kupewa mbinu mpya ya kuwabeba mbele ya mabeki wa timu pinzani.
Lakini hata mabeki wa pembeni kama Yao Kouassi, Chadrack Boka, Kibwana Shomari, Nickson Kibabage na mawinga wa timu hiyo watakuwa na kazi ya kusaidiana na wenzao kuona Yanga inarudi katika makali kama ilivyokuwa katika mechi za kimataifa ambapo imecheza mechi nne na kufunga jumla ya mabao 17-0.
Yanga ilianza raundi ya kwanza kwa kuifunga Vital’O ya Burundi kwa mabao 4-0 kisha 6-0 na kutinga raundi ya pili ilipoitambia CBE SA ya Ethiopia kwa bao 1-0 ugenini na kuichapa 6-0 Uwanja wa Amaani.
Pia katika mechi za Ngao ya Jamii Yanga ilipata jumla ya ushindi wa mabao 5-1, ikianza kwa kuilaza Simba kwa bao 1-0 kisha kuifumua Azam FC kwa mabao 4-1 na kuirudisha ngao hiyo baada ya msimu uliopita kunyakuliwa na Simba kwa penalti 3-1 ikiwa imelishikilia kwa misimu miwili mfululizo ikiimnyuka Mnyama.