
MCHEZO wa Ligi Kuu Soka Wanawake kati ya JKT Queens dhidi ya Fountain Gate Princess uliofanyika leo Jumamosi Mei 17,2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, umeshindwa kuendelea kipindi cha pili.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, wenyeji JKT Queens walikuwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Anastazia Katunzi, Jamila Rajabu na Stumai Abdalah.
Sababu za kutoendelea kwa mchezo huo ni kitendo cha Fountain Gate Princess kutorudi uwanjani kipindi cha pili, huku ikidaiwa timu hiyo haikuridhishwa na uamuzi wa waamuzi katika baadhi ya matukio.
Kocha wa JKT Queens, Ester Chaburuma, ameliambia Mwanaspoti kuwa, hawafahamu nini kiliwakuta wapinzani wao kwani wao waliporudi uwanjani kwa ajili ya kuendelea na kipindi cha pili, wenzao hawakutokea.
“Hatujui nini kiliwakuta (Fountain Gate Princess) kwa sababu walicheza vizuri sana kipindi cha kwanza.
“Baada ya kurudi kipindi cha pili, waamuzi wamefanya kama ilivyotakiwa kukaa muda husika na timu pinzani haikutokea, wakaondoka,” amesema Chaburuma.
Mwanaspoti lilimtafuta Kocha wa Fountain Gate Princess, Mirambo Camil kwa njia ya simu, lakini iliita bila ya kupokewa huku mtu mmoja wa benchi la ufundi la timu hiyo akisema waliona kuna uonevu kutokana na kuonewa katika baadhi ya matukio huku akisema mabao ya JKT Tanzania hayakuwa sahihi.
Kabla ya mchezo huo, JKT Queens ilikuwa kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 41 sawa na Simba Queens lakini zilitofautishwa na mabao ya kufunga na kufungwa.
Wakati hali ikiwa hivyo, mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha TFF uliopo Kigamboni, Dar, Simba Queens imeondoka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Bunda Queens.
Mabao ya Simba Queens yamefungwa na Asha Djafar, Aisha Juma na Janet Nyagali, huku yale ya Bunda Queens wafungaji ni Monica Samwel na Jenipher Dominic.
Kwa ushindi huo, Simba Queens imefikisha pointi 44 baada ya kucheza mechi 17, ikibakiza mechi moja ugenini dhidi ya Alliance Girls ili kuhitimisha msimu huu.