Fundi magari mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya Katekista Songwe

Fundi magari mbaroni kwa tuhuma za mauaji ya Katekista Songwe

Songwe. Jeshi la Polisi mkoani Songwe linamshikilia fundi magari, Lameck Mwamlima (29), mkazi wa Migombani, Tunduma, kwa tuhuma za kuhusika katika mauaji ya Katekista wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu.

Mwenda mbali na kuwa Katekista pia ni fundi ujenzi na mkazi wa mtaa wa Migombani-Tunduma Wilaya ya Momba, mkoani Songwe alifariki dunia Mei 10, 2025 kwa kushambuliwa na kitu chenye ncha kali kichwani na maeneo mbalimbali ya mwili.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa mtuhumiwa, Lameck, alitenda kosa hilo kwa kumvamia Mwenda akiwa amelala ndani ya nyumba yake, kitendo kilichosababisha taharuki kubwa katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Alhamisi Mei 22, 2025 na  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Augustino Senga amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji ya Katekista huyo ni wivu wa mapenzi.

 “Uchunguzi wa awali umebainisha kuwa sababu za mauaji hayo ni wivu ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu (Mwenda) kutembea kimapenzi na mke wake.

“Upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na pindi utakapokamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria,” amesema Senga.

Kulingana na Senga mtuhumiwa Lameck alikamatwa Mei 20, 2025 kwa tuhuma za kutekeleza mauaji hayo kwa kutumia kitu chenye ncha kali kichwani na maeneo mbalimbali ya mwili.

“Ninatoa wito kwa wananchi wote wa mkoani Songwe kuacha kujichukulia sheria mkononi, kwani matatizo ya migogoro ya kifamilia na ugoni yanaweza kushughulikiwa na vyombo maalumu vilivyokasimiwa kushughulikia matatizo hayo na si vinginevyo,” amesema Senga

Katika hatua nyingine Kamanda Senga amesema ukiwa ni mwendelezo wa operesheni, na doria  ndani ya mkoa huo, wamefanikiwa kukamata silaha mbili bastola  aina ya Retay G91C ikiwa na risasi 150 kwenye kasha zake tatu.

“Ndani ya begi lake lenye rangi nyeusi, silaha hiyo ilikamatwa Mei 21, 2025 majira ya saa 11:30 jioni kwenye maegesho ya magari maeneo ya majengo ikiwa imetelekezwa,” amesema.

Senga amesema katika uchunguzi wa awali umeonesha silaha hiyo imeingia nchini isivyo halali. Ingawa jeshi hilo linaendelea na msako makali kumtafuta mtu au watu waliohusika na tukio hilo.

Mbali na silaha hizo, Senga amesema silaha nyingine aina ya CZ92 Browning ikiwa na risasi ilikamatwa Mei 14, 2025 saa sita  mchana maeneo ya Black Market Tunduma Wilaya ya Momba.

“Silaha hiyo iliibiwa kwa mmiliki  Emmanuel Fungo katika tukio la kuvunja nyumba mchana na kuiba Mei 13, 2025 tukio hilo lilitokea maeneo ya Haloli Kata ya Vwawa Wilaya ya Mbozi na katika ukamataji mtuhumiwa alikimbia,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *