
KOCHA wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema ndani ya kikosi hicho kuna tatizo kwa wachezaji wake kushindwa kuzuia mashambulizi yanayotokana na mipira ya kutengwa.
Katika mechi nne zilizopita za Ligi Kuu Bara, JKT Tanzania imeruhusu mabao saba ya mipira ya kutengwa.
Kutokana na hali hiyo, Ally amesema atatumia siku chache ambazo ligi imesimama kushughulikia tatizo hilo ili kuona wanamaliza vizuri msimu huu.
Kwa sasa ligi imesimama kupisha mashindano ya Kombe la Muungano yatakayoanza Aprili 23 hadi 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba.
Kwa sasa JKT Tanzania ipo nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 32. Imebakiwa na michezo minne kumaliza msimu, huku hesabu zao zikiwa ni kushika tano bora.
“Kila mechi inakuwa na matukio yake, kuna muda tunapoteza umakini tunafungwa, kuna wakati tunakuwa bora tunashinda, lakini hili la kuruhusu mabao ya frii-kiki nitalifanyia kazi,” alisema Ally.
Mbali na hilo, Ally alisema anachofurahishwa ni namna vijana wake wanavyopambana kutafuta matokeo mazuri akieleza kuwa mipango yake ni kuona timu ikimaliza ligi kwenye nafasi nzuri zaidi ya sasa.
“Tunazo mechi nne zilizobaki ambazo ni za kimkakati sana kwetu, tunaenda kufanyia kazi makosa hayo kuhakikisha tunamaliza michezo hiyo tukiwa ndani ya nafasi tano za juu,” alisema kocha huyo.
Mechi nne zilizobaki kwa maafande hao ni dhidi ya Simba na Fountain Gate watakazocheza nyumbani, kisha kuhitimisha msimu ugenini mbele ya Pamba Jiji na Mashujaa.