
Dar es Salaam/Nairobi. Saa chache tangu Jeshi la Polisi nchini Kenya, litangaze kuanzisha uchunguzi juu ya kutekwa na baadaye kuuawa kwa Paroko wa Parokia ya Igwamiti ya Kanisa Katoliki huko Nyahururi nchini humo, Padri John Maina, Makamu wa zamani wa Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua ametoa kauli kuhusu mauaji hayo.
Mitandao ya kijamii nchini Kenya, imekuwa na mijadala inayohusisha tukio hilo la mauaji ya Padre Maina na kumkaribisha Gachagua katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25 ya Parokia hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, imebainika Padri Maina alikuwa akifuatiliwa na baadhi ya watu waliokuwa wakimtaka awagawie pesa alizodaiwa kupewa baada ya kuongoza sherehe ya Jubilei ya miaka 25 ya Parokia ya Igwamiti, iliyohudhuriwa na Gachagua.
Kupitia chapisho lake kwenye akaunti yake ya mtandao wa X, Gachagua amesema kifo cha Padre Maina ni pigo kwake huku akisema kiongozi huyo alikuwa mshauri wake wa karibu.
Huku akieleza kushtushwa na kusikitishwa na kifo cha padre huyo, Gachagua amesema alikuwa anapenda kusimamia ukweli na anachokiamini huku akitoa pole kwa familia yake.
Katika chapisho hilo Gachagua ameandika: “Kifo cha Padre John Maina Ndegwa, Paroko wa Parokia ya Igwamiti huko Nyandarua, ni cha uchungu mkubwa sana. Padre John alikuwa mtu wa kipekee na mchungaji wa kundi la Bwana; aliishi kwa ukweli na alisema ukweli bila kuogopa wala kupendelea, kama vile Kristo angefanya.”
“Wiki mbili kabla ya kufariki kwake, Padre John alinikaribisha katika sherehe za jubilee yake ya miaka 25, ambapo alitoa mahubiri yenye nguvu na akaeleza kwa ujasiri maoni yake kuhusu hali ya Taifa.”
“Alikuwa rafiki yangu wa karibu na mshauri wangu kwa muda mrefu. Tulikutana mara kadhaa na kujadili masuala mengi ya kitaifa. Naziomba taasisi za usalama kuharakisha uchunguzi na kuwakamata waliohusika na kitendo hiki cha kikatili na kuwafikisha mbele ya sheria.”
Ameendelea kwa kuandika kuwa, “natoa rambirambi zangu za dhati kwa Askofu, Jimbo Katoliki la Nyahururu, waumini wa Parokia ya Igwamiti, na familia nzima ya Kanisa Katoliki.Namwomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya Padre John kwa amani ya milele na mwanga wa milele umwangazie daima.”
Taarifa ya Polisi
Taarifa ya Polisi iliyotolewa Mei 20, 2025 na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) nchini Kenya, kupitia ukurasa wake wa X, imewataka raia wa Kenya kuwa watulivu kutokana na tetesi hizo mitandaoni.
DCI amebainisha Padre huyo alipatikana Mei 15, 2025 kando ya Barabara ya Nakuru akiwa na majeraha kichwani na alimweleza msamaria aliyemwokota kuwa alikuwa ametekwa katika Parokia yake, iliyopo umbali wa kilomita 40.
Ingawa taarifa hiyo ya DCI haikueleza ilipo gari yake aina ya Subaru Forester, lakini taarifa katika mitandao ya kijamii zinaeleza kuwa gari hilo bado halijapatikana hadi sasa.
Taarifa hiyo ya DCI imeeleza kuwa Aprili 27, 2025, Padri Maina alihudhuria Jubilei hiyo na ibada ya kuwekwa wakfu kwa Padri Simon Thuita iliyohudhuriwa pia na Gachagua, akiwa ameandamana na wanasiasa wengine wa Taifa hilo la Afrika Mashariki.
“Mnamo Mei 15, 2025, Padri Maina alipatikana kando ya barabara ya Nakuru kuelekea Nairobi na msamaria mwema, ambaye ni dereva wa bodaboda, karibu na kituo cha Diotomite akiwa na majeraha kichwani upande wa kushoto,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
“Dereva huyo alimpeleka Padri Maina katika Hospitali ya Misheni ya Mt. Joseph huko Gilgil. Alipofikishwa hospitalini, alionekana kuwa na majeraha ya wazi, yakiwemo ya kichwa upande wa kushoto yaliyokuwa yanavuja damu”.
“Licha ya jitihada za wahudumu wa afya, Padri Maina alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu dakika chache baada ya kulazwa,”ameeleza DCI.
“Mwili wake ulihamishiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Kaunti Ndogo ya Nyahururu kutokana na ombi la waumini wenzake kwa ajili ya kuhifadhiwa na kufanyiwa upasuaji wa uchunguzi kubaini sababu za kifo chake”
Kwa mujibu wa DCI, Mei 19, 2025, upasuaji ulifanywa na daktari wa serikali na matokeo ya awali yalionesha kuwa majeraha ya kichwani aliyokuwa nayo Padri Maina huenda hayakuwa chanzo cha kifo chake.
Mwanapalotholia wa Serikali, Titus Ngulungu ndiye aliyefanya uchunguzi wa mwili wa Padri huyo katika Hospitali ya Pope Benedict Catholic, lakini taarifa nyingine ambazo hazijathibitishwa zilidai alipigwa na kitu butu kichwani na wengine risasi.
Naibu Mkuu wa Dayosisi ya Nyahururu, Padri Timothy Maina pamoja na mapadri wengine 10 na ndugu wa marehemu walihudhuria uchunguzi huo, huku taarifa zingine zikidai mwili ulikuwa umejaa damu na majeraha yanayoonekana ni risasi.
DCI katika taarifa hiyo ameeleza kuwa maofisa wa upelelezi kutoka katika ofisi hiyo wanachunguza taarifa kwamba Padri Maina alikuwa amedai maisha yake yalikuwa hatarini, ingawa hakuwahi kuripoti hilo katika kituo chochote cha polisi.
Maofisa wa upelelezi wanaendelea kufuatilia ushahidi wa kitaalamu ili kuunda upya matukio ya mwisho ya Padri Maina na kuwakamata washukiwa, huku ikiwaomba wananchi wenye taarifa sahihi kuziwasilisha kwao.
“DCI inawahimiza wananchi kubaki watulivu katikati ya tetesi zinazozunguka mitandaoni. Timu yetu ya wachunguzi inafanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu ili kulitatua suala hili kwa uangalifu wa hali ya juu, kuhakikisha haki inapatikana.”
Akizungumzia mauaji hayo, Seneta wa Nyandarua, John Methu ameelezea namna Padri huyo alivyompokea Gachagua na ujumbe wake katika maadhimisho ya Parokia ambayo yaliambatana na harambee kuchangia ununuzi wa gari.
“Tumeshtushwa sana kusikia kuhusu kifo cha Padri Maina. Padri alimuhudumia Gachagua na timu yetu katika maadhimisho ya siku ya familia ya Parokia yaliyofanyika wiki mbili zilizopita. Apumzike kwa amani,”amesema.
Habari hii imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mitandao mbalimbali ya kijamii.