
KIUNGO mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Fredrick Magata anasubiri kwa hamu kuandika historia tamu ya maisha yake kwa kuhusika katika kuzipandisha Ligi Kuu Bara timu mbili tofauti.
Timu yake ya sasa, Mtibwa imebakisha pointi tatu tu kurejea Ligi Kuu msimu ujao, jambo ambalo litakuwa ni mara ya pili kwa nyota huyo baada ya msimu wa 2021-22 kuipandisha daraja Mbeya Kwanza.
Mtibwa jana iliibwaga Mbeya Kwanza 1-0 na sasa inahitaji pointi tatu tu kati ya 9 katika michezo mitatu iliyobakia ili kurejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao, kwani itafikisha 69, ambazo hazitafikiwa na timu yoyote.
Iko hivi! Mbeya City iliyopo nafasi ya pili na pointi 59, nyuma ya Mtibwa yenye 66, ikiwa itashinda michezo yake yote mitatu iliyobakia itafikisha 68, huku Stand United inayoshika ya tatu na pointi 55, ikishinda mechi nne itakuwa na 67.
Magata anayeitumikia timu hiyo kwa msimu wa pili sasa tangu ajiunge nayo akitokea Mbeya Kwanza, alisema anaamini ndoto hiyo inaweza kutimia, ndio maana wao kama wachezaji wenyewe wanahamasishana kukipambania kikosi hicho ili kirejee tena.
Mtibwa iliyocheza michezo 27, imeshinda 21, sare mitatu na kupoteza mitatu, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao 53 na kuruhusu 15, ikiwa kileleni mwa msimamo wa Championship na pointi 66.