
Dar es Salaam. Timu ya Fountain Gate leo itakuwa inaikaribisha Tabora United kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati katika muendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara huku ikitafuta ushindi wa kwanza katika mwaka 2025.
Katika mchezo wa leo utakaochezwa saa 10:00 jioni Fountain Gate itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu ya kutopata ushindi kwenye mechi tano za mwisho huku mara ya mwisho kupata ushindi ikiwa ni Desemba 13, 2024 iliposhinda mabao 3-2 dhidi ya Coastal Union.
Baada ya ushindi huo dhidi ya Coastal Union, Fountain Gate haijawai kupata ushindi mwingine ikiwa imefungwa mechi nne na kupata sare mechi moja dhidi ya Simba.
Katika mechi hizi tano za mwisho Fountain Gate imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13 huku yenyewe ikifunga mabao mawili.
Fountain Gate inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 21 baada ya kushinda mechi sita, sare mechi tatu na kufunga mechi 10 katika mechi 19 ilizocheza.
Kwa upande wa Tabora United yenyewe inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi 32 baada ya kushinda mechi tisa, sare mechi tano na kupoteza mechi tano katika mechi 19 ilizocheza.
Offen Chikola mwenye mabao sita na pasi mbili za mwisho sambamba na Heritier Makambo mwenye mabao matano ndiyo wachezaji wa kuchungwa wa Tabora United wakati Edgar William wa Fountain ambaye ana mabao matano atawaongoza wenyeji katika harakati za kuondoa jinamizi la vipigo.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana Septemba, 20, 2024 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora wageni Fountain Gate walishinda kwa mabao 3-1.