
Rais wa zamani wa Gabon Ali Bongo Ondimba na familia yake wameachiliwa na wamewasili Luanda, ofisi ya rais wa Angola imetangaza siku ya Ijumaa, Mei 16, na kutuma picha kwenye mitandao ya kijamii. Habari hizi zinakuja siku tano baada ya kuachiliwa kutoka jela kwa mke wa Ali Bongo, Sylva, na mwanawe, Noureddin, kulingana na vyanzo vya RFI. Familia hiyo ilikuwa imezuiliwa tangu mapinduzi yaliyoongozwa na Jenerali Brice Clotaire Oligui Nguema mnamo 2023.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Siku tano baada ya kuachiliwa kutoka jela kwa mke wa rais wa zamani Ali Bongo, Sylvia Bongo na mxanao Noureddin, Luanda imetangaza kuwa rais huyo aliyeondolewa madarakani Ali Bongo Ondimba na familia yake wametua Angola. Hatua hiyo inahitimisha miezi 19 ya kuzuiliwa huko Libreville, kufuatia mapinduzi ya Jenerali Brice Clotaire Oligui Nguema.
“Kufuatia jitihada za Rais wa Jamhuri ya Angola na Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, João Lourenço, pamoja na Rais Brice Oligui Nguema wa Gabon, familia ya Bongo imeachiliwa na ndiyo imewasili Luanda,” ofisi ya rais imetangaza kwenye mitandao ya kijamii, ikionyesha picha kuthibitisha habari hiyo. Kwenye picha hizo Ali Bongo, anaonekana akitabasamu akijikongoja kwa kutumia fimbo yake, akishuka kwenye ndege ya serikali ya Angola. Kulingana na chapisho la ofisi ya rais wa Angola, “baada ya majadiliano kati ya João Lourenço na Brice Clotaire Oligui Nguema, familia ya Bongo iliachiliwa na ndiyo imewasili Luanda.”
Rais wa sasa wa Umoja wa Afrika, João Lourenço, alisafiri kwenda Libreville siku ya Jumatatu, Mei 12, kuthibitisha maridhiano yake na mwenzake wa Gabon, baada ya kipindi cha mpito ambapo mahusiano yalikuwa si mazuri. Lakini João Lourenço pia alichukua fursa ya ziara yake kukutana na Ali Bongo nyumbani kwake katika wilaya ya Sablière, ambako alikuwa amefungwa tangu kupinduliwa kwake Agosti 30, 2023.
Swali la kesi ya Silvia na Noureddine Bongo
Kabla ya ziara hii, Sylvia na Noureddin Bongo walikuwa wamechukuliwa kutoka chumba walikokuwa wanazuiliwa wiki iliyopita na kurudi kwenye makazi yao, hali ambayo ilichochea uvumi wa watu hao kwenda uhamishoni. Mamlaka haijazungumzia chochote kuhusu kubadilika kwa msimamo wake.
Wala mawakili hawajazungumza chochote, lakini walikumbuka kuwa Aprili 30, Umoja wa Afrika uliomba tena kuachiliwa kwa Familia ya Bongo. Wakati wa mpito, mawakili wa Sylvia na Noureddine Bongo walilaani unyanyasaji huo na kuomba bila mafanikio kuhamishwa kwa wateja wao kwa ajili ya matibabu.
Kabla ya kuchaguliwa kwake kuwa rais mapema mwezi Aprili, Brice Clotaire Oligui Nguema alisema kwamba kesi “itafanyika.” Kwani Sylvia na Noureddine Bongo wanashitakiwa kwa makosa kadhaa yakiwemo ubadhirifu wa fedha za umma na utakatishaji fedha.
Katika taarifa yake kwa umma muda mfupi baada ya kuwasili Luanda, mwendesha mashtaka wa Gabon amesema kuwa Sylvia na Noureddin Bongo wameachiliwa huru wakisubiri kesi inayowakabili.