
Dar es Salaam. Timu ya Fountain Gate imeendeleza ubabe dhidi ya KMC baada ya kuifunga mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
KMC ndiyo ilikuwa ya kwanza kuandika bao katika dakika ya 45 kupitia kwa Oscar Paul ambaye alifunga kwa mkwaju wa penati baada ya golikipa wa Fountain Gate, Fadhil Kisunga kumchezea vibaya Darueshi Saliboko.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinakamilika KMC iliondoka kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza huku Fountain Gate ikionekana kutengeneza nafasi nyingi za kutafuta bao la kusawazisha.
KMC iliendelea kuzuia mashambulizi ya Fountain Gate lakini hisivyokuwa bahati Elie Mokono alifunga bao la kusawazisha katika dakika ya 78 kabla ya kufunga linguine la ushindi dakika ya 90+4.
Mokono ambaye aliingia kutokea benchi alionyesha kiwango bora na kuihakikishia Fountain Gate kupata pointi tatu muhimu katika uwanja wa ugenini.
Baada ya matokea ya mchezo wa jana Fountaine Gate inasogea mpaka nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikifikisha jumla ya pointi 28 ikiwa imeshinda mechi nane, sare mechi nne na kufungwa mechi 11 katika mechi 23 ilizocheza.
KMC yenyewe imeshuka mpaka nafasi ya 12 ikiwa na pointi 24 baada ya kushinda jumla ya mechi sita, sare mechi sita huku ikipoteza mechi 11 katika mechi 23 ilizocheza.
Baada ya mchezo kumalizika makocha wa pande zote mbili walielezea mchezo ulivyokuwa huku kocha wa Fountain Gate, Roberto Matano akitambia uwepo wa wachezaji chipukizi wanaokipa nguvu kikosi chake.
“Wote ni wachezaji wangu nimefurahia sana kuwaona wachezaji wangu wadogo wakifanya vizuri na timu lazima tucheze kwa uzoefu hata kama wachezaji bado wadogo.
“Hawa wachezaji wadogo wanakimbia haraka na wametusaidia kuifungua safu ya ulinzi ya KMC na tumepata matokeo bora,” amesema Robert Matano.
Kocha msaidizi wa KMC, John Matambala amekubaliana na matokeo ya mchezo huku akielezea kupeleka nguvu katika michezo iliyobaki.
“Mchezo huu tumepoteza, tunakwenda kuangalia wapi penye makosa ili tufanye vizuri katika mechi zinazokuja. Bahati haikua upande wetu leo hivyo tunajipanga kwenye mechi nyingine zinazokuja,” amesema John Matambala kocha msaidizi wa KMC.
Matokeo ya mechi nyingine za Ligi Kuu zilizocheza jana
Namungo 0 vs 1 Singida BS
Azam FC 4 vs 0 Tanzania Prisons