Gambo ahoji kusuasua ujenzi wa stendi ya mabasi Arusha

Dodoma. Mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, amemuhoji Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange, ikiwa yuko tayari kujiuzulu endapo ujenzi wa stendi ya kisasa katika eneo la Bondeni City, jijini Arusha, hautakuwa umeanza kufikia Mei 2025.

Akiuliza maswali ya nyongeza bungeni leo Jumanne, Aprili 15,2025, Gambo amesema anafahamu kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha kupitia Mradi wa Kuboresha Miji (TACTICS)  na fedha zipo.

“Tumekua tukipata majibu ya Serikali ambayo hayatekelezeki zaidi ya mara nne. Je, mheshimiwa naibu waziri yupo tayari kujiuzulu iwapo hadi kufikia Mei mwaka huu mkandarasi hatoanza ujenzi wa stendi ya kisasa?” amehoji.

Amesema kumekuwa na baadhi ya viongozi wanaotoa kauli kwa sababu ya msimamo wa mbunge na kwamba Serikali iko tayari kutoa maelezo kuhusu nini hasa kinachokwamisha ujenzi wa stendi hiyo ya kisasa.

Akijibu maswali hayo, Dk Dugange amesema wanafahamu umuhimu wa stendi hizo, lakini ni lazima taratibu za manunuzi zifuatwe.

Naibu waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange akijibu maswali ya wabunge leo Aprili 15,2025 bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Dk Dugange amesema kuwa Serikali ilitangaza zabuni na makandarasi walijitokeza, lakini hawakukidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za manunuzi.

Ameeleza kuwa kuendelea na mchakato huo kwa kumpatia kazi mkandarasi asiye na uwezo ingekuwa ni ukiukwaji wa sheria.

“ Dhamira ya Serikali ni thabiti na iko palepale na sasa tuko katika hatua za mwisho na tunaamini ifikapo Mei mwaka huu ujenzi utaanza na utakamilika Mei mwakani,”amesema.

Kuhusu mbunge kukwamisha ujenzi, Dk Dugange amesema si kweli kwamba mbunge wa Arusha mjini anakwamisha ujenzi wa stendi hiyo.

Amesema kuwa kumekuwa na taratibu zinaendelea na makandarasi waliopatikana walikuwa na upungufu hivyo Serikali inaendelea kutangaza ili mkandarasi sahihi aweze kupatikana.

Katika swali la msingi, Gambo amehoji ni lini Serikali itaanza na kumaliza ujenzi wa Stendi ya Kisasaya Jiji la Arusha katika eneo la Bondeni City.

Akijibu swali hilo, Dk Dugange amesema Halmashauri ya Jiji la Arusha ni miongoni mwa Miji 45 wanufaika wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya Miji ya Tanzania (TACTIC).

“ Jiji hili lipo katika kundi la kwanza (Tier 1) ya utekelezaji yenye miji 12 ambapo tayari miradi ya awamu ya kwanza ya barabara na mitaro yenye thamani ya takriban Sh20 bilioni ilianza kutekelezwa kwa kusaini mikataba ya ujenzi Septemba, 2023,”amesema.

Amesema kukosekana kwa makandarasi wenye vigezo kupitia zabuni zilizotangazwa Machi, 2024 katika miji minne ikiwemo Halmashauri ya Jiji la Arusha, Serikali imetangaza zabuni ya kumpata mkandarasi kwa mara ya pili Machi 2025. Mchakato huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Aprili, 2025 ambapo mshindi atatangazwa.

 “Utekelezaji unatarajiwa kuanza Mei 2025 ambapo ujenzi huu unatarajiwa kuwa wa mwaka mmoja na unategemewa kukamilika ifikapo Mei 2026,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *