Gachagua awindwa na polisi, sababu yatajwa

Nairobi. Maofisa wa Jeshi la Polisi nchini Kenya wamezingira makazi ya aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua kwa lengo la kumkamata kwa kile kinachotajwa kuwa ni tuhuma za kuchochea vurugu nchini humo.

Hata hivyo jitihada za polisi hao hazikuzaa matunda kwani hawakufanikiwa kumkamata mwanasiasa huyo.

Tovuti ya Daily Nation imeripoti jana kuwa mwishoni mwa wiki, Naibu Rais, Kithure Kindiki na Waziri wa Ulinzi, Kipchumba Murkomen walimuonya Gachagua, wakimtuhumu kuchochea ukabila kwa masilahi yake binafsi ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa urais wa 2027.

Wawili hao walisisitiza kuwa Gachagua, aliyeondolewa madarakani na Bunge Oktoba, 2024, baada ya kuhudumu kwa miaka miwili kama Naibu Rais, si mtu asiyeguswa wala aliye juu ya sheria.

Lakini Gachagua alijibu vikali, akiwakejeli Profesa  Kindiki na Murkomen kwa vitisho vya kutaka kumkamata. Badala yake, Gachagua aliwataka wawili hao wajikite katika kushughulikia masuala ya ‘watekaji nyara na wauaji’ katika wimbi la mauaji ya kiholela.

“Sijaamuru mtu yeyote achukue silaha. Nachukia vurugu na hali ya kutokuwa na utulivu. Ninaionya IEBC (Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)) kwamba siasa zetu ni tete. Ni wajibu wangu wa kiraia kutoa tahadhari. Hali tuliyonayo sasa haitakubali mchezo wa uchaguzi mwaka 2027,” alisema Gachagua Jumapili.

Hata hivyo, maofisa wa Serikali walisema hawatasita kumkamata Gachagua iwapo ataendelea kuwa tishio kwa usalama wa taifa.

Viongozi hao walisema Gachagua anajaribu kubadili changamoto zake binafsi kuwa mgogoro wa kitaifa kwa kuingiza nchi katika kampeni za mapema zilizojaa vitisho vya vurugu.

Hatua ya utawala wa Rais Ruto ilikuja baada ya Gachagua kuonya kuwa nchi inaweza kukumbwa na vurugu mbaya zaidi za uchaguzi kuliko zile za mwaka 2007, endapo IEBC itaharibu uchaguzi wa 2027.

Ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/08 zilikuwa na msingi wa kikabila, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000.

“Mwache huyo mtu aendelee kupiga kelele na kuchochea Wakenya. Tutamkamata. Siku nyingine alisema akiondolewa madarakani kutakuwa na vurugu Kenya; kulikuwa na vurugu? Hapana. Alipoona hakuna vurugu, alirudi nyumbani na kujifanya ndiye aliyewatuliza watu. Tutamkamata,” alisema Murkomen kwa lahaja ya Kalenjin katika hafla huko Iten Jumamosi, kabla ya kurudia ujumbe huo kwa Kiingereza.

Murkomen alirudia kauli kama hiyo Jumapili katika Kaunti ya Trans Nzoia. Akiashiria kuwa Gachagua si mtu asiyeweza kuguswa.

Waziri Murkomen alisema Serikali inaelewa njama ya wanasiasa wanaotaka kuwafanya Wakenya wahisi kutokuwa salama na kuionyesha serikali kama isiyo na utulivu.

“Wajue kuwa hawako juu ya sheria. Tumejitolea kuhakikisha taifa lenye amani na usalama kwa wote, na hatutatishwa na yeyote anayefikiria hatutamgusa kwa sababu ya nafasi yake,” alisema Murkomen.

Katika mazishi huko Matisi, Kitale Jumamosi, Waziri huyo alimtahadharisha Gachagua kuwa atawajibishwa kwa matamshi yake na uwezekano wa machafuko katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Wale wanaotaka kueneza hofu miongoni mwa Wakenya watawajibika kwa sababu hakuna mtu aliye juu ya sheria. Hakuna atakayeruhusiwa kusema chochote anachotaka na kutishia amani ya nchi,” alisema Waziri huyo.

Kwa upande mwingine, akizungumza huko Amogoro, Teso Kaskazini wakati wa ibada ya kidini ya madhehebu mchanganyiko, Profesa Kindiki aliwafananisha viongozi wanaotoa matamshi ya kuchochea vurugu na Al-Shabaab na majambazi wa Bonde la Ufa wanaowajeruhi na kuwaua Wakenya wasio na hatia.

“Nchi yetu haina hatari ya kupitia machafuko ya kabla au baada ya uchaguzi kama yale ya 2007/08. Wanaotabiri hali kama hiyo ni maadui wa kweli wa Wakenya na wanapaswa kukataliwa kwa gharama yoyote,” alisema Profesa Kindiki.

Naibu Rais alisema Wakenya walijifunza somo chungu katika machafuko ya 2007/08, na hawawezi kuruhusu kurudia kwa hali kama hiyo tena huku akiwahakikishia raia wa Kenya kuwa uchaguzi wa 2027 utakuwa huru, wa haki na wa amani.

“Unabii wao wa maangamizi unatokana na ukosefu wa uzalendo na kutokujua siasa,” alisema Profesa Kindiki.

“Kiongozi yeyote, awe wa kisiasa au kidini, anayechochea au kuchangia chuki za kikabila si mzalendo na ni wa kurudisha nyuma maendeleo. Wanasiasa wanaochezea hisia kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 kwa gharama ya miradi ya maendeleo ni makatili na maadui wa watu.”

Gachagua alisema hajafanya kosa lolote linalostahili vitisho vya kuzua hofu.

Alisema anatarajia IEBC itambue kuwa uchaguzi wa 2027 hautahusu Serikali pekee, na mwenendo wake mzima utaelekeza nchi inakoelekea, hasa iwapo makamishna wake na wafanyakazi watashindwa kutekeleza misingi ya haki, demokrasia, uwazi na uadilifu katika kusimamia uchaguzi huo mkubwa.

Gachagua alisema machafuko ya baada ya uchaguzi wa 2007 yanaweza kutokea tena.

“Sisi si watu wa kusahau. Watoto wasio na hatia na wazee walichomwa hadi kufa ndani ya Kanisa la Kiambaa kule Rift Valley,” alisema.

Gachagua alisema Serikali ya Rais Ruto ina hatia ya kuchochea vurugu na haipaswi kujifanya kuwa na msimamo wa kimaadili wa kuwaita wengine wavutiaji wa vurugu.

“Serikali hii imekuwa ikituma wahuni kwenye mazishi, harusi, makanisa… Serikali inakuza Mungiki, na wafuasi wake ndio wamekuwa wakivuruga mikutano yangu, sasa mara saba,” alisema.

Gachagua alimshauri Profesa Kindiki badala ya kutoa vitisho, ajibu kwanza nafasi yake katika wimbi la utekaji nyara na mauaji ya kiholela ya waandamanaji wa Gen Z.

“Ukweli ni kwamba huwezi kutoroka doa la mauaji ya Gen Z. Ilitokea ukiwa Waziri wa Usalama wa Ndani. Huwezi kushutumu vurugu wakati mikono yako imeloa damu ya Gen Z. Huwezi kusema mambo mawili tofauti kwa wakati mmoja,” alisema Gachagua.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *