Mtazamano wa wengi ulikuwa kwamba ameimudu vizuri: Kansela mpya wa Ujerumani, Friedrich Merz, amefanikisha ziara yake ya kwanza kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, bila mabishano makali wala dosari za kidiplomasia. Ingawa hakuwa na nafasi kubwa ya kuzungumza wakati wa mkutano wa karibu dakika 50 na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, aliweza kusisitiza kwamba Ujerumani itaendelea kuiunga mkono Ukraine katika kujilinda dhidi ya Urusi.
Kwa upande wake, Trump alimchukulia mwanasiasa huyo wa kihafidhina kwa heshima zaidi kuliko alivyowahi kumtendea Kansela wa zamani Olaf Scholz — ambaye hakualikwa hata mara moja White House — au Angela Merkel, ambaye Trump aliwahi kukataa kumsalimia kwa mkono hadharani.
Tangu Mei 6, Merz ambaye ni kiongozi wa chama cha mrengo wa kati-kulia cha Christian Demcoratic Union, CDU, alipoingia madarakani, siasa za Ujerumani zimekuwa na pilikapilika nyingi. Tangu wakati huo, kiongozi huyo mpya wa serikali ya Ujerumani amekuwa akitoa matamko ya kushangaza na tangazo thabiti karibu kila wiki.
Merz: Mwanasiasa asiye na uvumilivu
Hili linakinzana kabisa na mtindo wa mtangulizi wake, Scholz wa chama cha SPD, ambaye alijulikana kwa tabia yake ya kutokuwa muwazi kwa umma kuhusu mipango yake. Scholz aliwahi kuwaagiza wafanyakazi wake kufuata kauli mbiu: “Hatutashtuka, hatutakuwa na hofu.” Kwa maneno mengine, alilenga kuonyesha utulivu.
Merz, kwa upande mwingine, hakuwahi kuficha kukosa subira kwa muda mrefu kabla ya kupata wadhifa aliouhitaji sana. Mnamo 2002, alipoteza mchuano wa uongozi wa CDU dhidi ya Merkel. Akiwa na machungu, alihamia sekta binafsi na kurejea tena katika siasa ilipodhihirika kuwa Merkel anapanga kung’atuka mwaka 2021.
Miaka minne baadaye, akiwa na umri wa miaka 69, hatimaye alifikia kilele cha mamlaka nchini Ujerumani. Hii ndiyo nafasi yake ya kwanza ya kuchaguliwa au kushika wadhifa wa serikali maishani mwake.
Scholz na Merz ni watu wa tabia tofauti kabisa. Scholz ni mtu wa maneno machache, mpole, kutoka Kaskazini mwa Ujerumani, mwenye uzoefu mkubwa serikalini kabla ya kuwa Kansela. Aliwahi kuwa Meya wa Hamburg na baadaye Waziri wa Fedha katika serikali ya Merkel.
Kwa upande mwingine, Merz, ambaye kiasili ni mhafidhina na anayekasirika kirahisi, alipanda kwa kasi ndani ya chama chake bila kuwa na uzoefu wa utawala wa kisiasa. Pia, wawili hao hawapendani sana.
Mhariri Mkuu wa Siasa wa DW, Michaela Küfner, anawajua vyema viongozi hao wawili, baada ya kuwasindikiza katika safari nyingi za nje. Akitafakari kuhusu mitindo yao tofauti, alisema: “Wakati Merkel daima alikuwa akifikiria matokeo na Scholz alikuwa akisita hata kueleza lengo lake la kisiasa kabla ya kuandaa njia ya kulifikia, Merz anaweka wazi malengo yake.” Kwa mujibu wa uchambuzi wa Küfner, hili linaashiria mabadiliko makubwa ya mtindo wa kisiasa.
Sera kuhusu Ukraine
Ilichukua muda hadi majira ya kiangazi ya 2022 kwa Scholz kuitembelea Ukraine, iliyokuwa imevamiwa na Urusi mnamo msimu wa baridi mwaka huo. Kwa muda mrefu, Scholz alibaki kuwa msiri kuhusu kama angepeleka silaha kwa nchi hiyo — ingawa mwishowe alifanya hivyo.
