Fursa mabinti kurudi shule haijatumika

Fursa mabinti kurudi shule haijatumika

Kabla ya Serikali kuruhusu wasichana waliokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito, kelele zilikuwa nyingi. Kelele hizi zililenga kuhamasisha wasichana hawa kupewa nafasi nyingine ili waweze kutimiza ndoto zao.

Nasikitia kusema kwamba bado wasichana wengi katika kundi hili hawajaitumia fursa hii na wengine si kwamba wanakutana na changamoto, bali wameamua kwa kujivunia kabisa kwamba ujauzito ndiyo mlango wao wa kuzikwepa changamoto za kuisaka elimu.

Katika kazi yangu ya uandishi wa habari nikibobea kwenye elimu na habari za jinsia, nimepata bahati ya kufuatilia kwa undani tangu Serikali ilipotoa agizo kuwa wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito warejee shuleni.

Ni fursa adhimu ambayo wasichana hawa waliikosa kwa miaka mingi sana. Awali mfumo wa elimu na taratibu za uendeshaji wake, haukuwapa nafasi wasichana hawa hivyo kufifisha ndoto zao za maisha kwa walio wengi.

Matokeo yake kwa miaka hiyo, inawezekana kabisa Taifa lilikosa wanasayansi, wanasheria, wahasibu , walimu na wataalamu wa kada mbalimbali ambao wangeweza kuwa na mchango kwa jamii zao na Taifa kwa jumla.

Tangu kutolewa kwa fursa hiyo na Rais Samia Suluhu Hassan mara tu alipopata urais, nimewafikia wasichana kwenye mikoa na wilaya mbalimbali na kubaini kuwa fursa hii haijatumika vyema.

Wapo ambao wanashindwa kurejea kwa sababu ya vikwazo, lakini wapo pia walioamua kwamba hawataki tena kujihusisha na elimu.

Hivi karibuni niliembelea wilayani Kilwa nikifuatilia utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Makuzi, Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM).

Nilibaini katika halmashauri hiyo hakuna hata msichana mmoja aliyerudi shuleni baada ya kujifungua, licha ya kuwepo kwa taarifa za wasichana kukatiza masomo kwa sababu ya ujauzito.

Nilijaribu kuwafikia watendaji wanaohusika na elimu kwa ngazi ya msingi na sekondari, ofisa ustawi wa jamii na wadau wa elimu walio nje ya Serikali kote; huko jibu lilikuwa moja hakuna taarifa za msichana yeyote aliyerudi shule baada ya kujifungua ila utoro ni tatizo sugu.

Sikutaka kukubaliana na majibu hayo kwa haraka haraka, ikanibidi kufanya utafiti wangu mdogo kwa kuwafikia wasichana ambao walipata ujauzito wakiwa shuleni na sasa wako nyumbani.

Nikakutana na Arafa Said (18) ni msichana aliyekatisha masomo akiwa kidato cha tatu baada ya kupata ujauzito kwa sasa ni mama wa nyumbani.

Nilipomuuliza kwanini hakurudi shule baada ya kujifungua, alijibu hajioni kama anaweza kukaa tena darasani na watoto, kwa sababu yeye ameshakuwa mtu mzima na mawazo yake kwa sasa ni kumuangalia mtoto. Hilo suala la elimu sio lake tena.

Hamisa Yusuph (19) huyu aliacha shule akiwa kidato cha tatu kwa sasa ni mama wa mtoto wa miaka miwili, ujauzito ulikuja baada ya kuwa tayari alishaacha masomo.

Nilipotaka kujua sababu za yeye kutorudi shule hata baada ya kujifungua, alisema shule haikuwa kitu alichokitaka hata kabla ya huo ujauzito, ndiyo maana aliacha hivyo hawezi kurudi.

Kati yao hakuna hata mmoja aliyetoa aliyetoa taarifa shule kwamba asingeweza kuendelea na masomo kwa sababu ya ujauzito.

Kutokuwepo kwao shuleni ilionekana kama utoro wa kawaida na hatimaye wakapotea kabisa, hivyo hadi sasa hawajulikani wako wapi.

Majibu ya mabinti hawa yanaakisi kile nilichokipata kwa wasimamizi wa elimu ngazi ya halmashauri, kutokuwa na takwimu za wasichana waliokatisha masomo kwa sababu ya ujauzito.

Nasikitika kusema kwamba kwa mwenendo huu inaweza kuwa vigumu kutimiza lengo la Serikali la kuruhusu wasichana hawa kurudi shuleni, kwa sababu wao wenyewe kama walengwa wakuu hawaoni umuhimu wake.

Kama kuna nia ya dhati ya kuhakikisha kila mtoto nchini Tanzania anapata elimu basi kuna haja ya kuongeza makali kwenye ufuatiliaji hasa pale mtoto anapoanza utoro wa rejareja.

Katika hili hatua kali zichukuliwe kwa mtoto mwenyewe, mzazi na hata kiongozi wa mtaa au kijiji ambacho kitakuwa na mtoto aliyekatisha masomo.

Kwa kuwa Serikali imeshafungua milango isiwepo sababu ya mtoto aliyekatisha masomo kushindwa kurejea shuleni, hata kama amepata ujauzito. Akishajifungua zifanyike jitihada kuhakikisha anarudi shuleni kuendelea na masomo iwe katika shule ileile au nyingine atakayochagua, kama mwongozo wa kuwarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali, unavyoelekeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *