Arusha. Zikiwa zimebaki siku tatu kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayoadhimishwa kila mwaka ifikapo Machi 8, ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Arusha, wakazi wake wametaja fursa na matarajio yao.
Miongoni mwa fursa zinazotajwa na wakazi wa jiji hilo wakizungumza na Mwananchi leo Jumanne Machi 4, 2025 ni kuongezeka kwa wageni katika jiji hilo la kitalii lenye wakazi milioni 2.4 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo.

Prosper Msaki, ambaye ni mpiga picha jijini hapa amesema idadi ya wateja imeongezeka kutokana na shughuli mbalimbali zilizowekwa kwa sababu ya maadhimisho hayo ikiwamo, tenti la msituni lililofungwa katikati ya jiji.
“Najihusisha na upigaji picha, kufanyika kwa shughuli hii Arusha kumeniongezea fursa ya kupata wateja wengi, kama hapa katika eneo la ‘Clock tower’ pamejengwa hili ‘tent’ la kitalii.
“Pia, zimewekwa sanamu za wanyama, inawavutia watu kutaka kupiga picha na tangu asubuhi biashara yangu imeenda sawa hasa katika wakati huu ambao sio msimu wa utalii (low season),” amesema.
Naye Jasmin Lucas ambaye ni mkazi wa Arusha amesema licha ya fursa za idadi ya watu na wateja kuongezeka lakini bado kuna haja ya kuboresha huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo za afya.

Ameongeza viongozi wakuu wa nchi wanapokuja baadhi ya kero zinakuwa rahisi kufikishwa kwao ikiwamo ubovu wa miundombinu na uboresahaji wa huduma za afya.
“Kwa upande mwingine viongozi wakubwa kama Rais akija katika mkoa wako kuna fursa ya kuona kwa macho changamoto zenu kama hapa ni miundombinu ya barabara pamoja na kuboresha huduma za afya katika hospitali za Serikali,” amesema Jasmin.
Chiku Samuel, ambaye ni muuzaji shanga na bidhaa za kitalii katika eneo la mnara wa saa jijini Arusha amesema sherehe hizo zinaongeza uelewa wa haki za wanawake kutokana na kampeni zinazofanyika.
“Licha ya kuongeza idadi ya watu lakini pia uelewa unaongezeka katika masuala mbalimbali ikiwamo elimu ya usawa, sasa hivi hata uko kwetu kwenye jamii za Kimasai mwanamke anamiliki mifugo na mali.”
“Kwa hiyo natarajia siku hii itaongeza uelewa kwetu wanawake, jamii lakini pia itatoa chachu kwa Serikali kuziwezesha zaidi bishara za wanawake,”amesema.

Wakati wakazi wengine wa Arusha wakitaja fursa na matamanio yao katika upande wa biashara, Theresia Mushi amezungumzia suala la unyanyasaji wa kijinsia huku akitaka likemewe katika siku hiyo.
“Sherehe hizi zinatuongezea wateja hasa eneo hili la mnara wa saa (Clock tower) japokuwa tunatamani zitumike kukemea unyanyasaji majumbani kwetu na hata kwenye biashara zetu,” amesema Theresia.
Theresia amesema bado wapo wanawake ambao wanapigwa na waume zao huku wakikosa sauti ya kuwasemea, pia ameomba mazingira ya biashara kwa wajasiriamali yaboreshwe.
“Kwa sababu kuna baadhi ya familia mama ndiye mtafutaji kupitia biashara, akirudi nyumbani atapata kipigo kwa mume wake, basi huku kwenye biashara aboreshewe mazingira na unyanyasaji ukomeshwe,” amesema Theresia.
Kuhusu namna ya kuzitatua changamoto wanazokumbana nazo wanawake jijini Arusha katika biashara na masuala ya utalii Jumamosi Machi Mosi, 2025 Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) Kanda ya Kaskazini, Steria Ndaga alisema wanawake wanahitaji kuweka mkakati wa kushikana mikono katika sekta hiyo ili wazidi kuongezeka na izidi kuwanufaisha.
Awali, akizungumzia maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema mkoani humo kila kitu ni fursa na wanaigeuza kuwa chanzo cha mapato.
“Kwa upande wetu Arusha sisi kila kitu ni fursa na tunazigeuza kutuingizia kipato, na maadhimisho haya yataongeza idadi ya watu mkoani kwetu, hivyo wafanyabiashara watanufaika katika kila Nyanja,” amesema Makonda.