Gabriel Kipija: Chimbuko la mastaa Mbeya

Ukiona vyaelea, jua vimeundwa. Ndivyo unaweza kusema kuelezea baadhi ya mastaa wa Ligi Kuu wanaotamba katika timu tofauti kutoka mkoani Mbeya kujulikana chimbuko lao.

Mbeya ni moja ya mikoa nchini yenye historia ya kuzalisha vipaji ambapo kwa miaka mitatu nyuma, ilikuwa ya pili kuwa na timu nyingi za Ligi Kuu ikitanguliwa na Dar es Salaam.

Katika mwaka wa 2022, Mbeya ilikuwa na timu nne za Tanzania Prisons, Mbeya Kwanza, Mbeya City na Ihefu na kuamsha chachu ya maendeleo katika maeneo mbalimbali kiuchumi.

Pamoja na wachezaji wengi wanaong’ara Ligi Kuu, baadhi yao wametoka kwenye mikono ya mtu mmoja, Gabriel Kipija mwenye makazi yake wilayani Kyela ambaye hatajwi sana.

Wachezaji kama Aziz Andabwile (Yanga), George Mpole na James Mwashinga (Pamba), Chrispin Ngushi (Mashujaa), Godfrey Manyasi (Kagera Sugar) na Mwisho Yangson wa Namungo.

Pia waliwahi kupita mastaa kama Emanuel Mwagamwaga na Gaudence Mwaikimba ambao kwa sasa ni makocha na wanaendelea na shughuli zao wilayani Kyela kufundisha soka.

Wamo pia, Habibu Nassoro (TMA), Jonathan Ngesa aliyewahi kucheza Ihefu (kwa sasa Singida BS), Justine Manento ambaye ni mchezaji wa Vollyball na mwalimu wa taaluma shule ya Sekondari Keifo.

Hao wote ni baadhi ya nyota waliopita mikononi mwa Kipija ambaye ameamua kuwekeza kwa vijana kuwafungulia dunia, kuanzia elimu hadi vipaji ili kufika mbali.

Katika mazungumzo na Spoti Mikiki, Kipija ameelezea sababu ya kurejea nyumbani Kyela mkoani Mbeya baada ya kuishi zaidi ya miaka 15 nchini Marekani alipokuwa akiishi baada ya masomo yake.

Kipija ambaye hazungumzwi zaidi popote, anasema baada ya kukaa Marekani alipokuwa akisoma elimu ya lugha na michezo, aliamua kurudi nyumbani ili kusaidia Watanzania.

Anasema aliona kugeukia michezo ikiwa ni sehemu ambayo vijana wengi wanapata ajira na kuendesha maisha yao.

Anasema kutokana na mafanikio ya kuzalisha baadhi ya wachezaji wanaotamba Ligi Kuu na Championship, mkakati wake ni kutengeneza vijana wengine wenye vipaji.

“Niliona nitahukumiwa na historia, kwamba nimezaliwa hapa Kyela, nimeishi Marekani, je hawa Watanzania wenzangu watanisikiaje, nakula raha huko wakati huku shida tupu.”

“Nikaamua kuanzisha shule na kituo cha michezo kiitwacho Keifo (Kyela Education Improvement Foundation), ambacho kitatoa elimu na vipaji na nimeweza kuwapa njia hao wachezaji,” anasema Kipija.

Kuhusu Boma FC

Kipija ambaye alikuwa mmiliki wa Boma FC, anasema baada ya kuanzishwa shule za Keifo walishiriki Ligi ya Wilaya, Mkoa hadi Kanda na kufanya vizuri, ambapo aliamua kuibadili jina.

Katika mabadiliko hayo alinunua timu ya mtaani iliyoitwa Shangwe na kubadili jina na kufahamika Boma FC, ambapo ilishiriki daraja la pili (kwa sasa First League) na hatimaye Daraja la Kwanza (Championship).

Hata hivyo, anaeleza kuwa pamoja na malengo aliyokuwa nayo hayakutimia baada ya timu hiyo kushuka daraja kutokana na mambo ya kisiasa yaliyosababisha kupoteana.

“Baadaye timu ilipitia ugumu kwa mambo ya kisiasa, tukafungiwa uwanja wa nyumbani pale Mwakangale, tukaanza kuhangaika na viwanja timu ikapoteza mechi hadi kushuka daraja na hatimaye kupotea hadi leo,” alisema Kipija.

Mkakati mpya

Mkurugenzi huyo, anasema kuwa kwa sasa amerejesha nguvu mpya katika kuandaa kituo cha michezo na jukumu la kusimamia amempa Mwagamwaga.

Anasema vijana kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya wenye uwezo na vipaji wanakaribishwa kwani watapata huduma zote ikiwemo elimu ya darasani na kuendeleza vipaji.

Anasema uongozi umejipanga kuhakikisha kijana anayefika shuleni hapo anakuwa bora kitaaluma na kuendeleza kipaji kuliko awali ilivyokuwa kuzingatia kipaji tu.

“Nimeanza kufufua upya kituo na atasimamia Mwagamwaga, tutazingatia anayefika hapa anapata elimu darasani na kuendeleza kipaji, lakini niombe serikali kutoa japo ruzuku kidogo kwa wadau wanaowekeza kwa vijana,” alisema Kigogo huyo.

Uongozi wa shule

Mkuu wa shule hizo, Mpoki Mwaifunga anasema uongozi umejipanga kuzingatia ratiba za michezo na darasani kuhakikisha kila anayeingia kituoni hapo anapata huduma stahiki.

“Tunao vijana kama mifano akiwamo Edgar Mwaisunga ambaye katika Umitashumta mwaka jana aliitwa timu ya Taifa ya Vijana, tutajipanga kuzingatia ratiba darasani na michezoni”

Kwa upande wake Kocha wa kituo hicho, Mwagamwaga amesema vijana watakaoibuliwa watakuwa katika ubora kama ambavyo wengine walipita akieleza kuwa mkakati ni kutengeneza timu bora za Taifa.

“Tutarajie kina Andabwile wa baadaye, tumejipanga kama sehemu ya benchi la ufundi kufikia malengo, nimekua na kulelewa na Kipija hivyo anachofanya ni kurudisha kwa jamii,” alisema Mwagamwaga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *