
UWANJA wa Tanzanite Kwaraa, uliopo mjini Babati mkoani Manyara, leo Jumatatu utaamua jambo kubwa wakati wenyeji Fountain Gate watakapowakaribisha vinara wa Ligi Kuu Bara, Yanga.
Ni mchezo wa raundi ya 27, huku ukiwa ni mchezo wa 26 kwa Yanga ambayo inaongoza msimamo kwa pointi 67.
Umuhimu wa mchezo huu unakuja na hesabu tatu kutokana na kila timu kuhitaji alama za kuiweka sehemu nzuri kwenye msimamo ambapo kuna hesabu tofauti.
Hesabu ya kwanza Yanga inahitaji ushindi kuendelea kujikita zaidi kileleni mwa msimamo juu ya Simba inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 10, ingawa wapinzani wao hao wana michezo mitatu pungufu yao.
Pili, Fountain inahitaji alama tatu za kuisogeza juu kwenye msimamo, kwani hivi sasa inashika nafasi ya 10 kwa pointi 28 kabla ya mchezo wa Namungo dhidi ya Mashujaa uliochezwa jana Jumapili usiku.
Ukiachana hesabu hizo mbili, ishu ya tatu Fountain wanataka kulipa kisasi cha kufungwa 5-0 duru la kwanza walipokuwa ugenini kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar, Desemba 29, 2024. Hayo yote mwamuzi ni dakika tisini za mchezo huo.
“Tumejiandaa kushinda, Yanga inafungika vizuri tu, tunawakaribisha Tanzanite Kwaraa waje tuwaonyeshe kazi,” alisema Ofisa Habari wa Fountain, Issa Liponda ‘Mbuzi’.
Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi nzuri ya timu iliyoshinda mechi nyingi ugenini kwenye ligi hiyo msimu huu ambazo ni 12 kati ya 13, haijapoteza zaidi ya kutoka suluhu na JKT Tanzania.
Kupitia mechi hizo za ugenini pekee, Yanga imekusanya pointi 37 ambazo ni nyingi kuliko zile za nyumbani 30, huku pia ikifunga mabao 31 na kuruhusu mawili pekee.
Takwimu hizo zinaonyesha uimara wa Yanga kwenye viwanja vya ugenini kitu ambacho kinaiweka katika hatari kubwa Fountain ikiwa na jukumu la kuwazuia mabingwa hao watetezi.
Wenyeji Fountain rekodi za uwanja wa nyumbani zinaonyesha ni timu ambayo haina matokeo mazuri sana ikishinda tano, sare nne na kupoteza nne katika mechi 13 huku ikifunga mabao 14 na kuruhusu 14.
Mechi zao tano za mwisho nyumbani, Fountain Gate wameshinda moja, wakipoteza mbili na sare mbili.
Elie Mokono ndiye mchezaji tegemeo akionyesha makali yake duru la pili akifunga mabao manne kati ya sita yaliyopatikana, huku jumla akifunga sita na ndiye kinara kikosini hapo sawa na Seleman Mwalimu ambaye Januari mwaka huu alitimkia Wydad Casablanca ya Morocco.
Mbali na Mokono, Salum Kihimbwa aliyehusika kwenye mabao tisa akifunga manne na asisti tano, ni mchezaji mwingine wa kutumainiwa kikosini hapo, mbali na Edger Williams mwenye mabao matano, japo hajafunga muda mrefu kwani alifunga mara ya mwisho Desemba 13 mwaka jana wakati wakiichapa Coastal Union mabao 3-1, kitu kilichomfanya waliokuwa nyuma yake kumfikia na kupita idadi hiyo.
Kocha wa Fountain Gate, Robert Matano, alisema: “Lazima tupigane mpaka mwisho, tunapaswa kuongeza juhudi kwani ligi haijaisha, wakati kama huu ndiyo mashabiki wanapaswa kuja kwa wingi kutusapoti.”
Upande wa Yanga, jeuri yao kubwa inaanzia kwenye ulinzi hadi ushambuliaji kufuatia maeneo hayo kuwa imara zaidi kwa sasa.
Ikiwa imefunga mabao 64 yakiwa mengi zaidi kuliko timu nyingine kwenye ligi hiyo msimu huu, pia imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10, ni timu ya pili iliyoruhusu mabao machache nyuma ya Simba (8).
Takwimu hizo zinaipa Yanga nafasi kubwa ya kupata bao kwani ina wastani wa kufunga mabao 2.6 kwa mechi huku kujilinda ikiwa imara wastani wake ni 0.4.
Kupitia washambuliaji Prince Dube mwenye mabao 12 na Clement Mzize (11), Yanga inaonekana eneo lake la mbele ni hatari zaidi, huku pia ulinzi chini ya kipa DJigui Diarra mwenye clean sheet 13, mbili nyuma ya kinara Moussa Camara wa Simba (15), inamtoa wasiwasi kocha wa kikosi hicho, Miloud Hamdi ambaye hata hivyo anafahamu kucheza ugenini ni ngumu zaidi ya nyumbani.
Fountain Gate takwimu zinawabana, kwani mechi 26 wamefunga mabao 29 kwa wastani wa 1.1, huku ikiruhusu 47 kwa wastani wa 1.8.
MTIHANI WA KENGOLD
Upande mwingine, mchezo wa Coastal Union dhidi ya KenGold, umeshikilia hatma ya timu mojawapo kuwepo Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Pindi mwamuzi wa mchezo huu atakapopuliza kipyenga cha mwisho kuashiria kukamilika kwa dakika tisini, tunaweza kupata majibu ya hatma ya KenGold kwani ikipoteza, moja kwa moja itakuwa imeshuka daraja.
Pointi 16 ilizonazo KenGold kwa sasa, zinaifanya timu hiyo kulazimika kushinda mechi zote nne zilizobaki ili kufikisha 28, huku ikiziombea mabaya Kagera Sugar (22), Tanzania Prisons (27) na Pamba Jiji (27).
Ikiwa kinyume chake kwa maana ikipoteza mbele ya Coastal Union, KenGold itabakiwa na mechi tatu ambazo hata ikishinda zote itaishia pointi 25 zitakazowaacha kusalia nafasi mbili za chini kwenye msimamo, hivyo maana yake itakuwa imeshuka.
“Tupo kwenye hali mbaya, tunaangalia wapinzani wetu waliopo juu mechi zao zitakuwaje ili sisi kuwa salama ila kiuhalisia ni ngumu, lakini hatujakata tamaa, bado ligi haijaisha,” alisema Kocha wa KenGold, Omary Kapilima.
Coastal Union iliyokuwa na mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha, mara ya mwisho imetoka kuichapa Singida Black Stars mabao 2-1 kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Mkwakwani ambao imeutumia kwa mara ya kwanza baada ya kumalizika marekebisho.
Kwenye uwanja huo, itaikaribisha KenGold ambayo haijashinda mechi yoyote ya ugenini msimu huu kati ya 13 ikipoteza 11 na sare mbili.
Coastal Union inahitaji kushinda mechi hii ili kuzidi kujiweka eneo zuri kwenye msimamo, pointi 28 ilizonazo bado inaiweka kwenye hatari ya kushuka daraja, hivyo ikishinda itafikisha 31 na kupanda hadi nafasi ya nane kutoka ya 11. Hiyo itategemea na matokeo ya Namungo dhidi ya Mashujaa waliocheza jana Jumapili.@@@@@