Merz, kwa upande mwingine, alizuru Ukraine ndani ya siku chache baada ya kuingia madarakani, akiwa pamoja na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, na Waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk, walipotangaza kwamba makubaliano ya kusitisha vita na mazungumzo ya amani yangekuja hivi karibuni.
Hata hivyo, hilo bado halijatimia, huku Rais Trump akiwa ameonekana kujiondoa kwenye ahadi yake ya awali ya kuleta amani ya kudumu. Kutokana na kutotabirika kwa Rais huyo wa Marekani, hili halikuwa jambo la kushangaza — jambo ambalo Scholz angalizingatia mapema.
“Baada ya onyesho imara pamoja na Macron, Tusk na Starmer, ikaja aibu ya kidiplomasia,” anasema mwandishi wa DW mjini Berlin, Küfner. “Merz bado anapaswa kuthibitisha kuwa kushindwa huku kunaweza kubadilishwa kuwa uongozi imara.”
Ujerumani na Israel
Mabadiliko ya mtindo wa sera ya Ujerumani kuhusu Israel ni dhahiri zaidi. Baada ya wanamgambo wa kundi la Hamas kuishambulia Israel mnamo Oktoba 2023, Scholz alisisitiza haki ya Israel kujilinda.
Msimamo huo uliendelea hata wakati jeshi la Israel lilipoanza kushambulia vikali raia wa Ukanda wa Gaza. Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa mengine kadhaa yanaitambua Hamas kuwa ni kundi la kigaidi.
Wakati huo akiwa kiongozi wa upinzani, Merz pia aliunga mkono Israel kwa nguvu, na hata kutangaza kwamba tofauti na Scholz, angeonesha uungaji mkono wake kwa kumwalika Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu katika Ikulu ya Kansela.
Msimamo huu haukubadilika hata baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague kutoa waranti wa kukamatwa dhidi ya Netanyahu mwezi Novemba mwaka jana kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Lakini siku chache baada ya kuingia madarakani, Merz alibadilika ghafla: hivi karibuni alisema kuwa haelewi tena hatua za Israel katika vita vya Gaza, na kuongeza kuwa sasa haziwezi tena kuhalalishwa kama mapambano halali dhidi ya ugaidi wa Hamas. Haijawahi kutokea kabla kansela wa Ujerumani kusema kwa uwazi namna hii kuhusu hatua za serikali ya Israel.
“Ukosoaji wa Merz kuhusu hatua za Israel huko Gaza ni hatua ya kihistoria,” anasema Küfner. “Hana hofu ya kumkosoa moja kwa moja Waziri Mkuu wa Israel kuhusu madai ya ukiukaji wa sheria za kimataifa. Huu ni mwelekeo mpya kutoka Ujerumani.”
Kwa hili, Merz ameibua swali ambalo Scholz aliweza kuepuka kwa mafanikio: Je, dhamira ya Ujerumani kuiunga mkono usalama wa Israel inafikia wapi hasa?
Hii itamaanisha nini kwa mahusiano ya Ujerumani na Israel kwa vitendo bado haijulikani. Hata enzi za Scholz, usafirishaji wa silaha kwenda Israel ulikuwa mdogo, na Merz hajatangaza kumaliza kabisa usafirishaji huo. Pia hajarudia tena mwaliko wake wa awali kwa Netanyahu.
Kwa upande wa vitendo, mabadiliko si makubwa sana — lakini mtindo wa mazungumzo ni tofauti kabisa. Hali hii huenda ikaendelea katika wiki zijazo. Ujerumani italazimika kuzoea mtindo huu mpya wa kisiasa wa Kansela wake mpya. Wakati huo huo, Scholz sasa anafuatilia yote haya akiwa mbunge wa kawaida katika Bundestag — na bado hajatoa maoni yoyote kuhusu sera za mrithi wake.