Arsenal imepata habari njema baada ya kupata uhakika wa kumtumia mshambuliaji wake Bukayo Saka katika mechi mbili za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid mwezi ujao.
Winga huyo mwenye umri wa miaka 23 alipata maumivu ya nyama za paja yaliyomlazimisha afanyiwe upasuaji na kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu na sasa meneja wa Arsenal, Mikel Arteta anehakikishiwa na jopo la matabibu wa timu hiyo kuwa atamtumia dhidi ya Real Madrid.
Inaripotiwa kwamba mchezaji huyo kwa sasa yupo katika hatua nzuri katika mazoezi ya kuchezea mpira ambayo ni ya mwisho kwa mchezaji aliyetoka majeraha kabla ya kurejea uwanjani na Arsenal inaamini kwamba wiki tatu zilizobakia kabla ya kuivaa Real Madrid zitatosha kumfanya mchezaji huyo awe tayari kwa mechi za robo fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Na ili kumuandaa kwa ajili ya kuikabili Real Madrid, Arsenal imepanga kumchezesha Saka katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya Fulham, Aprili Mosi na kisha mchezo utakaofuata dhidi ya Everton, Aprili 05.
Urejeo wa Saka hapana shaka unamshusha presha Arteta kwani umekuja siku chache tangu mshambuliaji mwingine wa timu hiyo Gabriel Martinelli arejee uwanjani baada ya kukosekana kwa takribani miezi miwili.
Arsenal imekuwa buila Saka tangu Desemba 21 mwaka jana wakati nyota huyo alipoumia katika mchezo wa EPL dhidi ya Crystal Palace ambao Arsenal iliibuka na ushindi wa mabao 5-1.
Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta amethibitisha kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa Saka kurudi uwanjani katika siku za hivi karibuni.
“Anapiga hatua kubwa na amekuwa na maendeleo mazuri. Yuko karibu kurejea. Wiki ijayo tunahitaji kupanga na watu wanaomzunguka katika mazoezi ya kiushindani zaidi na kuona anaweza vipi kwenda nayo.
“Hivyo ngoja tuone pale tutakapoanza kumuweka kwenye timu namna atakavyokuwa na muitikio na namna gani atarudi kwa haraka,” amesema Arteta.

Saka amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa Arsenal msimu huu kutokana na mchango wa mabao ambao amekuwa akiutoa kwa kufunga na kupiga pasi za mwisho.
Katika msimu huu, Saka amehusika na mabao 22 ya Arsenal katika michezo 24 ya mashindano tofauti ambapo amefunga mabao tisa na kupiga pasi za mwisho 13.