Dar es Salaam. Awali lilipotajwa jina G Nako, wengi kwenye vichwa vyao zilisikika ngoza za Hip-Hop, lakini kwa sasa imekuwa tofauti kwani msanii huyo ameendelea kuonesha uwezo wake wa kutambaa na midondoko ya aina tofauti tofauti ya muziki.
Kwa mara ya kwanza msanii huyo alifahamika kupitia kundi la Hip-Hop la Nako 2 Nako ambalo lilikuwa linaundwa na wanachama wanne ambao ni Lord Eyez, G Nako, Ibra da Hustler na Bou Nako. Msanii Ibra Da Hustler alijitoa kwenye kundi Novemba, 2008.
Baadhi ya nyimbo maarufu walizotoa ni pamoja na Ndio Zetu Kuwakilisha (2005), Bang (2007), Hawatuwezi (2005), Bang Rmx (2008), Mchizi Wangu (2008), Hakuna Mahali Kama (2008), Hiphop (2008), Iko Wazi (2009), Mpango Mzima (2010), Wawiwo (2010), na Katikati (2010).
Baadaye kundi hio lilivunjika na G Nako akajipata kwenye Kundi la Weusi ambalo hapo awali lilikuwa linaundwa na Joh Makini, Nikki Wa Pili, G Nako, Lord Eyes na Bonta Maarifa, lakini baadaye Bonta alijitoa.
Kwa muda wote wakali hao wameweza kutengeneza Hit kama Gere, Humu Tuu, Show Time, Nicome, Mdundiko na zingine nyingi.
G Nako ngoma ambazo amekuwa akifanya kuanzia Nako 2 Nako hadi Weusi na zile ambazo amefanya kama Sol Artist amefanikiwa kufanya kwa mitindo tofautitofauti, kama vile mtindo wa Hip-Hop na Bongo Fleva, lakini pia Amapiano.
G Nako alifanikiwa kusimama kama rapa na mashabiki wakaukubali uwezo wake. Desemba 3, 2012, alitoa wimbo wa Mama Yeyo ambao amemshirikisha BenPol. Kwenye ngoma hiyo kapita kwa midondoko ya rap kitu ambacho kinafanya wimbo huo kuonekana classic mpaka leo.

Siyo hivyo tu, utakumbuka kwa asilimia kubwa nyimbo alizofanya chini ya Nako 2 Nako na Weusi, alizifanya kwa mtindo wa rap. Kama ile Interlude iliyotoka Julai 2, 2020.
Miongoni mwa ngoma kali ni hii Arosto ya kwake G Nako Ft Chin Beez & Nikki Wa Pili ambayo ilitoka Mei 20, 2024.
“Nikaanza peleka round kwanza, Nikamuendea kumuombea tenga mamaa, Nkamvuta chemba, Tema cheche kadhaa.” Amechana G Nako kwenye Arosto.
Ukiachana na michano, G Nako anatajwa kama mmoja wa wasanii wenye uwezo mkubwa wa kuimba viitikio kwenye muziki wa Bongo Fleva na hilo limejionesha katika ngoma nyingi ambazo ameshirikishwa.
“Kanipa maarifa, yakanipa nyadhifa, ikajipa sifa, kaziba nyufa, namuita ye mfalme.” Ameimba G Nako kwenye kiitikio cha wimbo Mfalme.
Hata hivyo, mkali huyu ni miongoni mwa wasanii ambao wameweza kuendana na kila soko la muziki ambalo Bongo Fleva imepitia.

Ndani ya miaka minne muziki wa Amapiano umekuwa ukifanya vizuri Bongo na Afrika kiujumla. G Nako pia ni miongoni mwa wasaniii ambao wameufanya kwa viwango vikubwa, Novemba 10, 2023 alishirikiana na Diamond Platnumz kwenye ngoma ya Komando ambayo ipo kwenye mtindo wa Amapiano,
Komando ni miongoni mwa ngoma ambazo zimempa mafaniko makubwa G Nako ikiwemo kutazamwa zaidi ya mara milioni 9 kwenye mtandao wa Youtube. Hii haikuwa mara ya kwanza kwake kufanya aina hii ya muziki, utakumbuka 2023 alishirikishwa na Jux kwenye wimbo wa Shugga Daddy.

Oktoba 31, 2024, Maua Sama aliwashirikisha G Nako, Jaiva & Ibra kwenye ngoma yake ya Kariakoo ambayo ni Amapiano na G nako ndio alipiga kiitikio. Mpaka sasa imesikilizwa mara laki mbili ikiwa ni audio tu. Lakini pia ameshiriki kwenye wimbo wa Kinamba Namba wa kwake Billnass ambao ulitoka Oktoba 3, 2024 pia ni Amapiano.
G Nako anaingia kwenye orodha ya wasanii wa Tanzania wenye uwezo mkubwa wa kuimba aina mbalimbali ya muziki.